KINGANGA PRO MAX

book cover og

Utangulizi

Sisi ving’ang’a bhana, tuna pepo yetu ya nguvu, tunang’ang’ania mpaka jasho la meno, na hatuchoki hata kidogo! Muulizeni Kevin awaambie moto wangu! Mwanzo alinikataa na kunipiga vita! Ila kwa uki-ng’ang’a wangu na mambo yangu ya ajabu, akajikuta ananipenda kuliko alivyo tarajia!

Mnataka kujua ilikuaje???
Embu twende pamoja………

SEHEMU YA : 1

Unajua mimi si mtu wa kujisifia bwana, ila kuna vitu nikikaa navyo kimya nahisi kama vinanikaba kooni. Ngoja kwanza nianze kuwapa habari kubusu habibi wangu Kevin.

Kwake Nilikua nimepiga bingo la maisha! Maana kijana ni Tajiri yule, sura safi, ka harufu kazuriii kanafukuzana na baridi, na pesa je?? Weh! Ni kama kisima cha maji. Ana pesa mpaka ana changanyikiwa. Alipokuja kuni kwaza ni pale aliposema eti hanitaki tena??? Shishi mimi?? Wallah kuachika ilikua ngumu kama alivyo tarajia.

Sasa sikia, nilipokutana na Kevin sio kama nilikua nimetoka saluni au kudai rejesho? hapana! Ilikua ni ile siku tulitoka na shoga zangu baada ya mimi kupokea hela yangu ya upatu.

Weh nilipanga nijispendi ile siku, acheni tu! Nikavaa kile kigauni chembamba cha mshono wa kufungia mgongoni, na heels zangu za kubana miguu hadi niwe mrefu kama dirisha la mlango.

Tulienda zetu pale Highness Lounge, ile ya Mikocheni sehemu yenye matawi ya pesa. Kuingia tu, nikajua kabisa leo nitajibebea mubaba wangu! Kule kuna harufu ya wenye pesa waliobarikiwa kuumbwa na Mungu siku ya weekend akiwa katulia👌.

Sasa nikiwa nacheza nikitikisa vinyama nyama vyangu nilivyo barikiwa na Mungu ndo nikashtukia kumuona Kevin kakaa meza ya VIP, amevalia suti nyeusi na shati jeupe la kushonwa wazungu wanaita Italian cut!

Alikua ananiangalia vibaya mno na mimi nikazidisha kutikisa vinyama vyangu makusudi. Yani mi mwenyewe nilijua lazima kuna kitu baina yetu maana sio kwa yale macho.

Ila sasa kijana hakuchukua hatua ya kunifata. Nikaamua kujiongeza lasivyo ninge mkosa mchumba. Si nikajidai kwenda ka-counter, nikajifanya kuchukua kinywaji kingine wakati tayari nina konyagi yangu nimeibania kwapani🤣🤣.

Na yeye akajongea taratibu tukaangaliana, tukapiga vistori viwili vitatu kisha tukachukuana na kwenda kumalizana nyumbani kwake. Toka siku ile nikawa nakwenda kwake kila wakati maana tayari tulishakua penzini😋.

Na nisiwafiche, mapenzi ya Kevin yalikuwa ya kificho! Si unajua matajiri wa Dar, ukianza kuwaibia moyo wanakuweka nyuma ya pazia. Ila mimi sikujali, mradi nikifika kwake akinikumbatia na busu juu basiii najihisi kabisa kama niko peponi kabla ya kufa.

Lakini sasa wapenzi mnajua tatizo lilikua wapi? Kevin hakua na moyo. Yule kijana hakua na roho ya mwanaume wa kusimamisha familia. Alikua anataka anipitie tu kama upepo wa Bahari. Sasa mi si upepo, mi ni Kimbunga cha Daraja la Tano! Ukinitupa, nakurudia kwa kasi ya 7G👌.

Nilimwambia mapema, “mimi siyo wa kuchezewa bwana, mimi shishi sio dada wa kuachika! Nikipenda nimependa kweli na kuachika kwangu ni kimbembe labda jeshi liingilie kati”

Mnadhani alinijibuje? Weh! Hata msijali wapendwa nitawaeleza yote hadi ile siku niliyopiga goti, nikamvisha pete kabla hajamaliza kuoga siku ya birthday yake na akaniambia sihitajiki tena 😭

Lakini sasa jamani, siwezi kuachika. Mimi Shishi, mtoto wa Mama Zena, King’ang’a Pro Max. Hadi Kevin aniache, lazima aingie ICU ya mahaba. Niliishikilia roho yake kama file la siri za serikali.

Na bado!

Je nini kitaendelea??
Nakuja………….

