MIMBA YA MHUNI

book cover og

Utangulizi

Alyssa ni mwanamke tajiri na mrembo, lakini anakumbwa na taarifa ya kusikitisha kuwa ana uvimbe kwenye kizazi. Madaktari wanamwambia kama hatapata mtoto ndani ya miezi 11, atapoteza kabisa uwezo wa kuzaa.

Kwa kuwa hana mpenzi wala mume, Anaingia makubaliano na Kipo, huyu ni mhuni wa mtaani aliyetoka jela, ili ampatie mimba kwa malipo ya milioni moja.

Alyssa anapata mimba kweli, Lakini mambo yanabadilika. Kipo anaanza kumpenda Alyssa kweli kweli, na anamsumbua kila siku. Alyssa hamwamini kwa sababu anaona Kipo bado ni mhuni. Ivyo Kipo anamuonyesha Alyssa kuwa hata wahuni wanapenda tena vibaya mno.

Unadhani nini kitatokea??…..

SEHEMU YA : 1

Sauti ya viatu vya kisigino vya Alyssa ilivuma kwa ustadi wa hali ya juu katika sakafu ya marumaru, ikiambatana na harufu ya marashi ya bei ghali yaliyokuwa yakiwasha midomo ya pua ya kila anayempita.

Alikuwa kwenye lifti ya ghorofa ya ishirini, akiteremka taratibu kwenda ofisini kwake
ghorofa ya kumi na saba.

Watu wote waliomsalimia walipokelewa na tabasamu la kinafiki ambalo halikua kwa ubaya, bali kwa heshima ya namna alivyokuwa.

Alyssa Mushi. Mkurugenzi wa kampuni ya masoko ya kidigitali, mwenye historia ya mafanikio ya kuvutia kwa umri wake wa miaka ishirini na nane.

Lakini leo alikuwa tofauti. Macho yake yalionekana kufifia, huku mkono wake wa kushoto ukiwa tumboni mwake. Alijua tu mwili wake haukuwa sawa.

Alipofika ofisini, secretary wake kwa jina la Monica alimwangalia kwa wasiwasi.

“Madam, leo umeamka vibaya au kuna mtu kakukera?” aliuliza huku akimfuata hadi kwenye mlango🤨

Alyssa alijitupa kwenye kiti cha ngozi kilichochongwa kwa ufanisi.

“Tumbo langu linaniuma Monica… halijakaa sawa kwa wiki mbili sasa. Sijui kama ni stress au ni tumbo la hedhi lililozidi mipaka,” alisema kwa sauti ya unyonge.

Monica aliweka karatasi chini na kumtazama kwa dhati na kumuambia

“Naomba nikwambie kitu bila chenga, madam. Tafadhali nenda hospitali. Umevurugika. Angalau ukakague afya yako ila nasema si vibaya.”

Alyssa alifunga macho na kukaa kimya kwa sekunde kadhaa. Kisha alijibu kwa sauti ya chini

“Leo nina kikao sidhani kama ratiba yangu itaruhusu mimi niende hospitali”

“Usijali kuhusu kikao, mimi nitasimamia kila kitu! Ila tu nenda hospitali ukajue tatizo ni lipi”

“Okay, Mpigie Janelle uniwekee appointment nae. Leo nataka kuondoa hii sintofahamu.”

Baada ya appointment kuwekwa, Saa mbili baadaye, Alyssa alikuwa ameketi kwenye chumba cha ushauri cha daktari wake na rafiki yake wa karibu ambae ni Dr. Janelle Mwenda.

“Tumekutana kwenye dinner za kifahari, kwenye safari za kibiashara, kwenye spa za kitalii… leo umekuja kuniangalia mimi kama mgonjwa haya ni maajabu” Janelle alisema akicheka baada ya kumaliza vipimo☺️

“Please acha utani, tell me straight. Nini kinaendelea katika mwili wangu?”

Janelle alipumua kwa uzito, akavuta kiti karibu na kumsogelea Alyssa.

“Bestie, usinichukie kwa nitakachokuambia. Kuna uvimbe kwenye kizazi chako. Tumeukamata mapema lakini bado ni hatari. Na unazidi kuathiri uwezo wako wa kushika mimba”

Alyssa alitetemeka maana hakua akitegemea kama tatizo lingekua na uzito kiasi icho.

“Hiyo inamaanisha nini? Sitaweza kupata mtoto?” Alitoa macho😳

“Siwezi kusema kabisa hutapata. Ila kama hautafanya uamuzi wa haraka, unaweza kupoteza kabisa nafasi yako ya kuwa mama wa mtoto wako mwenyewe”

Kimya kizito kilitanda. Alyssa alishusha pumzi ndefu. Machozi yalikuwa yakimjaa jicho moja, ila alipambania yasitoke.

