Naitwa Monroe Abeli.
Mzaliwa wa familia tajiri ya wachimbaji wa madini, tumelelewa kwenye misingi ya heshima, hofu, na ndoa za kupanga.
Kwetu sisi, ndoa haimaanishi mapenzi.
Inamaanisha mikataba. Mipango. Faida.
Miezi sita iliyopita, nilipangiwa kuolewa na mwanaume nisimfahamu.
Nilikuwa na miaka kumi na tisa.
Na nilikimbia.
Nilikimbia usiku, nikapotea kwa siku tatu, nikiwa na mkoba mdogo na mioyo yangu miwili—hofu na uhuru.
Nilipatikana na kurudishwa nyumbani lakini wazo la ndoa lilifutwa.
Lakini sasa...
Ni zamu ya mdogo wangu Alice.
Na yeye analazimishwa kuolewa.
Wakati huu, mchumba anayepangiwa ni Nico De Monte.
Mwanaume mzuri mtanashati anavutia mrefu mwenye kufua kipana na analijua hilo kama yeye ni mzuri ndio kinachompa jeuri.
Niite kichaa.
Sababu najua haifai.
Lakini nadhani…
Nampenda shemeji yangu.
Najua.
Si ruhusa.
Si sahihi.
Lakini moyo haumilikiwi na sheria.
Na kadri ndoa yao inavyokaribia, ndivyo moyo wangu unavyogeuka kuwa uwanja wa vita.
Swali ni moja tu:
Je, nitaweza kujizuia?
Au mapenzi haya ya mwiko yatanimeza kabisa?
Songa na hadithi hii —
ugundue kinachotokea wakati moyo unapigana na heshima, familia, na mipaka ya maadili.
SURA YA KWANZA — MONROE
Jua la jioni lilikuwa linapenya kwenye madirisha ya sebule kubwa ya kifahari nyumbani kwetu, likitoa mwanga wa dhahabu uliopambanisha mapazia meupe ya hariri na ukuta wa rangi ya krimu. Tulikuwa tumerudi kutoka ibada ya Jumapili — ibada ambayo ilinifanya nijisikie mbali, siyo kwa sababu ya sala au mafundisho, bali kwa sababu ya kile nilichohisi nilipomuona Nicholaus De Monte kwa mara ya kwanza.
“Nashangaa, Monroe,” sauti ya mama yangu ilisikika kwa utulivu lakini ikiwa na mshangao uliofichika ndani yake. “Mbona ulitoka kanisani mapema hivyo? Hukusubiri kutambulishwa kwa shemeji yako mtarajiwa.”
Nilijifanya kutabasamu, nikitazama kiganja changu badala ya macho yake. “Nilikuwa nimechoka, mama. Nilihisi kizunguzungu kidogo. Nikaona bora nirudi nyumbani mapema kupumzika.” Nilijua ni uongo, na naamini mama naye alihisi hivyo. Lakini hakuwa na muda wa kuchimbua zaidi.
Mama alinipatia taarifa hiyo kwa wepesi kana kwamba ilikuwa jambo dogo:
“Nicholaus anatarajiwa kumuoa mdogo wako Alice. Wazazi wamekubaliana. Ndoa itafanyika ndani ya week 4.”
Nilihisi damu ikinikimbia usoni. Mapigo ya moyo wangu yalichanganyikiwa. Alice? Nilijua mdogo wangu anapenda mtu mwingine — Ethan, mtunza bustani wetu. Mvulana mpole mwenye macho ya kahawia, na tabasamu la aibu ambalo nililiona mara nyingi likimwangukia mdogo wangu. Lakini Ethan si wa hadhi ya familia ya Abeli. Kwa baba, hilo ni kosa la kufukuzwa mtu kwenye familia.
Sikusema neno. Nilimeza pumzi ndefu na kutazama kutoka dirishani, nikikumbuka kile kilichotokea kanisani.