SEHEMU YA : 2

Sasa wapendwa tuachane na stori za nilivyo kutana na Kevin tuanze stori yetu rasmi sasa. Kevin alikuwa kama chocolate iliyotoka kwenye fridge, anang’aa hadi macho yanahema yenyewe.

Na mimi napenda sana kujitoa kwa vi suprise vya hapa na pale ili kunogesha penzi langu na Kijana. Na mtaa mzima walijua nina mwanaume tajiri maana ilikua ngumu sana kulifunga bakuli langu. Sasa nyie watu mlitaka nikae kimya? Nimebeba bonge la mwanaume, nisiseme? Aah, mtaelewa tu baadaye.

Basi Mambo yalikuwa hivi, kesho yake ilikuwa ni birthday ya Kevin. Nikiwa kama mpenzi wake wa kichini chini, nikaona kabisa hawezi kusheherekea kitu kwa sababu alikuwa bize kama vile yeye ndo rais wa nchi😂.

Mimi nikasema: “Shishi, huu ndo wakati wa kujituma. Mpenzi wa kweli haombi nafasi, anatengeneza nafasi!”

Nikaamka saa kumi alfajiri kabla hata jogoo hajawika. Nikavaa kanga mbili, nikafunga kile kitambaa changu cha vitenge nilichonunua Kariakoo, alafu nikajipulizia karafuu na ka pafyumu changu cha promo.

Nikakodi bolt ya tax tena ya bei ya kawaida maana bajaji au boda zisingeingia ule mtaa wa Kevin. Unaingia pale mpaka mlinzi anakutolea macho kama vile unaiba hewa😂😂.

Nilipofika getini, sikukuta hata mtu. Sikuendelea kubaki pale nje, Si nilishajua njia bhana kwaiyo huyo nikazama ndani moja kwa moja mpaka jikoni.

Nikaanza kazi sababu binti nilikua kwenye harakati za kupalilia penzi. Nilimpikia Kevin breakfast ya kiswahili maana kulikua na mihogo ya kukaanga, chai ya tangawizi, na vitumbua vya mama Sona nilivinunua kwa 500! Hata Mama Zena hakua akimuandalia baba chai ya namna iyo pindi tukiwa wadogo😅.

Nilipomaliza nilikaa na kumsubiri Kevin aamke sababu nilipofika alikua bado kalala. Nikaweka tray vizuri mezani, nikapulizia ile karafuu nyingine maana lazima apate harufu ya wifey material kabla hajaona sura.

Kama dakika 20 zilipita ivii ndipo Kevin alitoka chumbani akiwa kapiga boxer na singlet. Meno hajapiga mswaki, macho yanavuta usingizi. Alipoona meza imepambwa, nyumba inamvuto, na harufu ya mihogo inapiga kelele kwenye pua zake, alishangaa😳.

“Wewe, unafanya nini hapa?” akaniuliza kwa sauti ya ukali ni wazi hakupenda ujio wangu

Nikacheka kwanza kwa pozi la kike, nikajiweka vizuri na kusema

“Suprise baby! Leo ni birthday yako, na sikua tayari kuruhusu uamke bila harufu ya mapenzi!” Nikaendelea kucheka huku nikimpa busu lile ambalo wazungu wanaliita flying kiss.

Kevin hakujibu akabaki anashangaa. Nikaona nimpe suprise nyingine nzuri niliyokua nimemuandalia kwa kipindi kirefu mno.

Nilitoa pete ya mtumba niliyonunua kwa mama mmoja pale Tandale ya silver lakini inang’aa kama macho yangu yalivyo kua yana ng’aa pindi ninapo ionaa sura yake😂.

Nikapiga GOTI CHINI! Watu wanasema wanaume ndio hupiga goti, lakini mimi ni SHISHI wa Kinondoni! Mimi ninapo penda nafanya mambo ambayo hudhani kama nitafanya ata ukiniambia nisile wiki nzima sitakula😂.

“Baby Kevin utaniowa?” nikasema huku nikiwa nimekunja uso kama vile nalia, lakini macho yangu yakiangalia mshtuko wake.

Weh! Kevin hakukaa kimya. Alichukua mda kidogo kujibu huku akinishangaa kama vile ameniona mara ya kwanza. Kisha akatoa sauti ya upole lakini iliyochoma kama sindano ya ARVs.

“Shishi, hivi wewe unaelewa kweli tulichokuwa nacho ni nini? That was just a thing ya muda. Mi sikuwa serious na wewe. Na sasa hivi naona ni bora kila mtu aendelee na maisha yake. Please usirudi tena hapa”

BOOM! Nikawa kama nimepigwa na bomu la nyuklia!
Niliishiwa pumzi kama mtu aliyepigwa na fimbo ya manati.

Nikabaki nimepiga magoti, pete mkononi, uso wangu ukitafuta mahali pa kujifichia. Hapo hata ile mihogo iliyokua kwenye tray ilionekana kama yale mawe ya Ziwa Victoria. Hata chai ya tangawizi ilinikata koo.

