Anita anakubali kuolewa na Martin baada ya mpenzi wake Owen kwenda ujerumani kikazi kwa kipindi cha miezi nane bila mawasiliano.
Baada ya harusi kufungwa ndipo Owen anarejea na kueleza ni kipi kilicho mkuta huko ujerumani hadi kukata mawasiliano na Anita.
Lakini Anakuta Ameshachelewa kwani tayari Anita ni mke wa mtu. Hii haimfanyi aache kumpenda kwani wanakutana tena na kuendeleza penzi lao kisiri bila hata ya Martin kujua.
Mambo yanaanza kwenda vibaya baada ya ujio wa Kaylah ambae ni mdogo wa Martin. Owen anavutiwa nae na taratibu anaanza kumpenda kiasi cha kuwa kichaa.
Je Anita atakubali wifi yake amnyang’anye tonge lake mdomoni?? Na Je Kaylah atafanya nini pindi atakapojua kwamba Owen ndio mchepuko wa Wifi yake unao fanya kaka yake asifuraie ndoa yake???
Baki na mimi……..
SEHEMU YA :01
Ilikua ni siku nzuri sana ya harusi takatifu baina ya Martin na Anita. Maandalizi yalishakamilika na shamra shamra zilikua za kutosha sana siku hiyo hasa kwa upande wa Martin.
Ila kwa Anita mambo yalikua tofauti kidogo. Toka panakucha asubui alikua amejawa na huzuni mno na kila dakika alikua akitoa machozi hadi mpaka make-up akashindwa namna ya kumpendezesha bibi harusi wake.
“Ngoja nikupishe kidogo ukikaa sawa utaniita” mpaka make-up alitoka nje kisha Anita akawa amebaki peke yake mule ndani.
Basi Anita akiwa anazidi kulia mara akaingia Nadia ambae ni rafiki yake mkubwa sana.
“Bado unalia Anita??” Nadia alishangaa
“Roho inaniuma, nahisi kabisa sijafanya jambo zuri”
“Upo sahihi wala hata hujafanya jambo baya! Endelea na maisha yako na kama kuolewa na Martin ndio namna ya kuendelea na maisha yako basi mimi Nadia nakusapoti kwa asilimia 100%”
“Lakini bado nampenda Owen! Nampenda sana” Anita alizungumza huku machozi yakizidi kumtoka
“Shiiii! Ongea taratibu au unataka kila mtu asikie jamani??”
“Hata wakisikia mimi sijali”
“Anita acha ukichaa ujue! Huyo Owen angekua hai ama angekua na mapenzi ya dhati na wewe angeshakupigia simu kitambo sana! Ni miezi nane sasa imepita toka aende Ujerumani mbona hadi sasa tusisikie chochote kuhusu yeye”
“Huwezi jua labda amepatwa na matatizo huko”
“Amepatwa na matatizo ndo asipige simu! Hapa kuna mawili shoga yangu, yawezakana hayupo hai ama kashajipatia jimama lake la kijerumani lina mlea huko wewe upo hapa kazi yako kulia lia tu”
“Nadia please usiseme ivo”
“Anita, utampata wapi kijana kama Martin?? Anakupenda na anakuhudumia kwa kila kitu. Ama unataka urudi kuuza miwa barabarani?? Huyu ndie mwanaume anae kufaa achana kabisa na habari za Owen”
“Sawa basi naomba simu angalau nijaribu kumpigia huenda akapokea Nadia”
“Heee kumbe ninacho kizungumza hapa hukielewi?”
“Naelewa ila angalau nimpigie ndipo nipate uhakika zaidi kama nafanya kitu sahihi au laah!”
“Okay” Nadia alifungua pochi akatoa simu na kumpa Anita.
Pale pale Anita akaanza kuzipiga namba za Owen kupitia whatsapp na simu isipokelewe. Akatuma tena meseji nyingine ndefu akimpa taarifa kuwa anaolewa na hata ile meseji haikusomwa! Ni wazi Owen hakua tena online kama ilivyo kuwa miezi nane iliyo pita.
“Umeona sasa? Kujichosha tu!” Alisema Nadia akiwa kabinua midomo juu
“Kama ndo ivyo naenda kuolewa na Martin kwa moyo mmoja bila hata kinyongo” Anita alijifuta machozi yake taratibu huku akijitazama kwenye kioo.
“Unasema kweli?? Ayoo ndo mambo niyapendayo! Ngoja nikamuite yule binti aje kukupodoa maana muda umeshaenda kweli na unatakiwa kanisani saa nane na nusu” Nadia alitoka mbio mbio kwenda kumleta mpambaji kisha shughuli ikaendelea kama kawaida.
Baada ya kumaliza kupambwa Anita alivalishwa gauni zuri leupe huku Nadia akimalizia kumvalisha shela kama rafiki yake maana Kwa bahati mbaya Anita hakuwa na ndugu wala wazazi.
Walipomaliza hapo safari ya kuelekea kanisani ikaanza. Japo Anita alikubali kuolewa na Martin kwa moyo mmoja ila bado furaha ilimpotea kabisa.
Wakati Nadia na wengine wakifuraia yeye alitulia kimyaa akimkumbuka Owen na jinsi penzi lao namna lilivyokua tamu.
Ni miaka kadhaa nyuma Owen na Anita walikutana katika kituo cha watoto yatima huko Good Hope Arusha. Toka siku ya kwanza wanajuana walikua karibu sana kiasi cha watu kudhani pengine ni ndugu.