Nilimuona. Nicholaus. Akiwa amesimama mbali kidogo na baba yangu, wakiwasiliana kwa ukaribu kama watu waliokuwa wakijua mustakabali wa familia yetu. Alivaa suti ya buluu iliyomkaa kama ngozi ya pili, macho yake ya samawati yakiwa makini, tulivu — na kisha, yakaniona. Hatukusema chochote. Hakupiga tabasamu. Hakunyoosha mkono. Aliniangalia tu kwa sekunde chache ambazo zilihisi kama milele… halafu akageuka na kuondoka.
Kabla sijajitafakari zaidi, mjakazi wetu alikuja kuniita. “Baba anakuita ofisini kwake.”
Nilisimama kwa tahadhari, miguu yangu ikiwa mizito. Nilitembea hadi kwenye chumba cha baba — kile chumba kilichokuwa na mapazia mazito ya samawati, maktaba ya vitabu vya kisheria, na harufu ya kiofisi. Niliingia kwa heshima, nikimkuta ameketi nyuma ya dawati lake kubwa. Pembeni yake, alisimama Nicholaus. Mwenyewe. Akiwa amejipanga, akinitazama kwa macho yale yale ya kanisani — lakini safari hii, alinitazama moja kwa moja.
“Monroe,” baba alianza kwa sauti yake ya kawaida, tulivu lakini yenye mamlaka. “Huyu hapa ni Nicholaus De Monte, shemeji yako mtarajiwa. Nicholaus, huyu ni binti yangu mkubwa, Monroe.”
Nilipojaribu kusema "Nimefurahi kukufahamu", nilikatizwa ghafla na Nicholaus, sauti yake ikipenya kwa uzito uliojaa utulivu wa hatari.
“Tumeshaonana.”
Nilitetemeka ndani kwa ndani. Maneno yake yalivyotamkwa, kwa sauti hiyo tulivu lakini ya kuumiza, yalionekana kama hukumu.
“Alikuwa kanisani leo. Tumeonana,” aliongeza huku akitazama upande mwingine, kana kwamba haikuwa jambo la maana. Lakini mimi nilihisi tofauti. Kulikuwa na kitu katika namna alivyosema, katika namna alivyonitazama, kilichonisumbua zaidi ya nilivyotaka kukiri.
Nilisimama pale nikihisi kama mtu anayemezwa na hewa. Macho yangu yalihamia kwa baba, ambaye alitabasamu kwa kuridhika kana kwamba kila kitu kiko sawa. Lakini ndani yangu, hakukuwa na utulivu — ilikuwa kama ardhi inayotikisika taratibu chini ya miguu yangu.
SURA YA PILI — MONROE
Week ilipita kwa haraka hku tunaendelea kufanya maandalizi ya harusi ya mdogo wangu
Jua lilikuwa linazama polepole nyuma ya milima ya Meru, likiacha anga ya Arusha ikiwa ya dhahabu na zambarau. Sauti ya mazungumzo, vicheko na ving'ora vya magari vilikuwa mbali nje ya jumba la kifahari la familia ya Abeli, lakini ndani ya nyumba, hewa ilikuwa nzito kama mvuke wa mvua ya masika.
Ilikuwa ni jioni ya Jumapili, na kikao kidogo cha kifamilia kilikuwa kimepangwa kwa ajili ya chakula cha jioni — hafla ya kukutanisha familia ya De Monte na familia yetu. Mama alikuwa ameihakikisha kila kitu kiko mahali pake: maua safi mezani, kioo safi kwenye kaunta, taa za dhahabu zikitoa mwanga wa joto. Na mimi, kwa namna isiyoepukika, nilihusika kusimamia kila kipande cha hiyo jioni.
Nilikuwa nimevaa gauni fupi la silk la rangi ya waridi iliyochanganywa na maziwa, nikifunga mikoba ya vitambaa mezani, mpaka mama yangu aliponigeukia akiwa anakagua mpangilio wa divai.
“Monroe, nenda kamwangalie dada yako. Muda unakwenda na mgeni yuko njiani. Haijajiandaa bado.”
Nilinyamaza kwa sekunde kadhaa kabla ya kujibu, “Sawa mama.” Sikutaka kuuliza maswali, ingawa moyoni nilijua Alice anapitia mengi zaidi ya kuchagua gauni.