“Kevin, unamaanisha nini? Mimi nimetoka nyumbani asubui asubui kama mchawi nikaja huku kukufanyia suprise, na wewe unaniambia nisiendelee kuwa sehemu ya maisha yako? Acha utani bhana” sikutaka kuamini

“Unaona nakutania?”

“Ndio huu ni utani ambao sio mzuri! Kama unahitaji mda kufikiria kuhusu ombi langu la kuniowa sawa tu ila usinambie kuhusu kuachana”

“Ilo ndo tatizo lako! Hutaki kuambiwa ukweli!”

“Ukweli gani?? Kwamba hunitaki?? Na uzuri wote huu???”

“Fine wewe ni mzuri, kwaiyo??? Mimi nilikua napita kwako sio zaidi ya hapo! Hukuona hata sikukutambulisha kwa rafiki zangu! Come on Shishi mimi na wewe ni watu wawili tofauti”

“Au shida ni uswahili wangu?? Kevin mimi nipo tayari kubadilika wallah vile!” Machozi yalikua yakinilenga lenga machoni 🥺

“Bado hujakidhi vigezo vya kuwa na mimi! And please sitaki kukuona tena nyumbani kwangu! Sikuhitaji Shishi”

“Kevin jamani….! Nitabadilika jamani” niliomba Lakini Kevin alikua tayari kashaingia chumbani. Na mlango akaubamiza kwa nguvu.

Yani nikawa nimepigwa tukio zito Kama sinema ya Nigeria. Nikabaki sebuleni na mihogo yangu, na vitumbua vyangu vya 500.

Nilifikiria kwa dakika kadhaa kisha nikatabasamu badala ya kulia. Nahisi Kevin Bado hakua kamjua Shishi vizuri kama alidhani tungeishia pale alikua akijidanganya. Moyo wangu ni kama chuma cha reli, ni mgumu kuelewa.

Je nini kitaendelea?
Nakuja……..


SEHEMU YA : 3

Siku hiyo nilitoka kwa Kevin kama mtu aliyefukuzwa kwa uchawi. Nilijisikia mwepesi kama nimerukwa na roho. Pete ya Tandale ilikuwa bado mfukoni, chai haikunyweka, mihogo haikulika ni bora hata ningempa mbwa wake😏.

Nilipofika home, shoga zangu walikuwa tayari kibarazani. Macho yao yakinichunguza kama vile walijua kuna jambo limefeli.

Maimuna aliniangalia kwa jicho la dharau, akavuta sigara yake na kutoa moshi puani kiasha akauliza

“Shishi kwani umelia? Au umemkuta na mwanamke mwingine?”

“We acha zako, baby wangu yule kanishtua tu. Hakuwa ameamka vizuri. Mimi naona ni stress tu za kazi. Huyo mwanaume ananipenda mbaya mno”
Nililazimisha tabasamu. Lakini ndani ya moyo, nilikuwa kama mtu aliyezama mtoni na maji yamekata pumzi.

Siku hiyo usiku nilipost picha ya Kevin kwenye status yangu ya WhatsApp. Caption ikawa

“Mwanaume wangu! Tamu yangu mwenyewe😍❤️ Walionacho hawapigi kelele.”

Watu waliitazama, waka like na kunitumia meseji maana Kevin ni handsome alafu pia ndo ilikua mara yangu ya kwanza kumpost na watu kumuona.

Wengi walinipongeza ila kuna huyu shoga yangu Suzy alinitumia voice note akisema

“Shishi, achana na ndoto za mchana. Kama anakupenda kweli, angekuwa na wewe hadharani. Si mnakutana kichinichini na ana kuficha kama sehemu za siri”

Alinikera kweli ivyo nikamlamba block kila mahali maana nilishawai kumuambiaga mambo machache kuhusu mimi na Kevin sasa akajiona kama mjuaji sana wa maisha yangu😏.

Siku ya pili nilivaa sura ya kazi. Si kazi ya kawaida bali ni kazi ya kumrudisha Kevin!

Nilipiga nguo kali, ile tight ya pink na crop top niliyonunua kwa mtumba wa Bei Ya Mwisho. Nikajipulizia perfume ya mafuta ya mchina ile ya kuua harufu ya choo cha stendi🤣🤣.

Chini nikapigilia ndala zangu za kiswahili, nikapanda bajaji mpaka kwenye ofisi ya Kevin pale Mikocheni.

Nilipofika Mlinzi wa getini alinikazia macho. Aliniona kama kituko na jinsi nilivyokua nimevaa sikuendana kabisa na dressing code ya ile ofisi.

