HIVI UMEWAHI KUMPENDA MTU SANAAA, KIASI KWAMBA YAANI WEWE BILA YEYE MOYO WAKO HAUSOMI.
Lucas alipokuwa chuoni alitokea kumpenda sana msichana mmoja aitwae Edina, walianza mahusiano vizuri tu, kiasi kwamba kila mtu aliamini Lucas na Edina watadumu maisha yao yote, maana Lucas hakuwa na pesa za kutosha sana, na Edina alikuwa mrembo mno, Mahusiano yao yalikuwa ya dhiki lakini yalikuwa na nguvu kiasi kwamba hadi walipata mtoto wakiwa hawana hata pesa ya hospitali, wala pesa ya kutosha kula.
Baadae akatokea mtu wa tatu katikati yao Edina akuacha Lucas na kuamua kuwa na Nathan mwanaume tajiri na mwenye pesa nyingi sana, Lucas aliumia sana kwa sababu alimpenda sana Edina, kiasi cha kutaka kujiua, rafiki zake wakamsaidia akakaa sawa, hadi alipokutana na mwanamke mwingine aitwae Julieth, Julie alikuja kama Nuru na mwangaza mpya katika maisha yake, Julieth alikuwa mwanamke mwenye akili sana na alimpa mwanga zaidi Lucas akapata pesa na akawa tajiri mno, Ghafla tena akiwa katika kilele cha furaha yake na Julieth Edina akarudi kwenye maisha yake, hapo sasa Lucas akashindwa kuchagua, moyo unampenda Edina Maisha yanamtaka Julieth...... Soma moja mpaka mwisho bila kuacha ukurasa, utaelewa maana halisi ya neno KIRUSI CHA MAPENZI.
SIMULIZI: KIRUSI CHA MAPENZI
MTUNZI: SUMAIYA MWENDO
TUPO HAPA.
SEHEMU YA: 01
Saa nne asubuhi, vumbi la barabara ya kuelekea chuo kikuu lilikuwa bado halijakaa kabisa. Upepo ulikuwa mpole, ukicheza na matawi ya miti mikubwa ya miembe iliyozunguka jengo la maktaba kuu. Lucas alikuwa ameketi chini ya mti mmoja, mwenye kivuli laini kilichotoa hewa ya baridi inayoburudisha moyo. Miguu yake ilikuwa imekunjwa, mkononi ameshika kitabu cha Development Economics, lakini kwa dakika kumi mfululizo sasa, hajazungusha hata ukurasa mmoja.
Kichwani mwake kulikuwa na jambo jingine—au tuseme mtu mwingine. Edina. Mrembo wa mwaka wa pili anayesomea Social Work, mwenye tabasamu la kuvutia lililokuwa likitawala mawazo ya Lucas tangu siku ile alipomuona kwa mara ya kwanza akisalimiana na rafiki zake jioni moja katika viwanja vya cafeteria.
Lucas aliikumbuka siku ile kwa undani kama vile ilikuwa jana. Alivyokaa mezani akipiga stori na Freddie na Edgar, alishtushwa na sauti nyororo iliyopita kando yao. Alipoangalia, alikumbana na macho makubwa yenye nuru ya kipekee. Macho ya Edina. Muda ulisimama. Alijikuta akitabasamu bila kujua, na moyo wake ulianza safari isiyo na njia ya kurudi.
"Lucaas! Mbona leo umekaa kama unaota?"
Ilikuwa ni sauti ya Edina, ikimvuta kutoka kwenye mawazo yake.
Aliinua macho kwa mshangao, halafu akatabasamu, kwa aibu ya furaha. Edina alikuwa amesimama mbele yake, akiwa amevaa jeans nyembamba ya bluu iliyombana vizuri, na fulana nyeupe iliyoandikwa Be Kind. Nuru ya asubuhi ilimfanya ang'ae zaidi.
"Edina… hujambo?" Lucas alijibu kwa sauti ya kutojiamini, kama mtu aliyekamatwa akiutazama uzuri wa malkia bila ruhusa.
"Niko poa. Wewe je? Mbona unafikiria sana huku na masomo yamejaa kichwani?" aliuliza kwa tabasamu la dhihaka ndogo, lakini lenye mvuto.
Lucas alishusha pumzi taratibu. "Ni kweli, najifunza... lakini kuna kitu kinaniumiza kichwani."
"Kitu gani tena? Maswali ya uchumi au maisha kwa ujumla?"
Lucas alitabasamu, halafu akavua miwani yake ndogo ya kusomea. "Wakati mwingine... maisha. Kuna wakati unahisi mtu mmoja anaweza kubadilisha kila kitu kwako, lakini hujui kama na yeye anaona hivyo kwako."
Edina alinyamaza kwa sekunde chache, macho yake yakimtazama Lucas kwa makini. "Lucas, unamzungumzia nani sasa?"
Lucas hakujibu moja kwa moja. Aliinua uso wake, akamkazia macho. "Edina... kama nikuambie kwamba wewe ndiye unayesumbua mawazo yangu siku hizi, utanichukuliaje?"
Edina alishtuka kidogo, lakini akajizuia kuonyesha mshangao. Badala yake, alicheka kidogo, kisha akasema, "Wewe unajua kupiga mistari eeh? Haya, sema tu mapema kama unanitaka tujiue moja. mapemaaa."
Lucas alicheka pia, lakini ndani ya moyo wake, alijua haya si maneno ya kupitisha muda. Alikuwa tayari ameweka hisia zake juu ya Edina kwa muda mrefu, na sasa hakutaka kuchelewa.
"Sitaki tu nikujue… nataka kukujua sana, kwa undani zaidi. Nataka kukupenda, kwa namna ninavyojua kupenda. Nataka tupatane, tushirikiane, tuwe pamoja kwa muda mrefuu....."