“Na suluhisho ni nini? Sitamani kabisa kukosa mtoto” aliuliza kwa sauti ya kujizuia isitetemeke🥺

Janelle alimtazama kwa muda, kisha akasema kwa sauti tulivu lakini yenye uzito

“Hapa matibabu ni upasuaji na tukifanya upasuaji basi tutalazimika kuondoa kizazi chako ili kuokoa maisha yako. So Naweza kukupa dawa za kuchelewesha upasuaji kwa miezi kumi na moja, lakini ndani ya muda huo unapaswa kuwa mjamzito. Mara tu utakapopata ujauzito, hatutafungua kizazi chako, tutatibu hatua kwa hatua. Kama hutapata ujauzito kabla ya muda huo kuisha hatuta kua namna zaidi ya kufanya tu upasuaji”

Alyssa alitabasamu kwa maumivu akamtazama rafiki yake usoni kwa mda mrefu kisha akasema

“Ivi Wewe hujui ama unajitoa ufahamu? Sina mpenzi. Siko kwenye mahusiano Na siwezi kuingia kwa pupa eti tu kwa sababu ya mimba.”

Janelle alisogea karibu zaidi akamwambia

“Sikiliza, Alyssa Unajua maisha siyo kama kitabu. Na kuna njia zingine. Kuna watu wanaamua kupata mtoto bila ndoa Au bila hata ya kua na penzi. Kuna wanaume wanaokubali kusaidia hilo kwa makubaliano. Kuna mtu ninamjua, jina lake ni Riki, anahusika kutuunganisha kwa wanaume wanao elewa hali kama yako. Wanaume wa kusaidia kupata mtoto tu tena kwa siri sana! Hakuna atakae jua”

Alyssa alimpiga Janelle jicho la ajabu. “Wewe unanitaka nilipe mwanaume alale na mimi ili nipate mimba?” 😳

“Sijakutaka, nimesema tu ni njia. Maana pia mimi nafanyaga ivyo. Lakini wewe unajua maamuzi ni yako. Haya ni maisha yako So pia Uamuzi ni wako.” Janelle alicheka

“Unanunua wanaume na wewe?” Alyssa alizidi kushangazwa na Janelle

“Ndio! Unadhani nani huwa ananitimizia haja zangu za kimwili?? Nikipiga simu moja kwa Riki ananitumia vijana wake na wanani ridhisha vizuri mno! Kwaiyo hio ndo njia iliyo baki”

“Naenda nyumbani. Ninahitaji kutafakari hili maana Hili jambo sio la maamuzi ya chapchap.” Alyssa hakutaka kuendelea kusikiliza maneno ya ajabu ya rafiki yake.

Janelle alimtazama kwa upole huku akiandika kitu flani kwenye faili lake la hospitali

“Nimekuweka kwenye dozi za awali za kudhibiti uvimbe. Lakini kumbuka, countdown imeanza. Ndani ya miezi kumi na moja hakikisha unashika mimba”

Alyssa hakujibu, alitoka kwa mwendo wa pole, macho yakiwa yamejaa mawazo. Alijua dunia yake imebadilika. Haikuwa tena juu ya mafanikio, pesa, safari au brands kubwa alizinazo, bali sasa ilikuwa juu ya kitu cha ndani zaidi ambacho ni maisha yake ya uzazi.

Usiku huo, alipokuwa amelala chumbani kwake, macho yakiwa wazi, kichwa kilijaa mawazo, moyo wake ukawa kama unaulizwa swali moja tu

“Je kweli nitaweza kulala na mwanaume nisiyempenda ili nipate mtoto wangu mwenyewe?”

Aliji garagaza kitandani kama mtu mwenye homa ya mapenzi ya kulazimishwa. Na mwishoni akaona akapate kwanza kahawa ya moto huenda akili yake itamkaa sawa.

Je Alyssa atafanya maamuzi gani??
Nakuja………

Sehemu ya 02

Alyssa alikuwa ameketi kwenye sofa lake la ngozi, akiwa amevalia gauni jeupe la hariri lililobana mwilini.

Mkononi mwake alikumbatia kikombe cha kahawa ya moto, lakini hakikuweza kufuta ubaridi alio uhisi ndani ya moyo wake. Alikuwa amekaa kwa zaidi ya saa moja, akiwaza, akihesabu, akijaribu kulinganisha maadili yake, imani yake, na hitaji lake la kuwa mama.

Hatimaye, akaweka kikombe mezani. Akavuta pumzi ndefu na kuchukua simu. Alitafuta jina la Janelle kwenye contact list, akabonyeza “CALL.” Na simu ikaanza kuita.

“Alyssa?” sauti ya Janelle ilisikika baada ya sekunde chache.

“Ndio, ni mimi”

“Unanipigia simu saa hizi umefanya maamuzi nini?” sauti ya Janelle ilionyesha matarajio.

“Nimeamua na Niko tayari! Nataka kupata mtoto wangu. Kama hiyo ndio njia pekee iliyobaki basi nitaifuata”

Janelle hakua akitarajiwa Alyssa kukubali kirahisi! Alishangaa na kujikuta mwishoni anacheka kwa furaha ya dhati.