“We una appointment?” Aliuliza akizidi kunishangaa

Kabla sijamjibu nikacheka kwanza kwa dharau! Nikamsunya kidogo

“Kwani hujui? Mimi ni mke wa boss wenu. Leo kuna suprise yake nime mletea ofisini, usinitibue akili”

“Mke wa Boss?” Macho yakamtoka

“Kwani umesikia nimesemaje??”🤨

“mmmh! Lakini hauruhusiwi kuingia huku ndani ukiwa umevaa ivo!”

“Embu nipishe mimi, kwani nipo uchi” nilimsukuma nikaingia ndani nikitembea kama miss vile, yule mlinzi Akanisindikiza kwa mashaka huku akitikisa kichwa chake.

Nilifika mapokezi, yule dada mrembo wa mapokezi akanizuia na yeye,aliniambia,

“Samahani, Kevin hawezi kuonana na mtu yeyote bila booking ya awali.”

“Mrembo, nimesema ni mke wake. Mwambie Shishi yuko hapa, atajua” Nika tabasamu taratibu

“Mkewe?” Na yeye pia akanishangaa kama ilivyokuwa kwa yule mlinzi getini

“Ndio! Mkewe”

“Basi subiri kidogo” Dada wa mapokezi akapiga simu. Hatimaye Kevin akatoka mwenyewe. Uso wake haukuwa na furaha hata tone. Alinikazia macho kana kwamba mimi ni deni la bodi ya mikopo😂😂.

Alipofika akanikamata mkono na kunivuta kunitoa nje. Hakutaka kabisa wafanyakazi wake na watu waliokua pale wajue ni kipi tulichokua tunakizungumza.

“Shishi una matatizo gani? Mbona hunielewi? Nimekwambia hatuwezi kuwa pamoja. Hatuendani. Usinifatilie kazini tafadhali!”

Maneno yake yaliuchoma moyo ila bado sikutaka kukubali. Nikamsogelea karibu, nikamshika mkono na kumtazama machoni

“Kev usifanye hivi. Nilikupenda kwa roho yangu yote. Hata mama yangu sijamwambia kuhusu sisi ili nikulinde. Mi ni wako baby, na sitaki kuachika. Huwezi kuniweka kando kwa sababu tu sina degree wala sivai suti”

Kevin akanikwepa. “Please ondoka kabla sijaita ulinzi.”

“Kwaiyo unanifukuza?? Kabisa Kabisa Kevin??”

“Ndio! Ondoka! Sitaki unifuatilie! Narudia tena kwa mara ya mwisho Shishi, sikutaki na sikuhitaji, mimi na wewe tulikua tukijiburudisha tu sikua kabisa na mpango na wewe”

“Sawa Kevin lakini sikufuatilii kwa hasira, bali kwa upendo! Nitatoka, lakini mapenzi yangu hayatoki! Unaonaje nikija kwako usiku nikakupikia ukala kisha tukaongea?”

“Ivi hujasikia nilichokuambia lakini?”

“Mimi huwaga sikisikiagi! Ndo kwanza unazidi kunipa amsha amsha”😂

“Shishi, kaa mbali na mimi! Next time nikikuona nyumbani kwangu au ofisini kwangu tena basi nakuitia polisi and nipo serious” aligeuka na kuingia ofisini kwake akaniacha nikimsindikiza kwa macho yaliyojaa huruma na mahaba ya hali ya juu.

Basi Usiku huo usingizi haukuja kabisa, yani kitanda kilikua kama kina mi

“Kev, kama kweli unataka kuachana na mimi, basi jua sio rahisi. Mimi siwezi kuachika kienyeji. Kumbuka nilikupikia chai. Nilikusafishia nyumba. Nikakupa mpaka tamu yangu. Mapenzi haya si ya kulipua baby. Mimi ni wa kuolewa si wa kuachwa”

Sijui kama aliisoma ile meseji ila hakuijibu kabisa, nikajikuta nasubiri ijibiwe na kuishia usingizi.

Siku iliyofuata drama ikaanza rasmi. Nilijua Kevin anakutana na dada mmoja wa mrembo aitwaye Angela.

Inasemekana wako kwenye bodi moja ya kampuni. Eti walikua wakienda mpaka lunch pamoja. Kevin hakua akimficha Angela kama jinsi alivyokua akinificha mimi. Ni wazi kulikua kuna kitu baina yao na mimi sikutaka kukubali kirahisi.

Nilichokifanya ni kuandaa kadi feki za harusi nikazipeleka ofisini kwa Kevin. Ilikuwa ni kadi flanii nzuri zenye jina la “Kevin & Shishi – Harusi ya Karne.”

Mbaya zaidi pale juu ya kadi nikaweka picha ya Kevin ile niliyo mpiga akiwa kalala juu ya kifua changu kama mtoto. Hakuwai kujua kama niliwai kumpiga picha kama ile.