Edina alimtazama tena, mara hii bila tabasamu. Alionekana kuguswa, hata kama alijaribu kuficha. Aligeuza macho chini, halafu akasema kwa sauti ya chini, "Lucas… mimi sijawahi kuwa kwenye mahusiano, na siwezi kusema kama niko tayari, lakini… siwezi kukudanganya nimewahi kukuangalia kwa jicho la pili pia."
Maneno hayo yalimpeleka Lucas mbinguni. Hakukuwa na furaha nyingine kubwa kama hiyo kwa wakati huo.
Siku hiyo waliamua kuanza urafiki wa karibu zaidi. Mazungumzo yao yakaongezeka, walitembea pamoja, wakasoma pamoja, hata kula lunch pamoja likawa jambo la kawaida. Miezi ikasonga. Mapenzi yao yakakua haraka kama maua ya waridi wakati wa machweo.
Lucas alikuwa mtu wa kawaida, alitegemea boom lake tu, lakini hakuwahi kumficha Edina kitu. Alimpenda kwa dhati. Alimpa kila alichoweza kumpa; muda wake, hisia zake, na hata plan zake za maisha.
Na Edina? Alikuwa akizidi kuvutwa kwake. Aliona upole, uaminifu, na msimamo wa kweli ndani ya Lucas. Alimpenda...
☆☆☆☆☆
Mwaka mpya wa masomo ulianza kwa kasi. Wanafunzi walikuwa wakisongamana kila kona ya kampasi, wakiharakisha kurekodi kozi, kuandaa ratiba, na kujitayarisha kwa safari ndefu ya kitaaluma. Kwa Lucas na Edina, huu ulikuwa mwaka wao wa tatu—mwaka wa matarajio makubwa, lakini pia mwaka ambao ungeleta mabadiliko yasiyotabirika.
Penzi lao lilikuwa limekomaa. Wote wawili walikuwa na uhakika mmoja juu ya mwingine. Ilikuwa kawaida kwa Edina kulala katika chumba cha Lucas siku za wikendi, na mara kadhaa Lucas alimfuata Edina hosteli akiwa amebeba chakula cha jioni alichopika mwenyewe kwa juhudi zote, japo wakati mwingine kiliungua.
“Lucas… unajua ungekuwa chef mzuri kama tu usingekuwa mbishi kwenye chumvi,” Edina aliwahi kumcheka usiku mmoja alipomletea wali wenye pilipili nyingi.
“Si niwe chef wako basi, nikupikie maisha yako yote,” Lucas alimjibu kwa utani, lakini moyo wake ulikuwa ukimaanisha.
Maisha yalikuwa ya furaha, yalikuwa laini, hadi siku ile Edina alipohisi kizunguzungu asubuhi kabla ya kwenda darasani.
“Huenda ni uchovu tu,” alisema huku akijituliza sakafuni kwenye choo cha wanawake. Lakini hali hiyo iliendelea kwa siku kadhaa—kichefuchefu, usingizi mwingi, na hamu ya vyakula vya ajabu.
Aliposikia harufu ya chipsi kutoka cafeteria na akahisi kutapika, hapo moyo wake ulianza kucheza ngoma ya hofu. “Hapana… haiwezekani,” alijisemea kimoyomoyo, lakini wazo hilo likazidi kumtafuna.
Jioni ile, baada ya mazoezi ya darasani, Edina alitoka kwa haraka na kuelekea pharmacy moja nje ya kampasi. Akinunua kifaa cha kupima ujauzito, moyo wake ulikuwa kama bomu linalosubiri kulipuka.
Aliingia chooni peke yake, akapuliza pumzi ndefu, kisha akafanya alichotakiwa kufanya. Dakika tatu zilihisika kama saa nzima. Alitazama kijiti kile. Mistari miwili myekundu ikajichora.
Kimya.
Machozi yalianguka bila kualikwa.
Alikaa chini, akashika tumbo lake. “Mungu wangu... sijajipanga. Lucas... atasemaje sasa? Atanipenda bado au? Tutasoma vipi sasa?”
Usiku huo hakumpigia Lucas kama kawaida. Alijifungia chumbani, akizima simu, akilia kimyakimya.
SEHEMU YA: 02
Siku iliyofuata, Lucas alihangaika. Alimpigia mara tano, alituma meseji, hata akaenda hosteli kumfuata, lakini Edina alijificha. Hatimaye, baada ya siku mbili, Edina alikubali kukutana naye.
Walikutana kwenye uwanja wa wazi nyuma ya maktaba, sehemu yao ya faragha.
Lucas alimkumbatia haraka, “Mbona unaniogopesha, Edina? Upo sawa?”
Edina alimtazama kwa macho yaliyovimba kwa kulia. Hakusema chochote kwa dakika moja nzima. Kisha akavuta pumzi, na kwa sauti ya kutetemeka, akasema:
“Lucas... nipo na mimba yako.”
Kimya kilitanda. Upepo ulipita kati yao ukichanganyika na hisia za mshangao, hofu, na mshituko. Lucas alitikisa kichwa kwa mshtuko.
“Umesema... mimba?” aliuliza polepole, kama mtu aliyesikia vibaya.
Edina alitikisa kichwa akithibitisha. “Ndio.”
Lucas alikaa chini, akaweka mikono kichwani. “Edina… mimi… sijui niseme nini…”
Edina alijua hofu ile. Alijua Lucas alitamani maisha bora, alitamani kumaliza shule, kupata kazi, kisha ndoa na familia. Sasa... ratiba yote imevurugika.
“Usijali,” alisema kwa sauti ya chini, akigeuza uso. “Nikileta mtoto huyu duniani, haitakuwa kwa sababu ninalazimika. Ikibidi ntaitoa.”