Nilipanda ghorofa ya juu taratibu, kila hatua ikileta hofu isiyojulikana. Nilipofika mlangoni kwake, nilibisha taratibu. “Alice?” Hakuna aliyejibu. Nilifungua mlango taratibu na kuingia.
Alikuwa kitandani, amejikunja kama mtoto. Nywele zake nyeusi zilimwaga begani, machozi yakiwa yamebubujika mashavuni.
“Alice…” nilimuita kwa sauti ya polepole. Nilikwenda upande wake na kuketi pembezoni mwa kitanda.
“Huyu mchumba wangu…” alisema kwa sauti ya mwangwi. “Ameniambia hataki tena kuwa nami. Eti kwa sababu naolewa. Nimempoteza, Monroe.”
Nilimsogezea taulo dogo na kumfuta machozi, nikamshika mkono wake. “Ssshh… ni sawa, mdogo wangu. Tafadhali usilie…”
“Lakini nampenda! Monroe, Ethan ni kila kitu kwangu. Halafu baba... baba hata hajui. Akijua angefanya nini?”
Nilikuna nywele zake kwa upole, nikimwangalia kwa huruma. “Baba asingekubali kabisa. Ukijua baba alivyokasirika nilivyokataa ndoa yangu ya kwanza, si atamfukuza kazi Ethan bila hata kumwangalia mara mbili? Najua inakuumiza, lakini lazima usimame.”
Alice alinigeukia na kusema kwa sauti ya huzuni, “Lakini kwanini mimi? Kwanini sio wewe?”
Sikujibu. Kwa sababu hata mimi nilijiuliza swali hilo. Nilimsimamisha kwa upole. “Sasa simama, oga, vaa kile gauni la samawati unalopenda. Nitakuwepo kila hatua. Usimpe mama sababu ya kukuangalia vibaya tena leo.”
Alinitazama kwa macho mekundu na hatimaye akatikisa kichwa. “Sawa... nitajaribu.”
Nilitoka chumbani taratibu nikahisi pumzi nzito. Nilishuka ngazi kwa kasi ili kurudi chini, akili yangu ikiwa bado kwenye machozi ya Alice. Lakini nilipokuwa nikigeuka kwenye kona ya ngazi, ghafla nikajigonga.
“Kugh!” niligongana na kifua kigumu — kama ukuta. Mikono mikubwa ilinikamata kwa nguvu za kiustaarabu, kunizuia nisianguke.
“Samahani…” nilianza kusema, lakini sauti yangu ikakata ghafla.
Nilimtazama usoni. Nicholaus.
Alikuwa amesimama pale, sura yake ikiwa imetulia lakini macho yake yakiangaza utulivu wa ajabu. Alivaa shati nyeusi ya collar iliyofunguliwa juu, na suruali nyeusi iliyomkaa vizuri.
Alinitazama kwa jicho la swali, kama mtu anayetaka kujua kama niliingia katika ulimwengu wake kimakosa. Na kabla sijasema chochote, sauti yake ikakata ukimya:
“Utasimama hapo muda wote au utanipisha njia?”
Nilishtuka. “Oh. Pole,” nilijibu nikisogea pembeni haraka, nikijaribu kuficha aibu.
Lakini hakusogea. Alinitazama tena. Halafu nikajikuta nikiwa siko tayari kuondoka.
Mama alisema Nico ana tabia nzuri. Kwamba ni kijana wa heshima. Lakini hakuwa hivyo mbele yangu. Hakuwa na ukarimu wa kijana aliyefundwa, bali utulivu wa mtu anayeficha kitu.
“Hivi wewe ndo… shemeji anayesifika?” nilimwuliza bila kufikiria.
Alitabasamu. “Na wewe ndiye dada wa bibi harusi, ambaye haamini kila anachoambiwa na mama yake?”
Nilinyamaza. Alinigeukia kidogo, akichukua hatua moja mbele.