Basi nikasambaza zile kadi ofisi nzima kisha huyoo nikaondoka zangu. Aisee ile ofisi ilichangamka vibaya mno, wafanyakazi wakaacha kufanya kazi na kuanza kumjadili Boss wao.

Sasa Kevin na Angela walipokua wanarudi baada ya kutoka lunch ndipo wakakutana na zile habari. Wee Kevin alichukia sana kiasi kwamba alitamani ardhi ipasuke aingie ndani.

Kadi zote kule ofisini zikakusanywa kwa amri yake na kwenda kuchomwa zote. Kisha akawaambia wafanyakazi wake iwapo atasikia chochote kuhusu lile tukio basi watapoteza kazi.

“Kwani huyu dada ni nani??” Aliuliza Angela

“Ni binti flanii wa kiswahili nilikua nina one night stand nae hakuna zaidi ya hapo. Ila ni kama alihisi tuna mahusiano coz haachi kuniganda”

“Unajua alicho kifanya leo ni aibu, ungekua na mgeni mkubwa hapa ofisini ingekuaje”

“Yeah! Sitaki hata kufikiria hichi kitu”

“Kwaiyo utachukua hatua gani?? Mpigie mwambie humtaki”

“You know what Angela?? Nikimpigia nitazidi kumpa kichwa, nataka nimuonyeshe kwamba chochote atakacho fanya hawezi kupata attention yangu”

Kweli Kevin hata hakunipigia simu. Nilidhani angenipigia simu anifokee au anitukane kwa nilicho kifanya ili angalau nisikie sauti yake ile haikua ivyo.

Ina maana huyu kaka hajui kama moyo wangu ni kama gundi ya kiwandani haikauki kirahisi??? Ngoja auone moto🔥

Je nini kitaendelea???
Nakuja……….

Sehemu ya : 4

Siku mbili baada ya kunyamaziwa na Kevin kama hana salio, nilikuwa nimekaa kitandani kwangu, nimevaa kijora cha pink chenye michoro ya maua,
Nikinywa maji ya baridi kwenye mfuko wa plastiki nikiyatupa macho kwenye simu kila dakika.

Hakukua na SMS wala Hakukua na call. Hakuna hata emoji ya blue heart. Kevin alikuwa amenikata kama majani ya mihogo msimu wa kiangazi.

Lakini moyo wangu ulikuwa bado uko kwake. Kwa sababu moyo wangu mimi, Shishi binti wa Mama Mapenzi, si wa kawaida. Ni moyo uliotengenezwa Kariakoo, sehemu ya spare parts za kupenda bila breki.

“Nitamfuata mpaka kwao, Hii inchi bila kujitoa akili japo kidogo huolewi wallah. Kama mama mtu mzima anaweza kupewa mimba akiwa na miaka 50, basi mimi Shishi nitakuwa mkwe wa familia ya matajiri!” Nilijisemea kwa sauti ya chini huku nikikumbuka kitu.

Kuna siku Mama Kevin alikua ana kahoma ivyo Kevin akampelekea dawa ila hakutaka niongozane nae ndani ivyo nikabaki kwenye gari.

Sasa kama nyumbani kwa mama yake nilikua napajua sasa kwanini nisiende jamani?? Nikajitambulishe mapemaa kabla mambo hayajawa mabaya zaidi.

Basi Sikutaka kuonekana kama mcharuko wa uswahilini. Nilienda saluni kwa dada Lusekelo, yule wa kupaka rangi za kucha hadi kwenye vidole vya mguu.

Nikajiremba kama bibi harusi wa bure, nikavaa nguo niliyonunua pale Msimbazi Center, lile gauni jeupe lililoshika miguuni na kuruka juu kama hizi nguo za wana mitindo. Nikavaa heels feki, nikavuta perfume ya Karafuu iliyochanganywa na mchaichai.
Kisha nikapanda bajaji hadi Sinza, nilikojua mama Kevin anaishi.

Nilipofika, niliwakuta wapishi wakipika kwenye baraza ya nyumba. Harufu ya pilau ilipiga puani kama kiwembe cha bangi. Nikajua mama mtu mzima atakua ana wageni.

Nikagonga mlango kwa confidence ya mwanamke anayejua anakwenda kutambulishwa rasmi. Mlango ukafunguliwa na mama mwenyewe.

Alikuwa mwanamke mrefu, amevaa kitenge cha harusi, nywele zake zimepigwa flat twist. Macho yake makali kama CCTV za bank😂🤣.

“Habari mama, samahani nimekuja na barua ya moyo. Jina langu ni Shishi. Mimi ni mchumba wa Kevin. Nimekuja kuomba baraka zako kama mama mkwe mtarajiwa”😂🤣

Mama Kevin alinitazama juu chini. Akaangalia gauni langu, makeup yangu, alama ya tattoo ya nyota kwenye kifua changu.