Lucas alinyanyua uso, akamtazama. “Unasemaje Edina? Umtow mtoto wangu umechanganyikiwa wewe? Unafikiri nitakuacha wakati kama huu? Ni kweli nimechanganyikiwa, lakini siwezi kukukimbia jukumu langu la kuwa baba kwa mtoto wangu mwenyewe. Sijawahi kumpenda mtu kama nilivyokupenda wewe. Tutapambana pamoja, sawa?”
Machozi ya Edina yalitiririka. Alimkumbatia Lucas kwa nguvu. “Asante Lucas… lakini bado naogopa sana…”
Lucas alishika tumbo lake kwa mikono miwili. “Tutakua wazazi, Edina. Nitajitahidi kadri niwezavyo wewe na mtoto wangu muwe salama." Edina alitabasamu na kujihisi haueni.
☆☆☆☆
Wiki chache baada ya kugundua ujauzito, maisha ya Edina na Lucas yalibadilika kwa kasi isiyotarajiwa. Kila kitu kilionekana kuwa tofauti. Darasani, Edina alijitahidi kuficha hali yake, lakini maumivu ya mara kwa mara, kichefuchefu cha asubuhi, na mabadiliko ya hisia vilianza kumuandama bila huruma.
Lucas alijitahidi kumsaidia. Alijifunza kupika vizuri zaidi, alihakikisha Edina hakosi folic acid wala matunda aliyokuwa akiyahitaji kila siku, na mara nyingine alifika hosteli kuleta chai ya tangawizi usiku wa manane alipokuwa akisumbuliwa na kichefuchefu kikali.
Lakini changamoto haikuwa tu za kiafya.
Uhusiano wao uliingia kwenye hatua mpya ya ukimya mwingi, hofu ya mustakabali, na mijadala mizito ya maamuzi. Je, wangeweza kuendelea na masomo? Je, familia zao zingeitikiaje?
Siku moja jioni, walikutana kwenye bustani ndogo ya nyuma ya hosteli ya wasichana.
“Lucas,” Edina alianza kwa sauti ya kusitasita, “nadhani tunahitaji kuwaambia wazazi wetu hili ni jambo zoto sana ujue?…”
Lucas alinyamaza kwa muda. “Ndio. Lakini… nitawaambiaje mama na baba? Wananitegemea. Wananiona kama mfano wa familia... na sasa, nimevunja kila matarajio yao alafu isitoshe wale ni wana dini sana.”
Edina alikuna paji lake kwa wasiwasi. “Na mama yangu ataniua. Alishaniambia mara nyingi, ‘Ukiniharibia jina, nitakufukuza nyumbani.’ Na sasa… sijui hata nianzie wapi.”
Siku mbili baadaye, mambo yalienda mrama.
Mama yake Edina, Bi Regina, alipigiwa simu na rafiki wa Edina aliyekuwa akimjua vizuri. Alikuwa amemuona Edina akitapika nyuma ya jengo la darasa na kugundua mabadiliko ya mwili wake. Bila kuchelewa, aliwasiliana na mama Edina, akimfahamisha kilichokuwa kikiendelea. Kuhusu kuumwa umwa hovyo kwa Edina.
Saa chache baadaye, simu ya Edina iliita. Alipoona jina la mama yake, moyo wake uliruka kama mtoto mdogo anayeona bakuli la adhabu.
“Hallo mama…”
“Edina,” sauti ya mama yake ilisikika ikiwa na baridi ya ajabu, “nimeambiwa habari za aibu kukuhusu. Je, ni kweli unajiuza chuoni hadi umepata mimba?”
“Mama! Hapana! Sijajiuza—”
“Basi ni ya nani hiyo mimba? Mwanafunzi mwenzio? Mhadhiri? Hivi ndivyo nilivyokufunza?” sauti ya mama ilibadilika kuwa ya kilio cha hasira.
“Mama, tafadhali… tusizungumze kwa simu. Naomba nikueleze uso kwa uso—”
“Sitaki kuona uso wako. Rudisha heshima ya familia yangu kwa kutoendelea na hiyo mimba. Au usirudi nyumbani kabisa.”
Simu ilikatika.
Edina aliinama taratibu, akaweka uso wake mikononi. Machozi yalimtiririka kimya kimya.
Siku hiyo hiyo, Lucas alipokea ujumbe mfupi kutoka kwa baba yake, baada ya kumwambia mama yake ukweli, alihofia Edina asije akapata matatizo alafu wakose msaada.
“Kesho usiku, tunakutana hotelini. Nataka maelezo ya hili ninalolisikia kutoka kwa mama yako.”
Alifika hotelini akiwa amejitayarisha kwa yote. Baba yake, Mzee Yohana, aliketi kwa ukimya mkali, macho yakiwa kama rada inayochunguza moyo wa Lucas.
“Lucas,” alianza kwa sauti ya utulivu hatari, “umekuwa ukinivunja moyo. Tulikulea kwa nidhamu na maadili ya ki dini kabisa, kukulipia ada ghali, na sasa… hii ndio zawadi unayotulipa si ndio? Umeacha kusoma, umekua baba kabla ya wakati wako?”
“ Baba…” Lucas alijaribu kuongea.
“Usiniite Baba. Nimekosa mtoto kabisa. Nitawasiliana na mama wa huyo binti ili tujue namna ya kusuluhisha hili, siwezi kuruhusu aibu mimi. Mtapata msaada tu wa mda. Lakini kama unafikiri nitakuhifadhi, na kulea wajukuu wa dhambi, sahau. Utawajibika kwa namna yako tu.”
Lucas alitikisa kichwa taratibu. “Sawa baba. Lakini mimi nampenda sana Edina na sitatoroka jukumu langu. Sitamwacha Edina. Sitamwacha mtoto wangu. Hata kama nitatengwa na nyie… nitapambana kwa ajili yake na mtoto wangu.”