“Kama kweli unadhani dada yako anastahili mtu mzuri zaidi, basi tusaidiane kumfurahisha,” aliongeza kwa sauti iliyotulia lakini ya kukusudia. “Nahitaji vitu anavyopenda: rangi zake, saizi ya viatu, aina ya maua anayopenda, na gauni la ndoto yake. Niandae. Harusi itafanyika mapema zaidi ya mnavyodhani.”
Kisha, bila kungoja jibu langu, alinizunguka na kushuka ngazi kwa utulivu wa mtu mwenye mpango mkali kichwani.
Nikabaki nimesimama pale, nikijitafakari.
Yule hakuwa shemeji tu — alikuwa hatari tulivu.
Na kwa mara nyingine, moyo wangu ulihisi kwamba jioni hii haikuwa ya kawaida.
SURA YA TATU — NICO
Kelele za muziki wa chini zilitiririka kwa utaratibu ndani ya club yangu ya kifahari, Club Vesper, iliyoko pembezoni mwa barabara ya kuelekea Usa River. Ilikuwa ni mojawapo ya miradi yangu ya burudani — biashara ya pembeni ambayo wengi walijua kama "investment ya starehe," lakini mimi niliichukulia kwa umakini kama biashara yoyote ile. Niliwekeza kwenye muziki bora, huduma ya kipekee, na anga ya utulivu wenye hadhi.
Niliketi kwenye chumba cha juu kilicho na vioo vya kuangalia sakafu ya dansi. Mwanga wa buluu na zambarau ulikuwa ukicheza hewani, wakati waiter aliniwekea whisky yangu kwenye glass.
Pembeni yangu alikuwa Ricky, kijana wangu wa karibu, mshauri na pia meneja mkuu wa club. Alikuwa na sura ya kirafiki, lakini macho yake yalikuwa ya mfanyabiashara — anayefikiria takwimu, mikakati na faida kila wakati.
“Tumeongezeka asilimia 11 wiki hii,” alisema huku akifungua iPad yake na kunionyesha ripoti. “Haswa kwenye wageni wa VIP. Na reservation ya Jumatatu na Jumatano imejaa hadi wiki mbili zijazo.”
Nilinyoosha mkono na kugonga glasi yangu polepole. “Hiyo ni habari njema. Hakikisha DJ wa Jumatano ni yule mpya kutoka Cape Town. Nataka watu wahisi tofauti.”
Niliegemea kwenye kochi, nikiangalia chini ambako watu waliendelea kucheza, kunywa, na kusahau dunia kwa muda mfupi. Nilipenda kuona watu wakiwa huru wakufurahia Maisha
Lakini utulivu huo haukudumu sana.
Mlango wa chumba chetu ulifunguliwa kwa kishindo kidogo, na binamu zangu wawili, Jayden na Louis, wakaingia wakiwa na vicheko vya ajabu ajabu. Waliovaa vizuri, wakinukia harufu ya pesa, pombe na tamaa.
“Haya boss!” Jayden alinitupia salamu ya mkono. “Sema tumeharibu leo!”
“Siku zote,” Louis akaongeza, akijitupia kwenye kochi karibu nami.
Walichukua chupa walizokuta mezani bila hata kuniomba ruhusa, wakaanza kunywa na kubishana kuhusu mwanamke aliyepita mbele ya club. Mimi nilikaa kimya, nikiwasikiliza kwa jicho la pili.
Halafu, bila onyo, Jayden akageukia mimi.
“By the way bro... yule dada wa mchumba wako... what’s her name... ah, yes, Monroe... damn.”
Louis akaingilia. “Duh, yule mrembo ni kama malaika. Kwa nini hukuchagua yeye badala ya yule mdogo wake? Huyu Alice hata hatusisimui hivyo bana...”
Nikawatazama bila kusema neno. Walikuwa wakiongea kana kwamba walikuwa wakijadili magari au nyumba, si wanadamu.
Jayden aliendelea, “Sema kweli Nico. Kama ungetaka tu mwanamke wa familia ya Abeli, si ungemchukua yule Monroe? At least yeye ana class, sura, na... well, na umbo lake matata.”