Akaning’ong’a bila huruma, “Mchumba? Wewe? Kevin wangu? Acha masihara binti. Kevin hawezi kutoka na wasichana wa tabia zako. Hii si nyumba ya michezo. Hatuoi binti wa kuokota baa”

Nilimeza mate kwa hasira na uchungu! Na uzuri wote huu ananiita mwanamke wa baa?? Nilimvumilia ile dharau maana sikutaka kugombana na mama mkwe ikiwa ndo kwanza tumekutana.

“Mama, mapenzi hayajui kipato. Na mtoto wako ameniona mimi ndio faraja ya maisha yake. Tulikuwa wote hata siku ya birthday yake. Nilimpikia chai, nilimvalisha suti aliyoenda nayo kazini! Huwezi kunikataa hivi hivi tu.”

Mama Kevin akasimama mlangoni, mikono kiunoni, akazungusha kichwa kama anakagua uwanja wa mpira😂🤣.

“Sitaki usumbufu. Kevin ana mchumba wake anayeitwa Angela. Msomi, mwenye kampuni, anatoka familia ya heshima. Wewe ni nani? Umekuja hapa kwa fujo na mavazi kama mcheza video vixen. Ondoka kabla sijakuita mlinzi!”

Nikabaki nimesimama kama sanamu la Makumbusho. Aibu ilinichoma lakini roho haikuniponya. Mapenzi yalinifunga miguu hata kugeuka nyuma nikashindwa.

Eti yule Angela ndio mchumba wa Kevin! Yani kumbe lunch zao zimezaa matunda na wao kuwa wapenzi! Binti wa watu nikageuka nyuma taratibu nikaondoka huku uso ukiwa chini.

Nilipokaribia kufika nyumbani Nilienda kusimama pale kwenye kivuli cha duka lililokuwa limefungwa, mvua ikaanza kunyesha taratibu. Nikakumbuka nilivyomwambia Kevin, “Mimi siwezi kuachika.”

Niliandika tena ujumbe, na ujumbe huu ulikuwa wa voice note kwa Kevin

“Kev, mama yako amenifukuza kama mimi ni jini mahaba. Lakini moyo wangu bado upo kwako. Nimejikaza, nimevumilia, nimepika, nimeomba baraka, bado nakupenda na wewe upo moyoni mwangu. Tafadhali usininyime nafasi. Siwezi kuachika kimyakimya, itabidi unifunge gerezani au unioe kabisa”

Ujumbe ulifika, ulisikilizwa na Haukujibiwa. Kuona vile nikaona ni bora nije na mpango mpya kichwani lasivyo penzi nitalikosa😅.

Nilirudi uswahilini, nikakutana na shoga zangu. Wote walikuwa kwenye kikao cha upatu. Ni mimi pekee sikua nime udhuria sababu ya kuwa bize na Kevin

“Hee Shishi, umepotea! Ulikuwa wapi bby?” Maimuna akauliza.

“Nimeenda kwa mama mkwe, akanifukuza! But mimi si mtu wa kuachika kirahisi. Nataka sasa niendelee na mission ya kumdhibiti Kevin bila kutumia upendo, nataka kutumia akili”

Wote wakapigwa butwaa. Suzy akauliza,

“Wewe sasa una plan gani?”

Nikacheka taratibu, nikafungua mfuko wangu mdogo nikatoa USB flash.

“Ninaa picha zetu pamoja na video zake akinambia jinsi anavyo nipenda siku ile ya kwanza tuliyokutana! Japo alikua kalewa ila zitafaa! Sasa ni wakati wa kulitangaza penzi letu kwenye mitandao ya kijamii. Kama Kevin hataki kunikubali kimoyo, basi atanitambua kwa nguvu za content”

“Unajua wewe Shishi huna akili vizuri, mbona ni wazi kuwa hutakiwi?? Kama mama yake ameshakukataa ya nini kufosi” alisema Suzy ambae nilimtazama kwa macho ya hasira

“Ndo maana niliku block sababu ya kamdomo kako! Binti hujui nini ya mapenzi!” Nilimjibu nikiwa nimekunja sura

“Unadhani najali kuhusu kublokiwa?? Lakini nataka ujue huo ndo ukweli! Muache kaka wa watu! Hakupendi ni hakupendi”

“Hahhahahahahahhh! Weee, mimi nampenda na kama hanipendi atajua mwenyewe, nikimpenda mimi inatosha”

“Shishi! We shishi weee” Suzy aliniangalia kwa huruma alihisi labda nimedata.

“Eeeeh na wewe! Acha kuingilia mambo ya watu! Mwaya Shishi, kama unataka kuposti huko mitandaoni ni sawa tu! Mimi nakusapoti” alisema Maimuna baada ya kuona kama Suzy analeta pingamizi

“Ayo ndo mambo nayotaka kusikia” nilitabasamu huku nikiwa nimepania kabisa kufanya jambo langu.