“Mrembo, huo ni uamuzi wa kishujaa. Nitakutumia sasa hivi namba ya Riki. Usiogope. Ni muaminifu na yupo very discrete, na anaelewa sana namna ya kufanya kila kitu kwa heshima. We Mpigie”

Simu ilikatwa na Janelle akatuma namba zilizo andikwa kwa jina la Riki Fixer, Alyssa aliziangalia namba zilizotumwa huku Mkono ukianza kutetemeka na kuingiwa na uoga. Alizikodolea macho zile namba wee mwishoni akaikopi na kubonyeza kitufe cha kupiga.

Hakuita sana kwani ilipo kelewa na Sauti ya kiume iliyojaa kujiamini, ambayo ilisikikika ikisema

“Hello. Riki hapa”

“Hi naitwa Alyssa” alijibu kwa upole akivuta pumzi na kushusha kwa uoga. Alipojihisi anaweza kuendelea kuongea alisema

“Nimepewa namba zako na Daktari Janelle. Nataka kuongea na wewe kuhusu lile jambo”

Riki alinyamaza kwa sekunde moja tu. Halafu akasema, “Ndio, ameniambia. Pole sana kwa hali yako. Najua sio rahisi. Lakini nashukuru kwa ujasiri wako. Nataka unipe muda wa siku moja tu. Nitakutafutia mtu sahihi, halafu nitakupigia jioni”

“Okay asante” Alyssa alijibu. Alipoka simu, aliinamisha kichwa chake na kufumba macho. Moyo wake ulipiga haraka kama kengele ya hatari.

Siku iliyofuata upande wa gereza maarufu la kuwanyoosha vijana watukutu walio shindwa kula ugali mtaani kwa kutulia, zilisikika kelele za funguo kisha mlango wa chuma ulifunguliwa kwa kishindo.

Kipo alitoka na kusogea taratibu nje ya geti kuu, akiwa na mfuko mmoja mdogo wa plastiki na sura yake iliyochoka, macho yaliyodhoofika lakini bado yalikuwa na moto wa maisha ulioshindwa kufa.

Miaka mitatu gerezani ilikuwa imemkomaza zaidi ya miaka kumi mtaani. Alikuwa na umri wa miaka 30 lakini roho ya mtu mzima wa miaka 60. Alikuwa amejaa michoro ya tatoo mkononi na mgongoni kama ishara za historia yake ya kihuni na mitihani aliyoipitia mtaani.

Alipotoka tu, kitu cha kwanza alichofikiria ni mtu mmoja tu ambae ni Riki. Rafiki yake wa karibu tangu zamani. Mchonganishi na muunganishi wa madili ya pesa za kijanja, lakini mwenye moyo wa usiri kupitiliza.

Sehemu ni moja tu ya kumpata Riki napo ni maeneo ya kinondoni na huko ndipo alipo kwenda. Baada ya lisaa akafika hadi alipo Riki.

“Bro nimefulia kama pamba ya Kariakoo” Kipo alisema huku akitingisha kichwa. Hakutaka salamu wala kuulizwa maswala yake ya gerezani yeye alitaka dili la pesa tu. Alimtazama tena Riki akamuambia

“Na sina muda wa kulilia maisha. Nipe dili yoyote ya kuingiza pesa fasta. Hata kama ni ya kuhatarisha roho, niko tayari”

Riki alimtazama kwa macho ya mshangao na kuvuta pumzi ndefu.

“Uko serious?”

“Kama shoka! We nipange uone jinsi nitavyo baruza”

“Okay” Riki alisogea karibu, akamshika bega.

“Kuna mwanamke mmoja. Tajiri, mrembo, lakini ana tatizo la kizazi. Anahitaji mimba ndani ya muda mfupi. Hakutaki kwa ndoa wala penzi. Anataka mtoto tu. Anaweza kukulipa milioni moja ukikubali.”

Kipo alicheka sababu hakutegemea dili lingekua la namna ile

“Unamaanisha nimlale tu? Alafu analipa milioni moja? Bro, hiyo si kazi, hiyo ni baraka!”

“Ni kazi bro, kwa sababu ni ya heshima. Si porojo. Lazima umthamini, umheshimu, usimletee dharau. Mkataba wote wa mdomo, lakini ukiuvunja, unalipia kwa maisha yako! Na pia ni siri”

“Heshima mbele, japo mimi ni mtoto wa mtaa. Nipange nikutane naye lini?” Kipo alikenua meno😁

“Subiri nimpigie simu kwanza!” Riki alivuta simu yake akasogea pembeni akatafuta namba za Alyssa na kuzipiga

Wakati huo Alyssa alikuwa nyumbani amekaa kwenye kiti cha bustani ya nyuma, akichezesha vidole vyake kwa wasiwasi. Hakwenda kazini siku iyo maana aliona kabisa kazi zisinge panda.

Mara Simu yake iliita na alipo tazama aliona Riki akimpigia. Aliogopa, akajiweka sawa na kuipokea.