Nilitabasamu kwa kubana, kisha nikanyanyuka na kwenda kusimama mbele ya dirisha. Niliangalia watu waliokuwa chini.
Monroe.
Kwa sekunde chache, nilimkumbuka alivyosimama pale ngazi za nyumbani kwao, akinitazama kwa jicho la mashaka na msimamo. Alivyogongana nami. Alivyosema maneno yake bila hofu, kana kwamba hakuwa na haja ya kunifurahisha. Mwanamke aliyejaa utu, sura na mvuto wa ajabu. Alinisumbua akili hata kabla sijaelewa kwa nini.
Lakini kisha nilijikumbusha kitu kingine.
Siwezi kuishi na mwanamke ambaye kila mwanaume anamkazia macho sitaki kujiingiza kwenye klabu moja na binabu zangu ya kumtumikia Monroe kana kwamba ndio malaika wanaomuongelea plus mwanamke kama Monroe atakuwa destruction tyu kwangu anatamanisha na kuvutia kweli lakini hafai kuwa mke sababu itanibidi nianze kugombana na ndugu zngu ilimradi tyu wasimuongelee nyuma yake.
Kazi yote ya nini hiyo
“Niko,” Louis aliniita. “Bado hujasema...”
Nikageuka, nikikunywa whisky yangu taratibu. “Hamuelewi kitu. Alice ni chaguo sahihi..”
Jayden alicheka. “Unasema hivyo kwa sababu umejizuia. But I bet she made your heart skip a beat…”
Sikumjibu. Nilimkumbuka Monroe akinisemesha siku hiyo ya chakula cha jioni, alivyovaa lile gauni la silk, mwanga wa taa ukimwangazia uso kama malaika wa dhoruba. Na kwa sekunde moja, nilihisi — hivyo kweli — moyo wangu uliruka kidogo.
Lakini sivyo maisha yangu yalivyopangwa. Mimi ni De Monte. Maamuzi yangu yana mantiki, si hisia.
Nilirudi kuketi. “Hivi vitu vyenu visinipotezee muda. Kesho tuna kikao na familia ya Abeli. Nataka kila kitu kiende kwa mpango.”
Ricky alitazama uso wangu. Alijua nilipotea kwa sekunde. Alijua sikumaanisha kila neno. Lakini hakusema kitu.
Na mimi?
Nilijua ukweli huu:
Monroe angeweza kuwa mwanamke wa kuniangusha kabisa.
SURA YA NNE — MONROE
Meza ya chakula cha mchana ilipambwa kwa ustadi na madoido ya hali ya juu. Sahani za ceramic zenye rangi ya ivory, vikombe vya divai vilivyong’aa chini ya mwanga wa chandeliers, na maua meupe yaliyowekwa katikati kama vazi la heshima. Familia ya De Monte walikuwa wamefika rasmi nyumbani kwa mzee Abeli kwa chakula cha mchana — ishara nyingine ya kuendeleza kile walichokiita ushirikiano wa kifamilia.
Nicholaus aliketi pembeni mwa baba yangu, akiwa kimya kama kawaida yake, lakini macho yake yalikuwa yakichunguza meza nzima kwa utulivu wa mtu mwenye lengo. Alikuwa na suti ya kijivu, isiyo na kasoro hata moja, na nywele zake zilizochanwa nyuma kwa mpangilio mkali zilifanya kila kitu amuonekane wa heshima, wa mbali… na wa kutisha.
Wakati wote wanafamilia wakiendelea kupiga soga, mimi nilikuwa kimya. Nilihisi kama nilikuwa sehemu ya onyesho la maigizo ambalo halikuwa langu. Kila tabasamu lilionekana kama sura bandia, kila kicheko kikiwa na maana iliyofichwa.
Nilijikuta nikigeuka kwa baba yangu. “Baba,” nilisema kwa sauti ya heshima, “kuna party ndogo kesho jioni kwa rafiki yangu. Pool party. Nilikuwa naomba ruhusa kwenda.”