Lakini kadri siku zilivyozidi kwenda ndivyo kila mmoja kati yao alianza kujenga hisia kwa mwenzake na mwisho wa siku wakashindwa kujizuia na kuamua kuingia kwenye mahusiano ya kimapenzi.
Walipendana sana na hata siku walipokuwa wanaondoka kwenye kituo cha Good Hope watu hawakutaka waondoke maana penzi lao lilikua likiwavutia vilivyo.
Basi Owen na Anita wakatoka Arusha na kuhamia Dar ambapo huko ndipo walipoanzisha maisha yao. Owen yeye alikua fundi magari na Anita alikua muuza miwa mtaani.
Hawakua na pesa ila walipendana mno na chochote kidogo walicho kipata waliridhika nacho. Ila Owen alitaka maisha mazuri zaidi ili kusudi Anita asiendelee kuteseka, ivyo akaanza harakati za kutafuta kazi nyingine ambayo alihisi ingempa mafanikio zaidi.
Kwenye harakati za kutafuta kazi nyingine Owen akagusiwa kuhusu kazi ya meli huko ujerumani, na mshahara wake kwa siku ulikua ni mkubwa kiasi cha Owen kutamani kwenda ujerumani.
“Hapana hakuna kwenda!” Anita alikataa
“kwanini sasa?”
“we ukiondoka mimi nitabaki na nani?? Nitaishije?”
“Sikai mda mrefu! Miezi sita tu kisha narudi”
“Hapana, mimi sitaki” Anita alisimamia msimamo wake
“Kwani unayafuraia haya maisha? Ya ugumu? Tunashindia na kulalia mchicha mpaka lini?? wewe mwenyewe hapo huna hata mafuta ya kupaka! Unadhani nina amani moyoni kuona jinsi unavyo teseka??” Owen aliongea kwa uchungu akimtazama Anita
“Mimi naogopa ukienda huko hutarudi tena, unaweza ukapata mwanamke wako hadii ukasahau kabisa kuhusu mimi”
“Ilo haliwezi kutokea! Tumetoka mbali na tumependana toka tupo wadogo unadhani naweza sahau penzi letu kwa mtu ambae nimekutana nae leo tu??”
“Bado sitaki”
“Anita Mama! Nakuahidi kila kitu kitakua sawa! Nakupenda sana na ninaomba ukubali, sifanyi hivi kwaajili yangu bali kwaajili yako pia”
Anita alivuta pumzi kwa nguvu na kushusha kisha akamshika Owen mkono na kumuambia
“Kama utaenda huko sawa ila hakikisha kila dakika ukipata nafasi utanipigia simu! Unanielewa?”
“Sawa Madam”
Walikumbatiana kwa furaha kisha siku iliyofuata Owen akaanza process za kwenda Ujerumani. Kampuni ya meli ilimtumia hela ya safari ivyo Owen hakuumiza kichwa chake juu ya namna ambavyo angefika ujerumani.
Baada ya kila kitu kukamilika Owen akaenda ujerumani huku Anita akiendelea kubaki Tanzania akiuza miwa mtaani.
Wiki mbili za kwanza za Owen kwenda ujerumani zilikua ni nzuri maana kila wakati alikua akiwasiliana na Anita. Ila baada ya hizo wiki kupita mambo yalibadilika ghafla na Owen hakuwa akipatikana hewani.
Anita akiwa yupo kwenye wakati mgumu kihisia ndipo Martin akaingia kwenye maisha yake. Toka siku ya kwanza Martin alionyesha wazi kumpenda Anita ila ndo ivyo Anita hakuonyesha kama yupo tayari kuwa na mwanaume mwingine maana bado alikua na matumaini kuwa Owen angerejea.
Ila baada ya miezi sita kupita na kuona bado Owen hakua amerejea ndipo Anita akaamua kumpa nafasi Martin. Tena hapo Nadia alimshawishi sana na kumpigia kelele za hali ya juu.
Kwaiyo Badala ya kuolewa na Owen kama ilivyo kuwa ahadi yao, Anita alikwenda kuolewa na Martin. Basi Anita alipokumbuka yale yote machozi yakaanza kumtoka tena.
Je nini kitaendelea????”
Nakuja……….
SEHEMU YA : 02
“Wewe unalia lia nini?” Nadia alimuuliza kwa sauti ya chini iliyojaa ukali ndani yake
“amna”
“Amna wakati unalia hapo? Anita jamani si tumeshazungumza kuhusu ili? Ama bado kichwa chako kinamuwaza uyo mjinga wako”
“Sio ivyo”
“Tena acha kulia haraka maana tumeshafika kanisani”
Anita alipo peleka macho yake nje kweli akaona tayari walishafika kanisani. Aliinama kidogo akajifuta machozi yake kwa juu ili asiharibu make-up ndipo akakaa sawa.
Huko ndani kanisani mambo yalizidi kuwa moto! Martin ndani ya suti yake nyeusi yenye kamng’ao kwa mbali alisimama akitazama mlangoni kwa shauku ya kumuona mkewe mtarajiwa.
Maskini hakujua kabisa kama mkewe huyo moyo wake ulikua kwa mwanaume mwingine, pengine angelijua hilo mapema angemuacha Anita na kutafuta mwanamke mwingine.
Basi kwa mbali lango la kanisa likafunguliwa, Anita akaingia akiwa ana meremeta kama dhahabu. Martin kumuona namna alivyo pendeza akazidi kutabasamu na kukubali kweli anakwenda kuoa chombo.