“Hello?” Alyssa aliitikia.

“Habari nzuri, dada Alyssa. Tayari nimepata mtu. Ana sifa zote. Ana afya nzuri, ameshafanyiwa uchunguzi wa awali, na yuko tayari kwa mpango. Kama upo tayari, tunaweza kupanga mkutano wa awali ili mzungumze. Utamwona kama anakufaa” Riki alidanganya kufanya vipimo ili tu asimfanye Alyssa awe na mashaka.

Alyssa alimeza mate kwa kigugumizi, akasita kidogo, kisha akasema

“Okay. Niko tayari kukutana naye. Lakini si eneo lenye watu wengi. Sitaki stress. Nipe muda wa siku mbili kujiandaa, alafu tutapanga”

“Deal” Riki alijibu kwa sauti tulivu.

Je, mkutano wao wa kwanza utakuwaje? Je, Alyssa atakubali kweli kulala na mwanaume wa aina ya Kipo?

Nakuja……….


SEHEMU YA 03

Mara baada ya kumaliza kuzungumza na Riki, Alyssa hakuwa na mwingine wa kuongea naye zaidi ya rafiki yake wa karibu kabisa. Alimpigia simu na
Alipoipokea simu, Janelle aliongea kwa sauti yenye uchangamfu

“Yes, shogile! Vipi tena?”

“Janelle nimeongea na Riki. Amesema amempata mtu. Jamaa atakutana na mimi siku mbili zijazo” sauti ya Alyssa ilikuwa na mchanganyiko wa wasiwasi na mashaka.

“Ahaaa! Hiyo ni hatua kubwa sana, baby girl. Hongera kwa kusonga mbele. Wewe ni jasiri kuliko unavyodhani. Trust me, you’re doing the right thing.”

“I hope so” Alyssa alijibu, kisha akakata simu kwa ahadi ya kumpigia tena baada ya mkutano.

Siku mbili baadaye katika Mgahawa wa Kimahaba wa Oysterbay ndipo ambapo Alyssa alipaswa kukutana na Kipo kama walivyo kubaliana.

Alyssa alikuwa amevalia suruali ya suti ya kijivu na blouse ya silk ya rangi ya cream, akafunika uso wake kwa miwani nyeusi kubwa kisha Akaingia kwenye mgahawa kwa tahadhari mno. Hakutaka ajulikane maana tayari alikua ana jina mjini.

Riki alikuwa tayari amemuelekeza kuwa atakutana na jamaa aitwaye Kipo.

Alipokuwa anaingia, macho yake yaligongana na kijana mmoja aliyeketi kona ya mwisho kabisa mwenye sura ya ukorofi, uso wenye toni ya chuma, macho ya mtu aliyewahi kupigana vita vya maisha, na mikono yenye tatoo za paka mwitu na maandishi ya “SURVIVE OR DIE”🤣

Huyo ndiye aliyekuwa Kipo sasa, jamaa wa kutisha tena mhuni kupindukia. Wahudumu wa mgahawa walishindwa kujizuia kutazama upande huo kwa wasiwasi.

Hakuna aliyesogea kumuuliza Kipo kinywaji alicho kihitaji sababu ya muonekano wake. Alyssa alipomtazama, moyo wake ulipiga kwa kasi. Macho yake yakaonekana kumshaanga. Hakuamini kuwa huyo ndiye mtu aliyepaswa kumsaidia kubeba mtoto wake wa kwanza😳.

Aligeuka, akachukua pochi yake kwa haraka na kutoka nje kabla hata hajaketi. Alipofika parking, alitoa simu yake fasta na kumpigia Riki

“Riki, yule jamaa hapana! Siwezi. Yuko kama jambazi. Hata siwezi kujiamini nikiwa naye chumba kimoja. Tafuta mtu mwingine” alisema Alyssa kwa uoga huku akitazama nyuma kila dakika

Riki alinyamaza kwa sekunde kadhaa, akatabasamu na kusema

“Alyssa, sikudanganyi. Kwa sasa hakuna mtu mwingine mwenye muda, afya nzuri, na aliye tayari kwa makubaliano yako. Yuko peke yake sokoni kwa sasa. Uamuzi ni wako”

Alyssa alikata simu bila kusema neno lingine. Kama mwanaume pekee aliebakia ni Kipo ambae angeweza kumpa ujauzito basi hakua tayari.

Alipanda ndani ya gari lake kisha huyoo akarudi nyumbani kupumzisha akili.

Usiku baada ya giza kuingia Alyssa alimpigia Janelle tena, na Mara hii waliwasiliana kwa video call.

“Sister, huyo mtu! Mungu wangu! Hata sura yake inanitisha. Mdomoni anaonekana mtu wa kuua, yaani siwezi!”

Janelle alicheka kwa sauti ya juu huku akigara gara kwenye kochi lake. Hakuwai kuona Alyssa akiwa muoga namna ile. Na jinsi alivyo mpa sifa za Kipo ndo akajikuta ana cheka zaidi.