Baba yangu alinyanyua uso wake kutoka kwenye sahani. “Rafiki? Huyo rafiki yako ni nani?”
“Anaitwa Max,” nilijibu kwa utulivu. “Ni mwanafunzi mwenzangu chuoni.”
Baba alikunja uso. “Max... huyo ni msichana?”
“Hapana. Ni mvulana.”
Kabla hata hajajibu, macho yangu yaliangukia kwa Nicholaus ambaye ghafla alikuwa amenikazia macho. Kama macho yake yangeweza kusema, yangesema: Don't you dare. Lakini baba aliongea kabla hajaleta neno.
“Sawa. Lakini hutakwenda peke yako. Binamu yako, Dennis, atakupeleka. Sitaki usafiri na mvulana yoyote asiye wa familia.”
Nilimeza mate polepole. “Sawa, baba.”
Nicholaus hakusema chochote, lakini niliweza kuhisi mtikisiko wa ukimya wake. Aligeuza macho haraka pembeni, kana kwamba hakuwa anataka kuniangalia hata kidogo.
Baada ya sherehe kuisha na wageni kuondoka, binamu yangu alinifikisha chuoni kama kawaida, huku nikimtazama kimya kimya barabarani. Moyo wangu haukuwa mahali pake — bado ulikuwa kwenye macho ya Nico, yale macho yaliyonikazia kana kwamba mimi ni kosa lililojitokeza mbele yake.
Chuoni, nilirudi katika maisha ya kawaida. Masomo ya maigizo, mazoezi ya sauti, na maandalizi ya onyesho la mwaka.
Nikiwa natembea kuelekea darasani, nilisikia sauti ya Max ikiniita.
“Heey! Umeshapewa ruhusa?”
Nikacheka kidogo. “Ndio. Baba ameruhusu… lakini nitakuja na binamu yangu.”
“Ah, si mbaya. Bora umekubaliwa,” alisema kwa tabasamu lake la kawaida. “Sitaki party yangu iwe bila Juliet wangu.”
Nikamwangalia kwa mshangao. “Juliet?”
“Yep,” alitoa karatasi mkononi. “Tulipata kipande cha kuigiza kwa wiki hii — Romeo na Juliet. Tupo pamoja.”
Moyo wangu uligonga kwa sekunde chache. Kipande hicho kinahusisha… kubusu? Nilijaribu kutojionyesha.
Darasa lilianza. Mwalimu wetu alitufanyia mgawanyo wa vipande na kuanza kupitisha vipande vya majaribio ya uigizaji. Ilikuwa ni kipindi cha masimulizi ya kina — kuingia kwenye hisia, kuishi ndani ya mhusika. Wakati wetu ulipofika, mimi na Max tulisimama mbele ya darasa, na kwa hisia ya Romeo na Juliet, tukakaribia… mpaka midomo yetu ikagusa.
Ilikuwa ni busu la maigizo, la sekunde moja tu. Lakini kwa akili yangu, lilihisi kama giza limeingia ghafla darasani.
Vipindi vilipoisha, Max alinitazama. “So… bado hujanijibu. Utaenda kweli?”
“Kama nilivyosema, nitarudi na binamu yangu. Nitakuwepo,” nilimwambia kwa sauti ya kujihami.
Alitabasamu na kusema, “Usinisahau Juliet.” Akageuka kuondoka… lakini kabla hajachukua hatua ya pili, nilihisi kitu nyuma yake.
Nikanyamaza. Nikatumbua macho.
Nicholaus.
Alikuwa amesimama mlangoni mwa darasa, akiwa amenikazia macho. Mikono mifupi mifukoni, uso wake wa baridi haukuonyesha hisia yoyote, lakini macho yake… yalikuwa yamejaa swali na shutuma.
Max aligeuka nyuma na kumuona. “Huyo ni nani?”
Nilijaribu kutabasamu. “Ndugu yangu.”
“Okay… basi nitaenda. Usisahau,” alisema kwa upole na kuondoka.