Baba yake alimuona kama mjeuri sana kisha akamwambia " sawa ni wazi kwamba unajiweza sana, kwa sasa wewe ni baba ee? Basi usitegemee msaada wangu kwa namna yoyote ile"
Kilio cha familia kikawa sasa mzigo wao. Wiki zilisonga. Maneno ya watu yalianza kuenea chuoni. Wengine walimcheka Edina. Wengine walimkwepa Lucas. Walimu wengine walijifanya hawaoni hali yao.
Lakini Lucas na Edina walibaki pamoja. Usiku mmoja, waliketi kwenye benchi la bustani. Edina alikuwa ameshika tumbo lake kwa mikono miwili.
“Unadhani mtoto huyu atatuchukia kwa kumleta mapema hivi ilhali sisi wenyewe hatuna kwetu?” aliuliza kwa sauti ya huzuni.
Lucas alimwangalia kwa upendo. “Hapana. Atatupenda. Na tutapambana hadi siku ya mwisho ili asitukute katika mazingira magumu. Mapenzi yetu hayakuzaliwa kwa bahati mbaya. Lilikuwa ni chaguo letu.”
Edina akatabasamu kwa shida. “Unahisi tutaweza kuvumilia mitikasi, Lucas?”
“Tutaishi, Edina. Tutaishi kwa upendo kikubwa sisi wenyewe tunaelewana.”
SEHEMU YA: 03
Wiki zilivyosonga mbele, hali ya Edina ilizidi kuwa dhaifu. Tangu mimba ilipotimiza mwezi wa tano, afya yake ilianza kuyumba kwa kasi. Kichefuchefu kiligeuka kuwa maumivu ya mgongo, uvimbe wa miguu, na uchovu wa kupindukia hata baada ya kulala kwa masaa mengi bado hakuwa na hali, mbaya zaidi kusoma kwake ikawa mtihani.
Lucas alijitahidi kumsaidia, lakini uzito wa kila kitu ulikuwa ukimzidi taratibu. Alikuwa na mitihani ya katikati ya muhula, kazi za makundi, usiku wa kumchunga Edina, na wakati mwingine kumtafutia matunda ya kumpunguzia kichefuchefu hata saa tatu usiku.
Asubuhi moja chuoni, akiwa kwenye lecture ya ‘Financial Modelling,’ Lucas alitazama kioo cha simu yake kwa hofu—Edina alikuwa hajamjibu ujumbe wake asubuhi. Alishindwa kuvumilia. Aliomba kutoka darasani na kukimbia moja kwa moja hadi hostel ya wasichana mahali ambapo Edina aliishi na rafiki zake.
Alipofika, alimkuta Edina akiwa amelala sakafuni, akivuta pumzi kwa shida. Haraka alimchukua mikononi mwake na kumkimbiza kwenye kliniki ya chuo.
Dakika kadhaa baadaye, muuguzi alimtazama Lucas na kumwambia kwa upole:
“Shinikizo lake la damu ni la juu sana. Huenda ikawa hatari kwa mtoto pia. Tunahitaji apelekwe hospitali kubwa mara moja.”
Ghafla, Lucas alihisi dunia ikimzunguka. Alijua kuwa hakuwa na bima, wala hakukuwa na msaada kutoka nyumbani.
Usiku huo, akiwa ameketi kwenye kiti kigumu pembeni ya kitanda cha Edina hospitalini, alimtazama mpenzi wake aliyekuwa akipumulia mashine ya oksijeni. Mikono yake ilikuwa dhaifu, lakini bado ilikuwa ikimtafuta Lucas kwa mguso wa faraja.
“Mimi nipo hapa… usijali,” Lucas alinyamaza, akimshika mkono.
Saa tano usiku, alitoka hospitali na kuelekea kwa rafiki yake Jay, ambaye alifanya kazi kwenye mgahawa wa usiku.
“Bro,” Lucas alisema kwa sauti ya kukata tamaa, “nahitaji kazi. Hata ya kuosha vyombo. Hata ya kulinda parking. Nahitaji hela ya. Haraka.”
Jay alimwangalia kwa huruma. “Una hakika? Utaweza masomo na kazi usiku?”
“Sijali tena kuhusu masomo. Kama itabidi niache, nitaacha. Edina ni kipaumbele changu kwa sasa.”
Jay alikubali kumtafutia kazi. Usiku huo huo, Lucas alianza kazi ya kuosha vyombo kwenye mgahawa. Kila usiku kuanzia saa nne hadi saa kumi alfajiri, alikuwa akisugua sahani, sufuria na vikombe kwa mikono iliyojaa majeraha ya sabuni na maji ya moto.
Asubuhi, alikuwa anakwenda hospitali kumhudumia Edina. Wakati mwingine alikuwa akimlaza miguuni pake, kichwa chake kikiegemea kitandani, akingoja matokeo ya vipimo. Alikuwa mwanafunzi wa masomo ya fedha, lakini sasa alikuwa mwanafunzi wa maisha magumu—na sie na fedha kwa kweli.
Siku moja, akiwa kwenye korido ya hospitali, alikutana na Mwalimu wa masomo ya ‘Strategic Planning,’ ambaye alimkumbuka kwa sura iliyojaa uchovu.
“Lucas?” mwalimu alishangaa. “Nini kinaendelea? Umekua ukikosa madarasa yangu kwa siku kadhaa sasa. Na sasa nimekusikia unafanya kazi za usiku?”
Lucas alimtazama kwa macho yaliyojaa ukimya wa uchungu. “Ni maisha, mwalimu. Kuna vitu havielezeki darasani, ila unavijifunza kwa maumivu.”
Mwalimu alitikisa kichwa, akimtazama kijana aliyekuwa na ndoto kubwa lakini sasa akijvua hatua kwa hatua, Lucas alikuwa mwanafunzi mzuri sana kwenye darasa lake.