“Alyssa! Wewe ni mtoto sana. Unataka mwanaume anayefanana na Barbie? Mwanaume legelege? Umesahau lengo lako? Huyu sio mume, bali ni project ya mtoto Na kwa taarifa yako, sura ya mtu haihusiki na sperms zake!”

“Lakini Janelle, ungemwona! Watu hata walikuwa wanamtazama vibaya mgahawani! Wallah ukimuweka mbele ya mtoto mdogo lazima alie nusu ya kuzimia”🤣

“Then that means you did good! Wewe mtu aliyepitia mengi kama huyo ana nguvu ya kuzalisha mapacha kumi! Kama kweli unataka mtoto, hiyo ndio njia. Vinginevyo, subiri miaka kumi uanze kusema ningejua”

“Hata kama Janelle yule kaka ni jambazi ujue”

“We una angalia muonekano ama shida yako ni mtoto? Mda unasogea na kwa kuchagua kwako utajikuta miezi kumi na moja inaisha na hujapata mimba! Embu Alyssa be serious”

Maneno hayo yalimgonga sana. Alyssa alikaa kimya, moyo wake ukichanganya mantiki na hofu. Hakulala usiku huo kabisa alikesha kuwaza.

Upande wa pili kwa Riki Kipo alikuwa amechukia vibaya mno.

“Bro, huyo dada alinikimbia kama nimevaa bomu. Hata hakusema neno, akapotea tu!” Alilalamika Kipo🤣

Riki alimpiga kofi la mgongoni na kucheka.
“Bro, usijali. Wanawake wa aina hiyo huwa wagumu mwanzo. Ila ukweli ni kwamba umeacha impression kubwa. Yaani siamini nimesikia ukimzungumzia vizuri hivi”

“Bro, ukweli? Huyo demu ana class. Ana ile vibe ya binti mwenye kila kitu lakini bado anatafuta maana. Ananivutia ile mbaya”

“Kipo, wewe sio mtu wa kusema mambo haya. Kila demu huwa unamchezea kama karata. Huyu vipi tena?”

“Sijui! Kuna kitu tofauti kwake. Kuna huruma. Kuna uzuri wa roho. Kuna kitu kinachonifanya nikose amani”

Riki akaanza kucheka, ni mara ya kwanza kwa Kipo kumuongelea mwanamke kwa undani namna hiyo. Alimuangalia tu na kuamua kunyamaza.

Siku iliyofuata asubui Alyssa aliamka mapema na kumpigia Riki. Alimua kukubaliana na hali! Na kama Kipo ndo njia peke ya yeye kupata mtoto basi alikua tayari.

“Riki niko tayari! Aje kesho Golden Glow. Nimeshabook chumba. Sitaki presha. Nataka kila kitu kiwe safi!” Alisema kwa kujiamini japo alikua na uoga

“Noted! Nitampa taarifa, una kingine cha kusema??”

“Ni siri sana! Usiri ni kitu kikubwa” aliongezea Alyssa

“Fresh!” Riki alipomaliza kuongea na Alyssa alimtafuta Kipo na kumpa taarifa pamoja na maagizo aliyo yatoa Alyssa

Basi Siku ya Miadi ikafika, Ndani ya Golden Glow Hotel aliingia Alyssa akiwa amejiandaa. Alikuwa na begi dogo la nguo za kubadilisha, manukato ya kifahari, na moyo wa ujasiri.

Alichagua chumba cha ghorofa ya tano, sehemu tulivu isiyokuwa na kelele. Aliwaambia wahudumu kuwa atakuwa na mgeni usiku huo, na asisumbuliwe.

Alijiweka vizuri, akavaa gauni fupi laini la hariri lililoacha bega moja wazi, kisha akatazama dirishani huku akishika glasi ya wine nyekundu.

Moyo wake ulichanganya hofu, wasiwasi, na tamaa ya kuwa mama.

Aliposikia mlango ukigongwa hofu ikatanda zaidi.

Je nini kitaendelea???
Nakuja……..


SEHEMU YA 04

Mlango wa chumba cha hoteli ya Golden Glow ulipogongwa, moyo wa Alyssa uliruka kama mlango wa benki.

Alisogea taratibu, akavuta pumzi ndefu, kisha akaenda kufungua. Macho yake yalipokutana na macho ya mwanaume aliyesimama mlangoni, aliduwaa.

Mwanaume alikuwa amevaa t-shirt nyeusi, suruali ya jeans iliyochakaa, sneakers aina ya Air Force zenye vumbi. Mkono wa kushoto ulikuwa na ile tattoo kubwa iliyoonesha paka mwitu, na mgongoni kulionekana kuchungulia tatoo nyingine nusu.

Alikuwa amenyolewa vizuri, lakini macho yake yalikuwa mazito kama mtu aliyelaaniwa na maisha. Huyu sasa ndiye alikuwa Kipo. Yulee alie mkimbia kule mgahawani😂

“Dah! Kumbe wewe ndo dada mwenye hela ya kunilipa milioni moja ili nikulaze?” alitamka kwa sauti ya kejeli, huku akimuangalia juu chini bila aibu.