Bila kuchelewesha Mda Padri akafungisha ndoa ile takatifu na rasmi kisheria na hata mbele ya Mungu Martin na Anita wakawa mke na mume.
Kisha baada ya kiapo kanisani sherehe ikaenda kumalizikia ukumbini. Watu walikula wakanywa na kuserubuka utadhani wasinge iona siku ya kesho.
Lakini bado Anita alikua mnyonge, kwa kiasi flani furaha ya Martin ikawa inamkera na namna alivyo mtazama ni wazi hakua na hisia nae hata kidogo.
Basi baada ya sherehe ya harusi siku iliyofuata wana ndoa walitakiwa kwenda honeymoon huko Zanzibar. Ingekua ipo ndani ya uwezo wa Anita basi asingekubali kwenda honeymoon ila kwakua haikua ndani ya uwezo wake ilimpasa tu aende pasipo kupenda.
Wakati Anita anakwenda honeymoon na mumewe nae Owen ndio alikua akirejea kutoka Ujerumani. Sura yake na muonekano wake tu ulitosha kuashiria kuwa ni mambo mengi mazito aliyo pitia huko ujerumani.
Hata afya yake ilidorora sana na mvuto alipoteza, lakini hakuonyesha kama alijali. Yeye alichokuwa anakiwaza akilini mwake ni Anita tu.
Ali mmiss sana mpenzi wake na alitamani mno kama angemuona tu angalau amkumbatie maana ilipita kipindi kirefu bila wao kuonana.
Basi baada ya kutoka uwanja wa ndege alichukua usafiri mpaka nyumbani ambapo walipokuwa wakiishi zamani.
Owen alipofika mtaa mzima ukaanza kuzizima kwa ujio wake hata habari zikasambaa haraka na kumfikia Nadia akiwa saluni kwake.
“Unasemaje eti??” Nadia alihisi labda hajasikia vizuri
“Ndio! Owen karudi”
“Acheni utani bhana Owen kafia huko ujerumani nani asie jua kuhusu ilo?”
“Nadia unakataa nini wakati sisi ndo tulio muona! Ni Owen kabisa sema kakonda kanyooka kawa kama rula! Yani hatamaniki”
“mmemuonea wapi kwani??” Ilikua ngumu kwa Nadia kuamini
“pale walipokuwa wanaishi zamani”
“Ngoja nikamuone”
Nadia hakutaka kuyakubali kirahisi maneno ya kuambiwa. Alirudishia mlango wa saluni yake haraka haraka, kisha huyoo akaelekea alipo ambiwa Owen yupo.
Alipokua anakaribia kwa mbali aliona kikundi cha watu na kwa pembeni alimuona Owen akiwa amekaa chini huku mikono kaiweka kichwani.
Nadia aliongeza mwendo hadi alipomfikia na kumtazama kwa ukaribu zaidi ndipo akajihakikishia kweli ndie Owen.
“Heeee? Wewe? Sisi tumejua umekufa??”
Sauti ya Nadia ilimtoa Owen kwenye wimbi la mawazo na kwa hasira akajikuta ameikamata mikono yake kwa nguvu.
“Anita yupo wapi??? Yupo wapi Anitaaa!”
“Nini?? Mimi najuaje??”
“Nadia usicheze na akili yangu! Anita yupo wapi?? Niambie” Owen alizidi kuibinya mikono ya Nadia kwa nguvu ndipo Nadia akaona ni heri aseme ukweli tu
“Kaenda Honeymoon na mumewe! … aya niachie… unaniumiza Owen”
Majibu ya Nadia yalimvunja moyo Owen na taratibu alimuachia Nadia kisha akarudi tena kukaa chini. Alidhani majirani walimdanganya ila baada ya kuthibitishiwa na rafiki yake ndipo akapata uhakika zaidi kuwa ua lake la moyo ni mali ya mwanaume mwingine.
“Hata usiumie Owen hiyo yote ni makosa yako. Umeenda Ujerumani miezi yote hiyo bila hata ya kupiga simu unadhani sisi tungejuaje kama upo hai?? Anita alidhani umekufa au umepata mke huko ujerumani ndo maana na yeye akaendelea na maisha yake” Nadia alisema vile makusudi ili azidi kumchoma roho Owen
“Hata kama! Hata kama! Ameshindwa kunisubiri na akaona ni heri aolewe?? Kwani miezi nane ni mingi jamani??” Owen alitoa chozi
“We unaona ni michache ila kwake ilikua ni mingi. Kashaolewa sasa ivi naomba na wewe uendelee na maisha yako!”
Owen hakumjibu Nadia badala yake alisimama na kuondoka kuelekea kwa rafiki yake Chaz ambae walikua wakifanya wote kazi gereji kabla ya kwenda ujerumani.
Chaz alipomuona jamaa yake alifurai mno, alikwenda akamkumbatia kwa nguvu kisha akampa kiti wakae ili wapate kuongea mawili matatu.
“Najua tayari umeshapata habari za Anita kuolewa” aliongea Chaz akimuangalia msela wake kwa huruma
“Ndio. Ni kitu cha kwanza walicho nambia”
“Ndo ivo! Demu alishindwa kusubiri urudi akaolewa na jamaa flanii ivii anapesa mbaya! Alafu harusi ilikua juzi hapa watu wakala na kunywa”
“Usiniambie tena bro, moyo wangu unachoma sana!”