Je nini kitaendelea?
Nakuja………..


Sehemu ya : 5

Wapenzi, Kama hujawahi kumpenda mtu mpaka ukajiona kichaa kwa akili zako mwenyewe, basi hujamjua Shishi.

Mimi ndiye mwanamke pekee Kinondoni mwenye roho ngumu kama chupa ya gongo. Na kama kuna mwanaume mmoja aliyefanya moyo wangu utembee kama kiatu cha spika ni Kevin. Tajiri mwenye sura ya kuumiza, pesa za kuingiza pressure, na tabia ya kukuacha bila huruma.

Lakini sasa nilikuwa nimechoka kuwa mpenzi wa siri na kuachika. Nilichoka kuwa yule binti wa kutumika na kuachika. Sasa ilikuwa ni zamu yangu ya kuweka mambo hadharani.

Niliingia ndani haraka na kuanza kuzikagua zile video zilizo kuwa kwenye flash. Niliporidhika nazo nikazihamishia kwenye simu.

“Leo na-trend, lazima watu wajue jinsi gani ninavyo mpenda huyu kijana!” nilisema kwa mbwembwe, nikishika simu yangu vizuri na kuingia TikTok.

Nikaiposti ile video, tena nakumbuka hii video nili mrekodi akiwa kalalia paja langu kama jinsi mtu anavyo kumbatia mto. Nilimrekodi akisema maneno ya mahaba maana alikua kalewa

“Baby, usiwahi kuniacha. Wewe ni kama oxygen yangu” 😂😂

Tena hiyo sehemu niliikata vizuri na kuiwekea nyimbo nzuri za mapenzi za TikTok.

Na kuhusu Caption je?? Hata sikuteseka kuandika maneno matamu. Hapa nilijimaliza kabisa

“Mwanaume wangu akiwa kwangu 🥰🫣 Mapenzi yana nguvu jamani! Jamaa haelewi kabisa kuhusu uswahilini yeye kachanganyikiwa na mahaba! Nakupenda pia Kevin 🫶 #Taken #WifeMaterial #Kevin❤️”

Kabla hata dakika 20 kupita, views zilianza kupanda kama bei ya mafuta.

10K
23K
50K…

Video ikasambaa na watu wangu wa karibu wakaanza kunitumia meseji nyingi kwenye whatsapp, yani mseji zilikua nyingi kama nyumba ya nyuki.

“Ina maana ni kweli?” Meseji moja ilisomeka ivyo

“Hivi Kevin sio yule mwenye kampuni ya vifaa vya ujenzi?” Akauliza mwingine na hata sikuhangaika kumjibu.

Nawaambia Mitaa ikachafuka. Vijana wa bodaboda walikuwa wananitambua barabarani maana nilipo pita kesho yake shangwe zikawa kwangu! Wasichana wa mtaa walinitazama kama vile nilikuwa First Lady wa Bongo. Chezea Shishi nini🔥

Basi Ofisini kwa Kevin, mambo yalienda mrama.
Bodi nzima ya kampuni yake iliitisha kikao cha dharura.

“Wewe ni public figure (kioo cha jamii) na sasa kila blog imeandika ‘Kevin Billionaire Alazwa Kifuani na pajani kwa Demu wa Uswahilini’ what is this nonsense? (Huu ni upuuzi gani”

Icho ndo kilicho sikika kwenye kikao cha Bodi. Kevin roho ilikua mkononi. Alitumia akili na maneno yake matamu kuishawishi bodi yake ya kampuni mpaka wakamuelewa na kutuliza hasira.

Baada ya kikao kuisha Kevin alirudi ofisini kwake akachukua simu na kuanza kuitazama ile video kwa mara nyingine, na mara hii alikua kama mbogo. Angela alipoingia ofisini kwake, alikuta Kevin akiwa ameshikilia simu na kutetemeka kama aliyetema betri.

“Kevin! Hii video ni ya kweli?! Ulienda uswahilini kulala kwa yule dada anayevaa miniskirt ya neti? Yule anayeishi na paka wawili na meza ya plastiki?”

Kevin alinyamaza kimya. Alijua kosa lake halikuwa kulala na mimi bali Kosa lake lilikuwa kunichezea, halafu kunisahau.

“Mbona hujibu? Ulisema ilikua ni one night stand (usiku mmoja) pekee?”

“Ndio pia tulikua tukionana kwa siri sana! Tulikua tuna mahusiano” alisema Kevin

“Kwaiyo unajihisi nini juu yake?”