Nilikuwa bado natafakari namna ya kujieleza kabla ya kusikia sauti yake — ile sauti ya Nico, iliyochanganya kejeli na onyo.
“Baba yako anajua kama unabusu wanaume shuleni?”
Nilihisi tumbo langu limefungwa kwa barafu. Machozi yalinikaribia lakini nikajizuia.
“Niliigiza. Ni sehemu ya somo,” nilijibu nikigeuza uso pembeni.
“Unajua hiyo si hoja itakayomvutia mzee Abeli,” alisema kwa sauti ya taratibu lakini kali. “Na unajua atajua… siku moja.”
Niligeuka na kumtazama. “Binamu yangu Dennis yuko wapi? Mbona wewe ndio umekuja kunifuata?”
Alivuta pumzi ndefu. “Baba yako aliniambia nije. Dennis alikuwa na dharura. Deal na hilo.”
Aliponigeukia kwenda mbele yangu, alinisogelea kwa hatua moja zaidi na kusema kwa sauti ya chini:
“Na jiandae... muda si mrefu, nitakuwa shemeji yako. So get used to it.”
Kisha akaendelea mbele, akiniacha nikiwa nimesimama kama sanamu lililogandishwa na baridi la maneno.
SURA YA TANO — NICO
“Nenda kwenye gari.”
Sauti yangu ilikuwa kali, kavu, na ya mwisho. Hakukuwa na nafasi ya kupinga.
Monroe alinigeukia, akinitazama kwa macho yaliyojaa hasira iliyofichwa na kero isiyo na jina. Alibana midomo yake, lakini hakuongea. Alijua mimi ni mtu wa kutekeleza, si wa kubembeleza.
Alipofungua mlango wa gari na kuketi ndani, nilimfuata na kuanza kuendesha. Ukimya ulikuwa mzito ndani ya gari — mzito kama mvua ya mawe isiyoshuka bado.
Niliigeuza gari kwa kasi, nikipinda kona ya lango kuu la chuo, moyo wangu ukiwaka moto.
“Unajua,” nilianza kwa sauti ya utulivu wenye kisu ndani yake, “ninapaswa kumwambia baba yako. Kama huo ndio mfumo wa masomo yenu chuoni — kufundisha mabusu kama somo la lazima — basi ni vizuri azijue hizo mbinu za kielimu.”
Aligeuka kunitazama. “Unasema kama mtu asiye na akili timamu.”
“Na wewe unafanya kama mtu asiye na mipaka ya heshima,” nilijibu.
Monroe akavuta pumzi. “Kwanza kabisa, busu lile… halikuwa na maana yoyote. Halikuwa la mapenzi. Halikuwa la hisia. Ni plutonic.”
Nilimwangalia kwa jicho la kando, nikikaza taya zangu. “Plutonic. Hm. Busu la kielimu? Ulimi ulifuata pia au hiyo ilikuwa sehemu ya ‘scene’?”
“Max hakuwa na hisia zozote. Ni sehemu ya onyesho. Sanaa,” alijibu kwa mkazo, akigeuza uso wake kuelekea dirishani. “Huna haja ya kuingilia.”
Nilinyamaza kwa sekunde chache, nikiendesha gari kwa kasi ya wastani, lakini kichwa changu kilikuwa kama tanuru.
Kwanini huyu mtoto abusuwe? Na kwa nini iwe yeye — yeye ambaye baba yake alitaka aolewe miaka miwili iliyopita? Mwanamke ambaye kila sauti yake huamsha kitu ndani yangu — kitu ambacho siwezi na sitaki kukikubali?
Hilo busu, hata kama lilikuwa la maigizo, lilinifanya nitake kumvuta pembeni na kumwambia kwanini siwezi kukubali mtu mwingine amtazame namna hiyo.
Nilijikuta nikirudia kwa ukali, “Sawa. Ni plutonic — basi umwambie baba yako hivyo. Mweleze kabisa. ‘Baba, nilimbusu mwanaume shuleni. Lakini usihofu, ni ya kichuo tu!’”