“fresh tu ila jamaa kwa kiasi flani na wewe ulizingua pia! Ukapotea kabisa huko bila mawasiliano we unadhani mchumba angefanya nini?” Alisema Chaz
“sikupenda bro”
“Nini kili kukuta huko maana hata afyaa imepotea kabisa”
“Acha tu! Sina nguvu hata ya kuanza kusimulia! Ila jua tu mambo sio mambo! Apa nilikua jela huko ujerumani ndo nimetolewa juzi na kukatiwa tiketi ya kurudi moja kwa moja Tanzania” aliongea Owen kwa huzuni
“Kwani ilikuaje??”
“Ile meli tuliyokua tunafanya kazi ilikua na madawa ya kulevya ambayo walikua wanasafirisha kwa siri! Kwaiyo sisi hatukua tukijua chochote zaidi ya kufanya kazi kama kawaida ndipo tulipo pigwa ambush na mapolisi. Wote kwenye ile meli tukatiwa ndani kisha uchunguzi ukawa unafanyika taratibu na watu walikuwa wanatolewa wachache iwapo tu, ukikutwa huna kosa. Mimi zamu yangu ilikua ni juzi! Na sikutaka kumpigia Anita na kumuambia kuwa nilikua jela we unadhani angejisikiaje??”
Chaz akashindwa la kusema akabaki akimtazama Owen kwa huzuni mno maana stori yake ilijua kumuumiza.
Je nini kitaendelea???
Nakuja………….
SEHEMU YA : 03
“Pole jamaa angu! Ila hata usijali karibu home tena, kikubwa pambana na usahau yale yaliyo kutokea”
“Asante Bro! Nitafurai sana kama utakubali niendee kulala gheto maana pale tulipokua tunaishi kuna mpangaji mwiingine” alisema Owen
“Fresh! Nenda kapumzike nikija jioni tutaongea zaidi”
Chaz aliingiza mkono mfukoni akatoa funguo za gheto na kumkabidhi Owen.
Waliagana pale ndipo Owen akaenda kupumzika kwanza huku akili ikimchemka kama maji yaliyo injikwa jikoni.
Katika kitu ambacho hakua tayari kabisa kukubaliana nacho ni Anita kuolewa. Aliamini bado alikua na nafasi ya kuwa nae tena na kuishi nae kwenye mapenzi kama ambavyo walikua wakiishi zamani.
Alijikuta akiwaza sana na mwishoni aliishia na usingizi kabisa, hata Chaz aliporudi jioni hakutaka kumuasha na alimuacha apumzike mpaka siku iliyofuatia.
Palipokucha Chaz alimka wa kwanza akaanda chai na vitafunwa ndipo akamuamsha Owen.
“Oi Brooh!” Alimtikisa hadi Owen alipofungua macho
“Aaah! Nimelala sana?” Owen alinyanyuka na kukaa kitako
“Hapana! najua ulikua umechoka ndo maana nimekuacha ulale” alisema Chaz
“daaah! Usingizi wa nyumbani niwa nyumbani tu!”
“Yeah iko wazi! Sema nini Owen jana nimeongea na Big Boss amekubali kukurudisha tena gereji”
Owen aliposikia vile alifurai sana maana angalau alipata mwangaza wa kwenda kuyaanza maisha yake upya.
“Daaah! Bro asante sana yani nilikua nawaza nitaishije bila kazi!”
“Pale ni kama nyumbani ndo maana Big Boss hakua amekumaindi wala nini!” Alisema Chaz na kumfanya Owen atabasamu
“Ni kweli mwanangu”
“Acha niwai job chap we pumzika kidogo then baadae ndo uje au unaonaje??”
“Fresh haina shida”
“Chai na mazaga zaga yote yapo mezani hakikisha unashiba si unajua tena mambo ya kule??” Alisema Chaz
“ndio ndio nakumbuka”
“Ok baridi!” Chaz alivaa viatu vyake kisha huyoo akaondoka. Huku nyuma Owen hakuona umuhimu wa kuendelea kulala tena.
Aliamka akanywa chai kisha nae akatoka kuelekea saluni kwa Nadia. Kuna mambo machache alitaka kumuuliza kuhusu Anita yake na yeye pekee ndie aliekua na uwezo wa kumjibu.
Alipofika nae Nadia ndio alikua anafika ivyo wakakutana mlangoni.
“We nini kazini kwa watu asubui asubui?” Aliuliza Nadia akimkagua Owen kuanzia juu mpaka chini
“Nataka kujua kuhusu Anitaa”
“Anita wewe wa nini saa izi si mke wa mtu tayari!”
“Sijali kuhusu ilo we niambie nampataje??”
“Wanini?? Au ndo unataka kuharibu ndoa za watu?? Eeh??”
“Nadia niambie ni wapi Anita anaishi au kama vipi nipe namba zake”
“Ngoja nikuambie kitu Owen, sasa ivi Anita anaishi maisha mazuri ambayo wewe ulishindwa kumpatia! Mume wake anampa kila kitu anacho kitaka tena kwa wakati sahihi! Unaona hii saluni yangu?? Ni Martin ndie anae nilipia kodi, we unadhani nitakuruhusu uharibu furaha yetu?? Aaah subutu”
Owen alimtazama Nadia kwa hasira na kuhisi huwenda ndie sababu ya Anita kukubali kuolewa na mwanaume mwingine. Alitamani kumpiga ni vile alikua na shida na yeye, na yeye pekee angeweza kumtatulia shida iyo ivyo akatulia.