Alyssa alikosa cha kusema. Akajitahidi kujiweka sawa ili asichukizwe na maneno ya Kipo yenye dharau.

“Ndiyo! ingia tafadhali.”

Kipo akaingia bila haraka, macho yake yakichunguza kila pembe ya chumba. Kisha akasogea kwenye kochi na kujibwaga.

“Kweli dunia imeharibika. Hadi mabosi wa kampuni mnaamua kutafuta watu kama sisi kwa kazi kama hii. Au ndo masharti ya kupata mtoto wa kitaa?”

Alyssa alikosa pa kuanzia. Alimwangalia yule mwanaume kwa mshangao, hasira, lakini pia mshangao mwingine usioelezeka. Alijikaza na kumkabidhi bahasha.

“Milioni yako hii hapa. Sitaki kuwe na makosa yoyote”

Kipo akaipokea bahasha ile na kuiweka pembeni kwenye meza, bila hata kuitazama. Hakuonekana kama mda huo alikua akijali kuhusu pesa.

“Usijali! Sitavuruga dili. Ila naomba tu unielewe kitu kimoja” alinyanyuka taratibu, akakaribia mahali alipokaa Alyssa na kusema

“Mimi siyo wa kuchezewa. Sitaki mchezo wowote, ukinichezea na mimi nakuchezea pia”

Alyssa alikunja uso, akijizuia kumjibu. Kisha akasimama na kujipeleka bafuni kujiandaa kwa yaliyo mbele. Moyoni alijutia kwa sekunde kadhaa, lakini hakuweza kurudi nyuma. Alishafanya maamuzi.

Alipotoka bafuni tukio lenyewe likafuatia sasa, Hakukuwa na mapenzi. Kilichotokea hakikuwa cha hisia bali kilikuwa ni kazi. Na kazi hiyo ilifanyika kwa ustadi wa hali ya juu mpaka ikamalizika.

Alyssa alipofumbua macho alfajiri, alikuta chumba kimya. Aligeuka upande wa pili Kipo hakuwepo. Lakini zaidi ya yote, bahasha ya hela ilikuwa pale pale mezani haikuguswa hata kidogo.

Alinyanyuka kwa haraka, akajifunika shuka huku moyo wake ukianza kuchanganyikiwa😳.

“Kwa nini hakuichukua hela? Hakutaka? Ana mpango gani? Alikuwa na madhumuni mengine?”
Akiwa bado anapigana na mawazo, akachukua simu yake na kumpigia Janelle.

“Hello?”

“Janelle nimeamka, Kipo hayupo. Hela hajachukua.”

“Hujui watu wa mtaa? Labda hajapendezwa, au kaamua kukutega. Kwani alikuumiza?”

“Hapana, sivyo. Ilikuwa kawaida tu. Lakini sijui kwa nini nahisi si sawa. Nahisi kuna kitu kinakuja…”

“Tulia Alyssa. Muda si mrefu tutajua kama umepata ujauzito au la. Kipo ni historia sasa, na kama hajachukua hela ni kivyake”

“Sawa kama ndo ivyo”

Baada ya simu kukatwa Janelle naye akampigia Riki.

“Riki, msela wako kaacha hela. Hii dili imeisha. Sitaki tena kumsikia! Wala usumbufu”

“Kipo kaacha hela?” Riki mwenyewe alishangaa, alikumbuka Kipo alipotoka tu gerezani alidai anataka dili la pesa! Amefanikiwa kupata dili na pesa kaacha!

“Ndo ivyo! Kaacha pesa na sisi hatutaki usumbufu”

“Fresh nitamuambia”

Dakika chache baadaye, Kipo aliingia kwa Riki akiwa na t-shirt yake ile ile ya jana usiku na harufu ya sigara.

“Brooo! Ilikuwaje usiku?” Riki alimshangaa😳

Kipo hakujibu. Badala yake alichomoa sigara mfukoni na kuichoma pale pale sebuleni. Alivuta kwa hasira, kisha akamtazama Riki kwa jicho la dharau.

“Namtaka huyo demu.”

“Alyssa?”

“Ndio. Nipe namba zake.”

Riki alicheka kwa mshangao.

“Bro, una akili timamu? Dili lilikuwa moja tu. Tena hela uliikataa. Huyo demu hawezi kupoteza muda na mtu kama wewe”

“Sina muda wa kubembeleza. Nipe namba zake”

“Kipo, hiyo ni ishu ya kifamilia sasa. Mimi sikupi. Nimeshamaliza kazi yangu! Umekataa pesa kausha usubiri kazi nyingine”

Kipo alikaa kimya , akavuta sigara nyingine haraka. Riki alipogeuka kwenda jikoni, Kipo akanyata kimya kimya, akachukua simu ya Riki na kuingia kwenye contact list.