Monroe aligeuka na kunikazia macho. “Hakuna kitu kinaendelea kati yangu na Max! Ukiacha kuigiza, sina hisia yoyote naye.”
Nilimsogelea kidogo upande wangu, macho yangu yakimtazama kwa ukali.
“Thibitisha hilo.”
Alikunja uso. “Nini?”
“Nimesema,” nilirudia kwa mkazo, “thibitisha. Kama busu la Max halikuwa la maana — kama kweli halikuwa la hisia yoyote — basi thibitisha kuwa busu la maigizo haliathiri kitu.”
Monroe alikaa kimya kwa muda. Halafu akageuka, akavuta pumzi ndefu. Alinyanyuka kutoka kwenye kiti chake taratibu, akawa anaelekea upande wangu wa gari.
Moyo wangu ulianza kugonga vibaya.
Aliweka mkono wake mwepesi begani mwangu. Nilihisi joto lake likipenya kwenye koti langu la ngozi.
Halafu — bila onyo — midomo yake ilikutana na yangu.
Ni busu la sekunde tano.
Sekunde tano zilizojaa kila kitu — utamu, ukakasi, maumivu, na msisimko.
Midomo yake ilikuwa laini, moto, na ya kualika dhambi.
Niliwasha kila kiungo cha mwili wangu kujaribu kujizuia nisimshike kiunoni na kumpa kile ambacho akili yangu ilikuwa inapinga.
Lakini moyo haukuwa na breki.
Sekunde tano. Lakini zilihisi kama masaa.
Kisha akaondoka taratibu, akaketi kwenye kiti chake bila haraka. Akaangalia mbele. Akavuta hewa taratibu na kusema kwa sauti tulivu,
“Umeona? Halina maana yoyote. Naweza kumbusu mtu yeyote — na haimaanishi chochote.”
Nilibaki kimya. Sikuwa na nguvu ya kujibu.
Kitu ndani yangu kilikuwa kimevurugika — uungwana wangu, mantiki yangu, na ahadi yangu kwa familia.
Maumbile yangu yalinichoma kwa msisimko wa hatari.
Nilihitaji hewa. Haraka.
Niligeuza gari kuelekea kituo cha mafuta kilichokuwa karibu. Niliweka gari pembeni, nikashuka kabla hata mafuta hayajaongezwa. Nilitembea hatua chache, nikavuta pumzi ya usiku uliokuwa baridi.
Nilihisi jasho linanitoka kifuani. Kama mtu aliyevuliwa silaha wakati wa vita.
Baada ya dakika tano, nilirudi kwenye gari. Nikaketi, nikaendesha gari kimya. Safari ya kurudi nyumbani ilikuwa ya ukimya mzito — lakini haikuwa ya amani.
Tulipofika mlangoni kwao, Monroe alikuwa tayari kufungua mlango wake kushuka. Nilimwangalia, sauti yangu ikitoka kwa taratibu:
“Hautamwambia baba yako… sindio?”
Alinitazama, akibana midomo. “Kwa nini? Unaogopa nini?”
“Kama akijua, hautaruhusiwa kwenda kwenye hiyo party yako ya ‘plutonic’,” nilimjibu kwa sauti ya chini.
Alivuta pumzi kwa hasira. “Ndiyo maana unasema napiga busu ovyo?”
Nilitabasamu kidogo, nikisema, “Ulipaswa kufikiria kabla ya kunionyesha jinsi unavyobusu ‘bila maana’.”
Monroe aligeuza uso wake, akifungua mlango wa gari. Lakini kabla hajashuka, niliongea:
“Sitamwambia. Lakini usirudie.”
Aligeuka, akinitazama kwa jicho la kike mwenye kiburi. Kisha akashuka, akifunga mlango kwa nguvu isiyo ya dharau, bali ya kukata mawasiliano.
Nilimtazama akitembea hadi mlangoni mwao.
SOMA MAELEKEZO
Bonyeza hi "Soma Kitabu" kisha itakupeleka kwenye fomu yaku login, hakikisha ume login na namba uliyojiunga nayo ndipo utaendelea sasa kusoma kitabu chote