“Angela, ningekua nampenda yule binti ningemuweka hadharani watu wamjue hata mama amjue! Lakini sikua na mpango nae”

“Sasa unaona anavyo enda mitandaoni kudai anakupenda? We unadhani ilikua ni utani ila mwenzako ameshika hisia kweli, na mimi sitaki shida kwenye penzi letu! Na ndo kwanza limeanza. Na unajua jinsi gani naona wivu, hujawai kunilalia kwenye paja na kuniambia unanipenda kama ulivyo fanya kwake”

“Nilikua nimelewa siku hiyo! Please elewa Angela”

“Naelewa ila ni mda sasa wa kusahihisha makosa! Sihitaji hili lijirudie” Angela alimsogelea Kevin na kumkumbatia.

Tukirudi upande wangu mda huo Nilikua nimekaa saluni ya Dada Lusekela, nikisuka nywele za crochet, mara simu yangu ililia. Ilikuwa Kevin. Mwanaume wa ndoto zangu na sasa ndoto yake ilikua ni mbaya😂.

“Shishi! Umerogwa?” Kevin aliropoka nilipo pokea simu na sauti yake ikiwa imechanganyikana na hasira na hofu. Alivuta pumzi ndefu kisha akaendelea kuongea

“Wewe una matatizo gani kichwani? Kwanini unaposti video yangu? Umekuja kuharibu maisha yangu?”

“Babe, si uliwahi kuniambia eti mimi ni oxygen yako?” 😂🤣 Nikacheka kimya kimya

“Usinifanye nicheke, Shishi! Wewe ni nani kwangu?! Hiyo ilikuwa siku moja, just one night! Na baadhi ya siku tulizo kutana kukata hamu! Haimaanishi ndo nakupenda! Halafu ukaanza kujipa cheo cha mke wa mtu. Acha hizo!” Kevin alipumua kwa nguvu

Nilikaza roho na kumuambia

“Wewe ulinikula kama ugali wa jana, ukalala kwangu siku tatu, ukanywa chai yangu ya limao, nikakusugua miguu kwa scrub ya ndimu alafu leo unasema nilikuwa one night?”

Kevin Akatulia kwanza Kisha akasema kwa sauti ya chini sana

“Nipe location yako sasa hivi. Tunahitaji kuzungumza”

Kusikia vile nikafurai mno, nikamuambia sehemu nilipo akasema hawezi kuja uswahilini ivyo tukutane hotelini. Wee! Nikazidi kufurai, nikamalizia kusuka chap, nikaenda kujiandaa na kwenda kukutana na Kevin wangu.

Tulikutana kwenye hoteli ya kifahari, Seacliff, maeneo ya Masaki. Nilivaa gauni refu jeupe, nikapaka red lipstick kali, na heels zangu zilizokuwa zikipiga sakafu kama polisi wa FFU😂🤣.

Kevin aliponiona, uso wake ulikuwa mweusi kuliko samaki wa kukaanga.

“Unajua nini unafanya?” akauliza kabla hata sijavuta kiti kukaa pembeni yake

“Najua, nafanya kama mke wa mtu anayetaka heshima” Nikamsogelea karibu huku nikizidi kumwambia

“Kevin, siwezi kuachika! Hata ukifunga ndoa na Angela, nitakufuata mpaka nyumbani. Nitakuwa mgeni wa kila chakula chako cha jioni. Nitakuwa kivuli chako. Na mimi ndo nitalea watoto wako!”

“Shishi, unahitaji msaada wa kisaikolojia” Kevin alishtuka😳

“Sitaki mtaalamu, nataka ndoa” nikacheka

“Nimekuita hapa tuongee kibinadamu, unataka kiasi gani ili uache kunifuatilia fuatilia?”

“Mimi nataka penzi lako, nakutaka wewe na sio hela”

Kevin alizidi kupagawa nahisi ilikua ni mara yake ya kwanza kukutana na King’ang’a Pro Max kama mimi.

“Kama hautaki hela basi acha nikupe onyo! This time Shishi sicheki na wewe! Kaa mbali na mimi, acha kuniposti mitandaoni ukidai mimi ni mpenzi wako! Ninae mpenzi sasa ivi! Kaa mbali na mimi” Kevin aliongea kwa kumaanisha maana alikunja uso na kunitazama macho ya hasira. Hakutaka kusikiliza jibu langu, alisimama na kuondoka.

Ajabu ni kwamba maneno yake hata hayakuingia kichwani kwangu. Ndo kwanza alinipa amsha amsha ya kuendelea kuipigania tamu yangu.

Unajua mpango wangu mwingine ulikua ni upi??
Nakuja………..


Soma Kitabu

SOMA MAELEKEZO

Bonyeza hi "Soma Kitabu" kisha itakupeleka kwenye fomu yaku login, hakikisha ume login na namba uliyojiunga nayo ndipo utaendelea sasa kusoma kitabu chote