“Usikate tamaa, Lucas. Nakumbuka thesis yako ya mwaka wa pili, ilikuwa na maono makubwa. Usisahau ndoto zako—hata kama sasa umebanwa na majukumu. Kila mtu ana wakati wake wa kuanguka, lakini si kila mtu ana ujasiri wa kuinuka tena, jitahidi usianguke.”
Lucas alibaki kimya. Maneno hayo yalimchoma kama moto, lakini pia yalikuwa mwanga mdogo wa tumaini kwenye giza lake la sasa.
Wakati huo huo, Edina alianza kujua kuhusu kazi ya Lucas kupitia rafiki yao mmoja, Joyce. Alijisikia vibaya sana, akihisi hatia kuwa mzigo kwake.
Siku moja Lucas alipomtembelea hospitalini, Edina alisema kwa sauti ya huzuni.
“Siwezi kukuangamiza, Lucas. Najisikia hatia sana ikibidi Achana na hiyo kazi. Nirudishe nyumbani. Nitaenda kuomba msamaha kwa mama.”
“Hapana, Edina,” Lucas alisema kwa upole lakini kwa msisitizo. “Mimi siwezi kukuacha. Kama kuna mtu wa kuumia, ni mimi. Wewe umetosha sasa—na mtoto huyu anaekuhangaisha hivi sasa inabidi ajue tu kwamba amepata baba mpambanaji.”
Kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu, Edina alitabasamu kupitia machozi.
☆☆☆☆
Wiki mbili baada ya kulazwa, Edina aliruhusiwa kutoka hospitalini. Madaktari walikuwa wametoa angalizo la karibu—mimba yake ilikuwa katika hatari endapo asingepumzika vya kutosha, kula vizuri na kuwa na utulivu wa kiakili.
Lakini maisha ya Edina hayakuwa na nafasi ya utulivu huo. Hakuwa na pa kwenda. Wazazi wake walikuwa bado hawakubali maamuzi yake, na marafiki waliokuwa wakimuunga mkono awali, sasa walikuwa kimya kama kaburi.
Lucas hakuwa na fedha za kumkodishia Edina chumba, wala ndugu wa kumpeleka kwake. Kwa hiyo, alifanya uamuzi wa mwisho—kumpeleka kwao, hosteli za wanaume. Ilikuwa ni kinyume na kanuni, lakini kwa sasa, hofu yao kubwa haikuwa sheria, bali maisha.
Chumba cha Lucas kilikuwa kidogo, kitanda kimoja, meza ndogo ya mbao, na dirisha dogo linaloangalia ukuta wa jengo jingine. Hakukuwa na feni, wala kabati. Vitabu vilikuwa vimejaa kwenye sanduku la plastiki, na nguo zilitundikwa kwa msumari uliochomekwa ukutani.
Usiku wa kwanza, Lucas alimwambia Edina alale kitandani, yeye akajitanda blanketi chini. “Usijali, Edina. Siku nyingine tutayakumbuka haya maisha huku tunacheka, lakini kwa sasa, acha tuvumilie.”
Edina alinyamaza kwa muda. Macho yake yalikuwa yamejaa machozi, lakini hakulia. “Nashukuru kwa kila kitu, Lucas. Najua haya sio maisha tuliyo yategemea.”
Lucas alitabasamu, akavuta blanketi zaidi juu ya mabega yake. “Maisha niliyotegemea hayakuwa bora kuliko kuwa na wewe hapa. Hii mimba ni changamoto kwa upande mmoja, lakini pia ni neema kubwa si unaona inavyozidi kutosogeza karibu.”
Siku zilizofuata zilikuwa changamano. Lucas alilazimika kujificha akiwa na Edina hosteli, kwani usimamizi wa chuo usingekubali mwanafunzi wa kike kulala hosteli ya wavulana. Walitumia muda mwingi wa mchana library au uani, kisha kurudi chumbani usiku sana, Edina akiwa amejifunika buibui kubwa kwa ajili ya kujifichia.
Wakati huo huo, mitihani ya mwisho ya muhula ilikuwa inakaribia. Lucas alikuwa anakaa macho hadi saa nane usiku akisoma, kisha kuamka saa kumi kujiandaa kwa mizunguko ya kufanya kazi mgahawani. Usiku mwingine, alijikuta amelala akiwa ameshika kalamu mkononi, na kichwa juu ya daftari.
Edina naye alijitahidi kusoma kadri ya uwezo wake, lakini mimba ya miezi saba haikuwa rafiki kwake. Alikuwa na maumivu ya mgongo, mikono iliyovimba, na uchovu wa kudumu. Mara kadhaa, alijikuta akilia kimya kimya usiku Lucas alipokuwa kazini.
Siku moja, walipokuwa library, Edina alianguka ghafla. Lucas alikimbia huku akipiga kelele, “Mtu anisadie! Tafadhali!”
Baada ya muda mfupi, walifika hospitali. Daktari aliwatazama kwa huruma na kusema, “Hali ya Edina inahitaji uangalizi wa karibu. Hatuwezi kumruhusu arudi katika mazingira yenye msongamano na presha. Atahitaji kulazwa hadi atakapojifungua.”
Lucas alihisi moyo wake ukizama. Alijua gharama za kulazwa zilikuwa juu—hakukuwa na bima, hakukuwa na familia ya kumsaidia. Lakini hakuwa na chaguo.
Usiku huo, akiwa ameketi pembeni ya kitanda cha Edina, Lucas alishika mkono wake na kusema kwa sauti ya uchovu lakini imara, “Tutapambana, Edina. Kwa ajili ya mtoto wetu. Kwa ajili ya sisi.”
Edina alimkazia macho, akasema kwa sauti dhaifu lakini yenye tumaini, “Nisamehe Lucas, nimekuwa mdhaifu sana kwa mimba yangu ya kwanza tu… safari yetu ndiyo kwanza inaanza ila nakupa ugumu kila kukicha.”