“hata namba zake tu sihitaji kingine chochote”
“Sikupi! Hapa kwangu hupati chochote kile kinacho husiana na Anita! Sawa babu???” Nadia alimkazia mno mwisho Owen akaamua kuondoka kwenda kuendelea na mambo yake.
Alipoondoka tu Owen, nae Anita akampigia simu! Nadia kwa bashasha alipokea haraka na kuipeleka sikioni
“shogile vipi honeymoon huko?”
“Hata sijaifuraia, tena nashukuru mno maana Martin amepata emergency kazini ivyo tutarudi na ndege ya usiku!” Aliongea Anita akionyesha kufurai
“Nini? Hata hamjamaliza siku tatu jamani”
“Ndo ivyo dear kazi kwanza! Hapa nimeku miss hatari kesho mchana nitakuja saluni kwako tushinde huko siku nzima”
“Hapana! Hapana! Hakuna haja, tutakutana ile sehemu yetu ya kila siku” Nadia hakutaka kabisa Anita aende saluni kwake akihofia angeweza kukutana na Owen na kuharibu kila kitu.
“Kwanini nisije huko??”
“Nime miss ice-cream bhana ndo maana nimekuambia tukutane sehemu yetu pendwa”
“Anhaa! Hakuna shida dear nikifika nitakuambia”
“Aya bye shogile”
Nadia alikata simu huku akipumua kwa spidi. Alijua kabisa ikiwa Anita na Owen watakutana basi kila kitu kitakwenda kuharibika.
Na kama kila kitu kikiaribika hata kwake itakua mbaya maana hatalipiwa kodi ya saluni tena wala kutumia vihela na Martin kama anavyo tumiwa kila wakati.
Basi kweli jioni Anita na Martin walirudi toka Zanzibar kuelekea nyumbani kwao. Wakiwa kwenye gari Martin alimtazama mkewe na kumuambia
“najua hujapenda ku cancel honeymoon yetu!”
“Ni sawa si nilishakuambia tena ivo?”
“Najua ila sio vizuri kuchanganya kazi na mambo yetu binafsi”
“Najua!” Anita hakutaka kabisa kuongeleshwa na Martin alihisi kama ana mboa vile.
“Alafu nimekumbuka kitu, Kaylah anarudi wiki ijayo! Ana hamu sana ya kukuona” alisema Martin akitabasamu
“Mimi pia” Anita aligeuza shingo yake na kuangaza macho yake nje ndipo Martin akaamua kunyamaza sababu hakutaka kuendelea kumkera zaidi mkewe.
Safari iliendelea na mwisho walifika kwenye jumba moja kubwa sana ambapo huko Anita alitakiwa kuishi na Martin.
Wafanyakazi walikuja kuwapokea na kuingiza mizigo yao ndani huku waki wapongeza mno kwa kufunga ndoa. Ajabu ni kwamba Anita hakuwajibu kabisa zaidi alipitiliza chumbani na kwenda kuoga.
Alipomaliza kuoga alipanda kitandani akalala pasipo kumsubiri mumewe. Martin alipoingia chumbani akashangaa kumuona Anita ameshapanda kitandani.
Taratibu alimsogelea karibu na kuanza kumchezea nywele zake huku akimuangalia namna gani alivyo kua mzuri.
“Niache bhana” Anita alifungua macho na kumtazama Martin kwa ukali
“Kwaiyo siwezi hata kuzichezea nywele zako japo kidogo?”
“Sio lazima, alafu sipendi mtu wa kunisumbua nikilala”
“Sijakusumbua nimekubembeleza tu Mke wangu”
“Sitaki sasa! Ama huoni ilo” Anita alikua mkali
“I am sorry Anita ila tutaishi hivi mpaka lini? Tulipokuwa wachumba hukutaka hata nikuguse na mimi nikakuelewa lakini mbona hali hii inaendelea ikiwa sasa ni mke na mume??” Martin alilalamika
“Sipo tayari na sijiskii! Siku nikiwa tayari utanigusa tu kwani naenda wapi??” Anita aligeuza shingo yake pembeni akaendelea kulala na kumuacha Martin akiwa anamtizama kwa huruma.
Je nini kitaendelea???
Nakuja…………
SEHEMU YA : 04
Basi siku iliyofuata Martin aliamka mapema akaelekea kazini bila kumuamsha Anita maana hakutaka kabisa kumsumbua.
Ilipofika saa nne asubui Anita aliamka akaelekea bafuni akaoga, akajiandaa ili kwenda kuonana na Nadia.
Kabla ya kutoka alichagua gari moja la kutoka nalo na Alitaka aendeshe mwenyewe sababu tayari alishajifunza jinsi ya kuendesha gari mwezi ulio pita.
“Boss kaniambia niwe nakupeleka sehemu utakazo” alisema Dereva na kumfanya Anita akasirike
“Kwaiyo? Unadhani najali ulicho agizwa ufanye?? Mimi ninacho kijali hapa ni wewe ufanye nitakacho mimi”
“Madam tafadhali hakuna madhara kama mimi nikikupeleka” Dereva alizidi kusisitiza
“Embu nipe funguo kabla sijakumeza mimi! Unanichelewesha kutoka ujue!”
“Sawa” Dereva alimpatia Anita funguo kisha Anita aliingia ndani ya gari, aliliwasha na kuondoka nalo.