Alipoiona namba ya Alyssa iliyoseviwa Alyssa Client macho yake yakang’aa kama mwizi aliyeona almasi. Akaichukua fasta, akaijisave kwenye simu yake mwenyewe, kisha akatoka bila kusema neno.

Wiki kadhaa baadae Alyssa alikuwa ofisini akisubiri kwa hamu kuona matokeo ya kazi aliyo ifanya siku za nyuma. Alishasahau kabisa kuhusu Kipo na akili yake mda huo iliwaza mtoto tu!

Akiwa ofisini simu ilianzaa kuita! Ni namba mpya ambayo haikua ime seviwa kwenye simu yake. Alijiuliza sana ila mwisho aliipokea.

“Hello?”

“Ningependa kujua uko wapi. Sitaki mtu mwingine akuangalie. Kuanzia sasa, mimi ndo baba wa watoto wako.”

Sauti ya Kipo ilisikika kama bomu lililorushwa ghafla tena bomu la nyuklia. Alyssa alipigwa na butwaa. Hakujua aanzie wapi. Kwanza alijishtukia kwa namna alivyotamka maneno hayo. Halafu akajiuliza ni NANI KAMPA NAMBA YAKE?

Kwa hasira kali, alikata simu na kuiangalia kwa sekunde kadhaa, kisha akaifungua na kuiblock haraka.

“Huyu mwanaume atananitaka nini jamani? Si tumeshamalizana na pesa alikataa kuchukua?” Alijiuliza Lakini hakujua mzimu wa mtaa ulikuwa umeshaingia kwenye maisha yake na huo ulikuwa ni mwanzo tu.

Je nini kitaendelea???
Nakuja……..


SEHEMU YA 05

Japokuwa Alyssa alimblock na kuendelea na maisha yake, bado sauti ya Kipo ilikuwa ikimjia kichwani kama sauti ya msanii anayepiga mziki mzito kichwani kwake.

Na uoga pia ulikuwepo wa kutosha sababu Kipo hakua mwanaume wa kawaida.

“Unafikiria nini Aly?” Janelle aliuliza huku wakitembea taratibu kwenye korido ya hospitali, hatua chache kabla ya kuingia kwenye chumba cha vipimo.

“Nafikiria kama hiki nilichofanya ni sahihi na kama kweli kimefanikiwa” sauti ya Alyssa ilikua ya kutojiamini.

Janelle alimsogelea na kumshika bega “Ulitaka mtoto, na ulichukua hatua. Leo tutajua, relax”

Baada ya vipimo, walikaa kimya ndani ya chumba cha kusubiri majibu hadi daktari alipoingia na tabasamu pana usoni.

“Hongera Alyssa, you’re pregnant (ni mjamzito)”

Alyssa alishtuka kwa furaha “What? Are you sure?!”

“Absolutely! Ujauzito wa wiki tatu. Mtoto wako yupo njiani”

Alyssa alijikuta akilia kwa furaha. Janelle alimkumbatia, na wote wakicheka kwa shangwe.

“Tunaenda kula! Tunaenda kuogelea! Leo ni leo!” Janelle aliongea kwa kumaanisha tena mwenye furaha.

Wakatoka hospitali moja kwa moja na kuelekea beach resort. Alyssa alivua huzuni zote, akavaa swimming costume nyekundu (nguo za kuogelea), akacheza huku akitembea mchangani, akiangalia bahari kama vile alikuwa anamuonyesha mtoto wake anayeanza ndani ya tumbo uzuri wa dunia.

Lakini upande mwingine wa jiji, Kipo hakuwa na hata chembe ya furaha.

Alikua anakula mihogo ya kuchoma na kuvuta sigara kali, macho yakiwa hayajatulia.

“Riki, nimemwelewa huyu demu. Sasa anajifanya kuniblock? Ana mimba yangu ama lah? Nataka kujua”

Riki alimtazama Kipo kwa muda na kuzidi kushangazwa nae😳

“Buda, we unapagawa! Makubaliano yalikua ni pesa kisha upotee! Sasa masuala ya kutaka kujua kama ni mjamzito yanaingiaje hapa?

“Nataka kujua. Nataka pia kumuona Lakini sijui anakoishi! Fanya mpango nijue nampata wapi”

“siri ya ofisi! Siwezi kutoa taarifa za mteja”

“Aaah! Unazingua! Nambie anapoishi kisha mimi na wewe tutamalizana kisela!”

“Mi simjui sana huyo demu maana Aliunganishwa kwangu na rafiki yake Janelle. Ila Janelle namjua vizuri. Namuunganishia machalii kadhaa wakampe mambo! Sema kama unataka kujua ni wapi huyu manzi anakaa basi anzia kwa Janelle! Anafanya kazi kwenye ile hospitali ya HerMed.”

“Bonge moja la wazo! Nitalifanyia kazi” Kipo alipiga pafu lingine la sigara akitabasamu kidogo.