Lucas alitabasamu na kusema. " hata hivyo mimi ndo sababu hadi leo hii, hausomi kwa amani unalazwa kila mara, na sasa inabidi ufanyiwe upasuaji kwa sababu tu nimekupa mimba, nisamehe Edina." Edina na Lucas mapenzi yao yalikuwa kama mbalamwezi angavu.
SEHEMU YA: 04
Siku iliyoanza kwa mawingu ya ukimya iligeuka kuwa dhoruba ya tukio. Ilikuwa saa moja asubuhi pale Edina alipolalamika kwa uchungu mkali wa tumbo akiwa kitandani hospitalini. Lucas, ambaye hakuwa amelala usiku kucha, aliruka kwa haraka na kuita wauguzi. Damu ilikuwa imeshaanza kutoka. Mimba ilikuwa imefikia wiki ya 36—hatari ilikuwa juu.
“Tunampeleka chumba cha upasuaji sasa hivi,” daktari alisema huku wahudumu wakimsukuma Edina kwenye machela.
Lucas alienda pembeni ya machela na kuushika mkono wake. “Nitakuwa hapa, usiogope mpenzi wangu. Tafadhali Edina, shikilia na ujikaze... kwa ajili yetu na mtoto wetu sawa mamaa.”
Edina aliinamisha kichwa taratibu. Hakuwa na machozi, lakini macho yake yalikuwa na tafsiri ya huzuni na matumaini kwa wakati mmoja. Mlango wa chumba cha upasuaji ukafungwa, ukimuacha Lucas akitetemeka kwenye kiti cha kusubiria, mara asimame mara akae.
Dakika zikawa masaa. Lucas alitembea huku na huko, akishika simu yake, lakini hakuwa na mtu wa kumpigia. Hakuwa na hata senti ya kulipia upasuaji. Alikuwa na shilingi elfu saba tu mfukoni—na yenyewe ilikuwa ya chakula cha Edina ataporuhusiwa kutoka reba.
Akiwa hana msaada, Lucas alifungua akaunti ya Instagram aliyokuwa amepost picha chache tu kwa miaka yote aliyoanza kutumia Instagram. Aliandika:
“Leo Edina yuko chumba cha upasuaji. Mchumba wangu, rafiki yangu, mwanamke wa ndoto zangu kipenzi changu. Hajala vya maana kwa siku kadhaa, hajalala vizuri kwa wiki, lakini leo anapigana—kumleta mtoto wetu duniani. Sina kikubwa cha kulipia huduma hii, lakini nina imani, moyo wangu, na maombi yangu zaidi. Mungu atatuwezesha kupitia nyie waungwana, na ikitokea nimesaidika basi nitaikumbuka siku hii milele. Tafadhali, yeyote mwenye msaada wowote... hata sala, tupo pamoja nae. Tunahitaji msaada.”
Aliambatanisha picha ya mkono wa Edina aliokuwa amemshika kabla ya kupelekwa chumba cha upasuaji. Dakika kumi baadaye, ujumbe huo ulikuwa umeenea kama moto nyikani. Wanafunzi wa chuo wakaanza kushiriki. Marafiki wa zamani wa Edina walimwona. Mmoja wao akamwandikia mdogo wa Edina ujumbe ambae ni Daniel —na ndani ya dakika 30, mama yake Edina, Bi. Regina, alipokea kiungo cha hiyo taarifa kwenye WhatsApp.
Kwa zaidi ya miezi mitano, hawakuwa wakizungumza na binti yao. Walikuwa wamehisi kusalitiwa, aibu na hasira. Lakini sasa, alipoona kile kilichoandikwa—na picha ya mkono wa binti yake akiwa kitandani kuelekea chumba cha upasuaji—alihisi ulimwengu ukimgeuka.
“Hii si kweli... Edina... mtoto wangu...” alilia kwa sauti, simu ikianguka mkononi. Baba wa Edina, Bwana Emmanuel, alikuwa kimya tu, ameshika paji la uso wake kwa mikono miwili.
“Sasa tuelewe... huyu Lucas... ana moyo wa namna gani?” Bi Regina aliuliza kwa sauti ya kulia, “Bila kitu chochote, bado amesimama na mtoto wetu...?”
Wakati huo huo, mlango wa chumba cha upasuaji ulifunguliwa. Daktari alitoka akiwa na tabasamu lenye uchovu.
“Ni mtoto wa kike. Mama yuko hai, japokuwa alipoteza damu nyingi. Tutamuweka ICU kwa saa chache kwa uangalizi, lakini amepona. Hongera sana Lucas."
Lucas alijihisi akishindwa kusimama. Alijiegemeza ukutani, akifuta machozi kimyakimya.
“Na kuhusu malipo?” aliuliza kwa sauti ya mashaka.
Daktari alimtazama kwa huruma. “Mtu ametuma kiasi cha awali kupitia benki ya hospitali. Alisema ni ‘familia ya mama mzazi wa Edina.’”
Lucas alipigwa na butwaa. Simu yake ikaita muda huo huo—namba ya simu ya kawaida ya nyumbani kwao Edina iliingia.
Alipojibu, sauti ya mama wa Edina ilisikika kwa sauti ya taratibu na yenye hisia:
“Lucas... pole kwa yote. Tulikuwa na hasira. Lakini sasa, tunaelewa. Asante kwa kuilinda roho ya mwanetu. Tuko njiani kuja hospitali.”
Lucas hakujibu. Koo lake lilikuwa limekauka kwa mshangao na maumivu yaliyopoa kwa faraja. Dunia ilikuwa imebadilika ndani ya saa chache tu. " Asante sana Mungu"
Edina alitolewa ICU usiku huo, akiwa na uso mchovu lakini wenye tabasamu la ushindi. Alipoambiwa wazazi wake walikuwa njiani, alilia kama mtoto mdogo.