Aliendesha gari na alipofika nusu ya safari yake gari likazimika njiani. Alikasirika sana maana kila kitu kilikuwa sawa na mafuta yalikua full tank sasa kwanini gari lizimike lenyewe??
Alichukua simu na kumpigia Martin mda ule ule akiwa bado kavimbisha uso wake.
“Gari limenizimikia njiani!” Aliongea baada ya simu kupokelewa
“Anita mke wangu hakuna hata salamu?” Martin alionekana kuto kupenda kabisa kile kitendo
“Nimesahau”
“fine! Uko wapi? Mpe simu Dereva niongee nae”
“Nipo mwenyewe sina dereva”
“Utatokaje bila dereva ikiwa hujui kuendesha gari vizuri Anita?? Mbona unataka kuniweka roho juu juu mke wangu?”
“Utanisaidia ama utaendelea kunigombeza??”
“Sorry, ngoja niongee na fundi kisha atakuja sehemu ulipo! Uko wapi kwani??”
“Hapa makutano”
“Sawa” Martin alikata simu na kuanza kutafuta namba ya fundi kwenye simu yake. Alikua anamjua Big Boss ambae ndie mhusika mkubwa wa kutengeneza magari yake na ndie aliekua akimuamini sana.
Alipozipata namba zake alizipiga na dakika zile zile simu ilipokelewa.
“Ndugu! Vipi??”
“Safi Boss! Hongera bhana kwa harusi, nisamee sana sikuweza kufika”
“Hakuna shida Big Boss! Tutaongea zaidi kuhusu hayo baadae ila now kuna emergency pale makutano, gari la wife limezima nahitaji uendee ukalicheki chap, malipo nitakutumia kwenye simu”
“nipo nina kazi kubwa sasa ivi ila usijali namtuma kijana wangu hapo dakika mbili” alisema Big Boss
“Una hakika atafanya kazi nzuri kama yako?”
“Hana shida kabisa! We niamini kwenye hili”
“Okay nakuaminia Big Boss”
“Sawa Tajiri”
Baada ya Simu kukatwa Big Boss aliwatazama vijana wake watano akiwaza ni nani kati yao amtume kwenye kazi. Wote walionekana wapo busy na kazi zao kasoro Owen ambae alikua mbali kimawazo.
Big Boss alimsogelea Owen akamtizama kwa umakini kisha akamuambia
“Dogo huna kazi? naona umepoa hapa”
“Amna Big Boss nilikua nimepumzika kidogo ata ivyo kazi yangu nimemaliza” Owen alidanganya maana mda wote alio kua amekaa pale alimuwaza Anita tu.
“Basi fresh kuna mteja amezimikiwa na gari pale makutano unaonaje ukaenda kumtengenezea chap!”
“Chaz ndo anayaweza hayo mambo”
“Dogo acha kuwa mzembe! Kati ya vijana wangu wote ni wewe mwenye ujuzi mzuri wa magari! Usikubali matatizo yaliyo kupata yabadilishe muelekeo wako wa maisha! Nyanyuka hapo uende chap” Big Boss Alimpa elfu tano ya nauli ndipo Owen akabeba vifaa na kwenda sehemu husika.
Ukweli ni kwamba hakua akitaka kabisa kwenda mahali zaidi ya kutuliza tu akili yake maana aliona ndo njia sahihi ya kujiliwaza juu ya Anita.
Basi alipofika eneo husika alikuta kweli kuna gari na ndani yake alikua mwanamke. Owen hakujali sana kuhusu yule mwanamke aliweka boksi lake la vifaa chini akisubiri maagizo.
Sio kwamba Anita hakumuona Owen alivyokuja, alimuona sana ni vile aliganda kwa dakika kadhaa machozi yakimtoka.
Hakuamini yule aliyekua kasimama mbele yake ni Owen! Mwanaume wake kipenzi anae mpenda mpaka anahisi kuchanganyikiwa.
Alishindwa kuendelea kuvumilia akaufungua mlango wa gari na kuteremka ndipo hapo Owen nae akafanikiwa kuliona Tunda lake.
Hakuna aliejali watu wangewaonaje walisogeleana na kukumbatiana kwa nguvu mno huku Anita akilia kama mtoto.
Lile kumbato lilikua lirefu kushinda miezi nane waliyokuwa wametengana. Baada ya kumbato Owen alimuachilia mwenzake na kuanza kumfuta machozi yake kupitia kiganja.
“Ulikuwa wapi Owen! Ulikuwa wapi mpaka naolewa na mwanaume mwingine” Anita alizungumza kwa uchungu huku akimpiga piga Owen kifuani.
“nisamee Anita! Please usilie” Owen akamrudisha tena Anita kifuani kwake ndipo hapo Anita akapunguza kulia.
“Nambie sasa ulikua wapi kipindi chote icho?”
“Anita tutaongea hapa barabarani?? Tutafute sehemu tuongee kwanza hapa silo eneo zuri”
Anita aliona kweli lile halikua eneo rasmi la wao kuongea, ivyo akamuacha Owen atengeneze gari haraka haraka, lilipo waka wakaondoka kwenda kwenye hoteli iliyo kuwa na utulivu ili iwe rahisi kwa wao kusikilizana vizuri.
Walikaa karibu karibu kama wapenzi vile huku Anita akimtazama Owen pasipo kuchoka.
“nambie sasa ni kipi kilicho kukuta Owen? Ulikuwa wapi kipindi chote icho na kwanini hukua ukipatikana eehe??”