Kwa siku tatu zilizofuata, Kipo alimfuatilia Janelle bila yeye kujua. Alimwona akipanda gari, akitoka kazini, akienda salon, mpaka siku alipomuona akimtembelea Alyssa nyumbani kwake hata kazini kwake. Pale pale akajua nyumba ya Alyssa ipo wapi na wapi anapo fanyia kazi. Na ilipo fika siku ya tano, Kipo alichukua hatua.

Alivaa bukta ya jeans, buti za ngozi, tisheti nyeusi iliyoonyesha tattoo zake za paka mwitu na fuvu kisha akaelekea ofisini kwa Alyssa.

Alipofika kwanza akajibusti kwa kuvuta sigara akiwa nje ya jengo la ofisi ya Alyssa. Walinzi walipomuona, walirudi nyuma. Macho ya Kipo hayakutaka maelezo bali yaliamuru.

“Alyssa yupo?” aliuliza kwa sauti ya kibabe, akitoa moshi mwingi wa sigara mdomoni

“Eeh… eeh yupo… ofisi namba kumi na saba” mlinzi mmoja alijibu kwa kigugumizi na kutetemeka😰

Kipo hakupoteza mda akazama ndani ya jengo, watu wakamshangaa na kuogopa huku kila mmoja akijaribu kuubana vizuri mkoba wake kwapani wakidhania ni mwizi.

Na Kipo hata hakujali, alichukua lifti na sigara yake mdomoni hadi juu kabisa ofisi namba kumi na saba.

Lifti ilipofunguka Kipo akatoka na kukutana na ofisi iliyo changamka kwa kujaa wafanyakazi. Hakuuliza maana ofisi ya Alyssa ilionekana vizuri ikiwa na jina lake mlangoni.

Kipo aliusukuma mlango akaingia ndani kama mtu mwenye hati miliki ya jengo. Alyssa alipogeuka na kumuona, alisimama ghafla. Mapigo ya moyo yakaanza kumuenda mbio huku kijasho chembamba kikimtoka

“What the_Kipo? umeingiaje ofisini kwangu?”

Kipo hakujibu! aliketi kwenye kiti cha mbele yake, akainua miguu na kuiweka juu ya meza ya Alyssa kana kwamba ni sofa la ghetto. Macho yao yalitazama na ndipo akasema

“Kwanini umeni block?” aliuliza kwa sauti tulivu lakini yenye uzito wa amri.

Alyssa alinyamaza bila kujua amjibu nini. Kipo aliendelea kusema

“Na swali la pili, una mimba au lah?”

Alyssa alihisi moyo ukimdunda kwa nguvu. Huyu mwanaume, aliingiaje ofisini kwake kwa jeuri hii? Akakumbuka alivyolala naye usiku ule, macho yake yalivyokuwa yakiangalia uso wake kwa makini kabla hawajalala. Akakumbuka bahasha ya pesa aliyompa na jinsi alivyoipokea bila kujali.

Lakini pia akakumbuka alivyoamka asubuhi na kumkuta Kipo hayupo na bahasha ya pesa ikiwa pale pale. Hakuchukua hata mia moja.

“Kipo..” Alyssa alianza kwa sauti ya upole akasema

“ulipaswa kuchukua ile pesa na kuondoka. Huu mpango ulikua wa muda tu! Sioni kama tunapaswa kusumbuana”

“Mpango ulikua wa muda, lakini mimba haikua ya muda” alijibu akinyanyuka na kusogea mbele kidogo akamtazama Alyssa kwa ukaribu.

“Toka kwenye ofisi yangu Please” Alyssa aliongea kwa hasira iliyo changanyikana na uoga ila Kipo
Hakua ameuliza swali lake la pili.

“Una mimba, Alyssa? Nambie ukweli! Tulicho kifanya kule hotelini kimezaa matunda??”

Alyssa hakuweza kujibu Alibaki kimya akimshangaa Kipo! Habari za yeye kutaka kujua kama ana mimba ziliingiaje pale ikiwa hayakua makubaliano!

“hili halikuhusu! Tulikubaliana ulale na mimi, nikulipe kisha kila mtu ashike njia yake! Haya sio makubaliano Kipo”

“Kwaiyo una mimba sio! Vizuri!! Tunakwenda kuwa familia sasa jiandae”

“Familia na nani?? Ivi unajisikia unacho kisema??”

“Wewe ni wangu! Na huyo mtoto ni wangu!”
Kipo Akageuka na kutoka!

Alyssa alikaa kwenye kiti chake, moyo ukimdunda. Ni wazi Kipo alitaka zaidi ya makubaliano yao! Na mda huu hadi alimfuata ofisini kwake bila uoga!

Je nini kitaendelea???
Nakuja……..


Soma Kitabu

SOMA MAELEKEZO

Bonyeza hi "Soma Kitabu" kisha itakupeleka kwenye fomu yaku login, hakikisha ume login na namba uliyojiunga nayo ndipo utaendelea sasa kusoma kitabu chote