“Na mtoto wetu?” aliuliza kwa sauti ya kicheko kidogo.
Lucas alishika mkono wake, akasema taratibu, “Mzima kabisa. Tumempata Arianna wetu, Edina. Tumeishinda dunia na vilivyomo." Edina alitabasamu akitamani kumuona binti yake mpendwa.
SEHEMU YA: 05
Saa kumi alfajiri, korido za hospitali zilikuwa kimya kama maktaba ya roho zilizochoka. Ndege wachache wa asubuhi walikuwa wakipita dirishani, na harufu ya dawa na sabuni ya hospitali ilikuwa imejaa hewani. Lucas alikuwa amelala kwenye benchi dogo nje ya wodi aliyolazwa Edina, akiwa ameukunja mgongo na kutojua ni lini alizama usingizini.
“Lucas...” sauti ya kike iliitisha kwa upole lakini kwa sauti yenye uzito.
Alipofumbua macho, aliona mguu wa mwanamke akiwa amevaa viatu vya heshima, kitenge cha heshima na uso wake ukionyesha kuzeeka kwa huzuni kidogo, si sana. Alipoangaza juu zaidi, alikutana na macho ya Bi. Regina—mama mzazi wa Edina.
Nyuma yake alisimama mumewe, Bwana Emmanuel, akiwa na uso wa kimya kimya, kama kuta za jela zisizo na sauti wala huruma. Walikuwa wamefika.
Lucas alinyanyuka kwa haraka, akashindwa kuamua kama apige goti au asimame kama mwanaume wa kweli. Mikono yake ilitetemeka.
“Shikamoo... mama... baba...” alijaribu kusema, lakini sauti yake ilikatika nusu.
Bi. Regina hakujibu mara moja. Alimtazama kwa sekunde kadhaa, macho yake yakijawa na machozi taratibu. Kisha akauliza:
“Edina yuko wapi? Na mjukuu wetu?”
“Wako salama,” Lucas alijibu kwa sauti ya chini, “Daktari alisema Edina ataruhusiwa kutoka ICU leo jioni... mtoto yuko kwenye wodi ya watoto wachanga... ni msichana.”
Machozi yakaanza kumtiririka Bi. Regina. Aligeuka na kumkumbatia mumewe kwa sekunde kadhaa, kabla hajamkaribia Lucas.
“Ulipigana peke yako. Ulibeba lawama zetu. Tulikushtumu kwa kuharibu maisha ya binti yetu, tukasahau kuwa ulikuwa sehemu ya wokovu wake kwa sababu haukumkana, sio rahisi kupata kijana kama wewe kwa nyakati za sasa Lucas, asante.”
Lucas alijaribu kuongea lakini alikosa maneno.
“Siwezi kufuta yote tuliyokutamkia. Lakini nashukuru haukukata tamaa,” aliongeza.
Bwana Emmanuel alikuwa bado kimya. Alimsogelea Lucas polepole, kisha akasema kwa sauti nzito lakini ya wazi:
“Huu si mwanzo tuliotarajia kwa binti yetu. Lakini ni ukweli tuliokutana nao. Na sasa tutalikabili hili pamoja.”
Lucas alishtuka kwa maneno hayo. Alikuwa tayari kupokea matusi, vitisho, hata kashfa. Lakini maneno hayo yalikuwa msamaha aliouombea kimya kimya kwa miezi.
“Natamani ningekuwa na nguvu ya kuwapa kila mlichokosa...” Lucas alisema, machozi yakimlenga. “Lakini kwa sasa, nina moyo tu. Na mapenzi ya kweli kwa Edina na mtoto wetu, naombeni mnisamehe kwa sababu sina mahali ya kuwalipa ili kumuoa Edina, ila tafadhali naombeni msiniweke mbali nae."
Baba Edina alitabasamu na kusema
"haina shida, kikubwa mmalize masomo yenu kwanza, na kwa sasa tutamchukua Edina akae nyumbani kwanza mpaka wakati atakapokuwa sawa, awe anatokea nyumbani." Lucas hakuwa na uwezo wa kumpinga baba yake mkwe.
Kimya kidogo kikafuata. Hapo ndipo mlango wa wodi ukafunguliwa polepole, na muuguzi akaweka kichwa nje.
“Lucas... mama wa mtoto wako ameamka sasa. Anataka kukuona.”
Bi. Regina alishika mkono wa Lucas, akasema kwa sauti yenye upole:
“Twende pamoja.”
Walipoingia wodini, Edina alikuwa amelala pembeni ya dirisha, macho yakiwa bado mazito lakini na tabasamu la kweli alipowaona. Alipowaona wazazi wake, machozi yakaanza kumtiririka.
“Mama... baba...” alitamka kwa sauti ya msononeko wa moyo.
Bi. Regina alikimbia na kumkumbatia binti yake. “Samahani, mwanangu... pole kwa kukutelekeza wakati ambao ulihitaji sana mapenzi yetu...”
Mzee Emmanuel alisimama kwa muda, kisha akaegama ukutani huku akisema kwa sauti ya kuumia:
“Hakuna mzazi anayefurahia kuona binti yake akiteseka... lakini hatujui kila wakati ni vipi tuwe sahihi. Sisi pia tulikosea kama binadamu.”
Edina alilia kwa sauti, akimkumbatia mama yake kwa nguvu. Lucas alibaki kando, akiwaangalia kwa upole, kisha akasogea karibu na kitanda, akamtazama Edina kwa macho ya mshikamano.
“Tunaweza kuanza upya, sasa si ndio ee?” alisema taratibu.
Edina alimpungia kichwa, macho yakiwa yamejaa mvua ya furaha na huzuni iliyoyeyuka.