Owen bila kusita alianza kumsimulia Anita kila kitu kilicho mtokea kule ujerumani kuanzia mwanzo mpaka mwisho. Alipomaliza kusimulia uso wa Anita tayari ulisha lowa kwa machozi tena.
“Sikujua kama ulikua ukipitia haya yote! Nisamee maana nilikufikiria vibaya nikadhani labda ulipata mwanamke mwingine”
“Hapana Anita! Unaikumbuka ahadi yetu? Ya mimi na wewe kuoana na kupendana?? Nisingeweza kukusaliti kwa namna moja ama nyingine bado nakupenda Anita”
“Nakupenda pia Owen! Nisamee mimi kwa kuolewa! Nisamee maana kwenye ahadi yetu mimi ndo wa kwanza kuivunja”
“usinge ivunja kama mimi nisinge sababisha! Ni makosa yangu pia Anita” Owen alimsogelea Anita na kumbusu mdomoni.
Kwa dakika za mwanzo Anita alitulia tuli akilifuraia busu la Owen ila alipokumbuka kuwa yeye ni mali ya Martin alishtuka na kurudi nyuma kidogo.
“Owen ila mimi nimeshaolewa sasa” aliongea kinyonge
“Kwaiyo kipi bora kati ya hiki? Mimi unipendaye kwa dhati? Au huyo mwanaume wako ambae upo nae kwa geresha”
“Wewe nikupendaye kwa dhati”
“Sasa kwanini unamuwaza? Na kwanini ulikubali kuolewa nae?”
“Sikua kabisa na mpango wa kumkubalia ila Nadia alinishawishi mno ndipo nikakubali! Sina hisia nae hata kidogo na ananichefua mno! Toka niwe nae hajawai kuambulia kunigusa hata tone”
Owen aliposikia vile akatabasamu na kuamini kweli Anita anampenda kwa dhati. Alimshika na kumbusu tena, mara hii Anita hakumkumbuka kabisa Martin.
Alitoa ushirikiano vilivyo na mwishoni wakachukua chumba na kwenda kumalizana huko!
Je nini kitaendelea???
Nakuja………..
SEHEMU YA : 05
Majira ya jioni Martin aliwai kurudi nyumbani akiamini mkewe alimuandalia chakula cha jioni kama wanavyo fanya wake wengine kwa waume zao.
Ajabu ni kwamba hadi mda huo Anita hakua amerejea nyumbani. Hii ilimpa mashaka Martin, alitoa simu yake na kumpigia Anita ambapo simu iliita tu bila kupokelewa.
Akiwa ana hangaika kujua mkewe yupo wapi mda huo mkewe alikua katulia kifuani kwa Owen huku akitabasamu.
“Giza limeshaingia, mumeo hatapata mashaka kweli?” Owen alimuuliza Anita
“Unadhani najali sana kuhusu yeye?”
“Hata kama ila ni bora ukawai kurudi”
“Mbona kama unanifukuza?? Mimi hata nikitaka kulala na wewe mpaka asubui nalala kwani shida nini?”
“Mimi pia nataka iwe ivo lakini kwa leo naona bora uwahi nyumbani, sitaki upate shida huko kwa mumeo! Kisha tutaandaa siku special ili tulale huko huko! Unaonaje kuhusu ilo?”
“Hakuna shida my love”
Anita alikubali ndipo wakaenda bafuni kuogeshana kisha wakavaa nguo na kutoka. Anita alimpeleka Owen hadi gheto kwa Chaz, akampa elfu 50 kisha huyoo akaelekea nyumbani.
Owen hakujali sana kuhusu hela ila alimjali mno Anita. Aliangalia gari mpaka lilipoishia mbele ya macho yake ndipo akafungua mlango akaingia ndani.
Akashtuka kumkuta Chaz kasimama mbele yake huku akimtazama kwa macho makali yaliyo jaa maswali mengi mno.
“Gari gani ulienda kutengeneza mpaka sasa ivi?” Aliuliza Chaz
“Acha tu ndugu yangu mambo ni mengi” Owen alitabasamu na kujitupa kwenye godoro
“Umerudi tu juzi ila tayari ushapata mshangazi unakushusha hadi mlangoni?? Mbona tunafichana Bro?”
“Mshangazi gani??? Ooooh unadhani ni mshangazi?? Ni Anita bhana! Kumbe ndo maana ananitazama kiukali”
“Anita?? Anita huyu mke wa mtu??”
“ukisema ivo utakua unakosea, Anita ni manzi angu. Bado yupo moyoni” alisema Owen bila uoga
“Jamaa usijisahau sana. Yule kashakua mke wa mtu! Heshimu kitu kinacho itwa mke bro?”
“Unajua Anita kaolewa na mshkaji sababu ya kushawishiwa na Nadia? Sio kama anampenda wala nini hata game hajawai kumpa”
“Kwaiyo? Hio haibadilishi ukweli kwamba ni mali ya wenyewe, tafuta wako Owen kwa yule haikua riziki”
“Katika kitu ambacho siwezi kamwe kufanya ni kumsahau kabisa Anita! Toka nakua sijamjua demu mwingine zaidi yake so tutapigana juu yake! Na nipo tayari kufanya chochote kile ili niwe karibu yake tena”
“ivi unajisikia kweli Owen”
“Bro ndo mapenzi yalivyo…. Kwanza acha maneno mengi mtonyo huu hapa” Owen alitoa elfu 30 kati ya ile elfu 50 aliyopewa akampa jamaa ake.