Mtoto aliletwa dakika chache baadaye. Alikuwa mdogo sana, akiwa amelala kwa amani kwenye blanketi jekundu. Lucas alimbeba kwa mara ya kwanza akiwa na familia nzima pembeni yake—na kwa mara ya kwanza, hakujihisi kuwa peke yake tena. Alikuwa baba sasa, baba wa binti yake mrembo mno Arianna.
☆☆☆☆
Mwezi mmoja baada ya Edina kujifungua mtoto wa kike, ambaye Lucas alimpenda kwa moyo wake wote hata kabla hajamwona, hatimaye Edina alirejea chuoni. Ilikuwa ni siku ya Jumatatu yenye jua kiasi, huku upepo mdogo ukipuliza kwa upole, kana kwamba ulihisi kuwa mwanzo mpya kwa moyo wa binti huyo aliyeamua kuendelea na maisha yake ya elimu licha ya changamoto.
Alipofika chuoni, Edina alikumbatiwa kwa shangwe na rafiki zake wakina Joyce na Linda. Walimkimbilia kwa furaha, macho yao yaking'aa kwa mshangao na huruma mchanganyiko.
"Edinaaa! Kumbe umesharudi eeh? Hongera sana mama mtoto!" Joyce alimpapasa tumbo lake na kucheka.
"Hongera sana mrembo, lakini umependeza hata kuliko kabla ya ujauzito, jamani!" Linda aliongeza kwa furaha.
Edina alicheka, akiwakumbatia wote wawili. "Asanteni sana wapenzi wangu... sasa mimi ni mama, sio kama nyie ambao bado mnaishi maisha ya kuhangaika na vijana wa hovyo alafu mnachomoa watoto!"
Joyce alicheka sana na kumjibu kwa kejeli ya kimapenzi, "Tatizo siyo kuwa mama Edina... tatizo ni yule mwanaume uliyeamua kumzalia. Imagine wewe leo unatuvimbia kwa sababu ya mwanaume mwenyewe Lucas.?"
Wote walicheka lakini Edina alitabasamu tu kwa maumivu yaliyofichwa ndani ya kifua chake. Hakusema lolote, alibaki akiwatazama, kisha akasema kwa utulivu, "Kama mngemjua Lucas vizuri... msingesema maneno hayo. Kuna wanaume wachache sana kama yeye duniani."
Wakati huo huo, upande wa pili wa chuo, Lucas alikuwa ameketi kwenye moja ya benchi maarufu nyuma ya darasa la Uchumi. Alikuwa na Freddie na Edgar, marafiki zake wa karibu. Walikuwa wakizungumza kuhusu midterm test iliyokuwa karibu, lakini mazungumzo yalihamia kwa haraka kwenye jina la Edina.
"Bro, hivi umemuona Edina? Ameonekana chuoni leo, anaonekana poa sana," Freddie alisema huku akimeza mate ya mshangao.
"Nimemuona... anapendeza zaidi kuliko hata nilivyotarajia," Lucas alijibu kwa sauti ya kujidai.
Edgar alimkazia macho Lucas, kisha akasema, "Unajua lazima ujitahidi sana kimasomo na kimaisha ili uje kummiliki Edina ki halali. Huwezi kuwa na mwanamke kama huyo halafu ukaishi kwa matumaini tu. Atakukimbia bure shauri yako, mwanamke apewe hela bhana anogeshwe."
Lucas alitabasamu polepole. "Namwamini sana Edina. Nimeona upande wake ambao wengi hawaujui. Ni mwanamke wa kweli. Na sina shaka nae kabisa, alafu kwenye haya maisha sio rahisi kupata mwanamke kama yeye, lazima nitajitahidi kwa ajili yake, nitamfanya wa halali kwangu... rasmi, kihalali."
Freddie alibofya ulimi wake, "Una moyo mkuu kaka. Maana wanawake wengi wakishazaa na kuona life ni tough, wanahamia kwa wenye status zao. But you? Una imani ya ajabu na huyo mwanamke wako."
Lucas aliinamisha kichwa chake kidogo, macho yake yakitazama mbali. "Ninachojua ni kuwa... mapenzi ya kweli hayakimbii mateso. Yanavumilia. Na mimi nimechagua kuvumilia hadi mwisho."
Jioni hiyo, Lucas alimpigia simu Edina. Wakakutana sehemu yao ya kawaida, kwenye mti mkubwa karibu na zahanati ya chuo. Walikaa chini, Edina akiwa na mfuko wake wa vitabu. Lucas aliuchukua mkoba wa Edina akaufungua na kuweka bahasha. Edina akauvuta huo mfuko na kuichomoa bahasha haraka sana aliifungua na kuchunguza ndani kuna nini?
Alipochungulia akakutana na kiasi kikubwa cha pesa, Edina akaongea kwa sauti we Lucas, pesa yote hii umetoa wapi?
Lucas alikaa karibu yake akamwambia,
" Ujue Edina kwa sasa mimi na wewe ni wazazi, sasa kama nikibweteka na kuacha kufanya kazi kwa bidii wewe na Arianna mtaishi vipi hapo baadae? Kwanza kabisa nimefikiria kupanga chumba, lazima nitafute chumba cha kuishi tena sio chumba tu chumba na sebule ili tukimaliza tu chuo basi tuanze maisha yetu"
Edina alitabasamu na kumwambia Lucas hilo ni jambo jema, "lakini Lucas hakikisha kazi unazofanya ni halali na sio haramu, mi sitaruhusu binti yangu awe na baba muhalifu." Lucas alicheka kwa nguvu akamkumbatia Edina na kumbusu.
" siku moja moja nikiwa muhalifu sio mbaya ujue" Lucas alimwambia Edina akamng'ata lips zake. Kisha akainuka na kuanza kukimbia.
SOMA MAELEKEZO
Bonyeza hi "Soma Kitabu" kisha itakupeleka kwenye fomu yaku login, hakikisha ume login na namba uliyojiunga nayo ndipo utaendelea sasa kusoma kitabu chote