“Japo sipendi unacho fanya ila haimaanishi ndo sipendi hela” Chaz alizipokea huku wakicheka kwa pamoja
“Namna iyo kamanda!”
“Ila kuwa makini!”
“Baridi”
Upande wa Anita alitumia kama lisaa limoja na nusu hadi kufika nyumbani ukizingatia hakua akijua kuendesha gari vizuri.
Alipofika alikutana na Martin akiwa kavimba kwa hasira vibaya mno. Ila Hata Anita hakushtuka wala kuogopa maana anajua hawezi kumpiga wala kumfanya chochote.
“Ulikua wapi?”
“Kwa Nadia”
“Hadi sasa ivi Anita?? Kwaiyo ukiwa kwa rafiki yako hata simu zangu hupokei?”
“Mda mwingine Martin mtu asipo pokea simu mara ya kwanza na mara ya pili jua kabisa huyo mtu yupo busy! Umenipigia sana mpaka imekua kero sasa”
“Kero? Anita wewe ni mke wangu, ni haki yangu kujua ni wapi ulipo so please nipe heshima kama mume”
“Ni wapi nilipo kudharau? Kutokupokea simu yako tu ndo imekua mateso?”
“Naumia maana naona kabisa wazi unaninyanyasa na upendo wangu. Ama kisa unajua nakupenda? Ndoa haijamaliza hata wiki ila tayari umeshaanza kunipa stress Anita. Na sitaki Kaylah akija kesho kutwa aone kaka yake sina furaha na mke wangu”
“mbona furaha ipo labda wewe ndo unakuza mambo! Alafu unajua nini Martin? Nimechoka, acha nikapumzike” Anita alipiga hatua kuelekea chumbani ila kabla hajafika mbali Martin alimuita na kumuambia
“Chakula kipo mezani wife maana naona hujali kabisa kama mumeo nimekula au laah!”
“sina njaa”
“Ila nimewaambia waandae chakula kwaajili yetu sitaki chakula kikamwagwe”
“Ningekua na njaa ungeona badala ya kubishana na wewe ningekimbilia mezani kwenda kula na sio vinginevyo! Kale wewe” Anita hakutaka kumsikiliza tena bali alielekea chumbani kwake.
Maskini Martin alitia huruma mno na alishindwa kuelewa ni kipi kilimpata Anita. Alikumbuka pindi walipokuwa kwenye uchumba hakua ivo kabisa japo hakuonyesha upendo ila hata siku moja hakuwai kumjibu vibaya wala kumuonyesha ukaidi.
Ila baada ya ndoa ni kama makucha yake yalianza kujitokeza. Hakujua kabisa kama mwenzake tayari alifanikiwa kukutana na mwanaume wake wa maisha na penzi lao lilirudi kama Mwanzo.
Basi Anita alipoingia chumbani tu alikimbilia bafuni, akafungua shower kisha yeye akasimama mbali kabisa akimpigia Nadia simu.
Nadia alipokea huku akimtupia malalamiko ya kumkalisha siku nzima akimsubiri bila kutokea.
“Najua umechukia Sweetie ila sio kama nimependa ni vile kuna jambo lilitokea”
“Jambo gani ilo? Hata kama kuna jambo lilitokea ndo ushindwe kunipigia simu kunipa taarifa? Nimeaibika mimi kwa kushindwa kulipia ice-cream ya elfu 30”
“Nisamee kipenzi kesho nitakutumia hela nyingine ila kwanza ngoja nikupashe kilicho tokea! Leo nimekutana na Owen! Owen wangu karudi Nadia” Anita aliongea kwa furaha ila mwenzake hakuonyesha kama alifurai zile habari
“Kwaiyo?”
“Kwaiyo? Amenieleza kilicho mkuta ujerumani, kumbe ali…” kabla hajamaliza kumsimulia Nadia alimkatisha kwa kusema
“Najua kuwa Owen karudi, alikuja hapa kuomba namba zako za simu nikamkatalia unajua kwanini? Kwasababu wewe ni mke wa mtu! Unapaswa kuwa na mumeo hata kama humpendi, mheshimu japo kidogo kaka wa watu Anita”
“Kumbe ulikua unajua Owen alirudi na hukutaka kuniambia? Ukanyamaza kimya Nadia”
“Nikuambie ili nini? Ni kipi unacho kihitaji kutoka kwake?”
“unajua nampenda Owen kiasi gani kumshinda hata huyo Martin! Unajua ni namna gani furaha yangu toka mdogo ipo kwa Owen ila ukaamua kabisa kuni nyang’anya furaha yangu”
“Hata kama ila hii ni busara”
“Nadia tangu lini ukajua busara wewe? Umenikwaza sana” Anita kwa hasira alikata simu kisha akatafuta namba za Owen alizo zisevu kwa jina Mary na kumpigia.
Waliongea kidogo sababu Anita hakutaka Martin apate wasi wasi kwa ukaaji wake wa bafuni mda mrefu ila walikubaliana watoke out kesho kutwa ambayo ndio siku Kaylah alikua akirejea.
Je nini kitaendelea?
Nakuja………..
SOMA MAELEKEZO
Bonyeza hi "Soma Kitabu" kisha itakupeleka kwenye fomu yaku login, hakikisha ume login na namba uliyojiunga nayo ndipo utaendelea sasa kusoma kitabu chote