MOYO WANGU HATI HATI

book cover og

Utangulizi

SIMULIZI: MOYO WANGU HATIHATI
MTUNZI: SUMAIYA MWENDO
SEHEMU YA: 01
Ni katika kijiji cha Irembo, Hewa ilikuwa safi sana na tulivu mno kama kawaida.
Ndege walikuwa wakiruka angani bila usumbufu wa aina yoyote ile. Ndege mmoja aina ya Kasuku alipaa juu na akatua kwenye kiota chake, katika nyumba ya Mzee Omary.
" Nut, mambo" aliongea binti mmoja mrembo sana aitwae Naima kumsalimia Nut huku akimpa mkono Nut ampandie wasalimiane vizuri.

"Safi, safi, Nakupenda " kasuku huyo alijibu huku akimdandia dandia Naima ambae alitabasamu na kumwambia Nut aache utundu wake.

" Dada Naa chai tayari, kila mtu amefika mezani kasoro wewe tu" alisema Nasreen mdogo wake Naima. Naima alitabasamu na kumuaga Nut, kisha haraka sana akaelekea mahali ambapo familia nzima ilikuwa imekaa wakitumia chai.

" Asalam alaykum" aliwasalimia na wote baba na mama yake waliitikia salaam yake.

Mama yake alimtazama kwa makini kisha akamwambia kwamba. " Naima ujue leo umetimiza miaka 26 umri wako unaenda sana, na bado huna hata mchumba, mwanangu kwani unapanga kuolewa ukiwa mzee?" Naima alimtazama mama yake na kujikuta anakosa raha hapo hapo.

" mama umeanza, unajua kabisa dada Naa hapendi hayo maswali" alijibu Nasreen

" hata hivyo mama yake yupo sahihi, mtoto wa kike anapovunja tu ungo haswaa kwa sisi waislam, inabidi atafutiwe mchumba na aolewe kwa sababu akikaa tu nyumbani inakuwa sio rahisi kuepuka vishawishi" alijibu Mzee Omary, Naima akawatazama na kusema moja kwa moja.

" yaani mtu akichokwa sababu huwa ni nyingi sana, hata hivyo msiwe na wasiwasi, baada ya ramadhan hii kupita nitaondoka zangu nikapange nyumbani kwangu, haina haja ya nyie kunitaka mimi niolewe na mtu tu eti kisa umri wangu unaenda kwa upande wangu mimi naona umri wangu hauna shida ila nyie ndo wenye shida na mimi" Naima aliinuka na kikombe chake cha chai pamoja na kipande kimoja cha chapati.

Nasreen aliwatazama wazazi wake kwa hasira kidogo.
" mna watoto wawili tu, Naima na Nasreen lakini kukaa na Naima wakati huu mpaka akiamua kuolewa yeye mwenyewe hamuwezi, oh Mungu tunusuru sie waja wako" aliinuka pia na kumfata dada yake ndani.

Nasreen alipofika chumbani alimkuta Naima akiwa ameshikilia picha moja ndogo ambayo ni wazi kwamba ilipigwa zamani sana, aliitazama huku akitabasamu kwa hamu ya kumuona huyo aliekuwa kwenye picha.

" ni wewe tena dada na huyo mchumba wako asiekuwepo? Huyo ni Invisible acha kabisa kumfikiria " alisema Nasreen Naima akamkumbatia mdogo wake ki utani utani na kumwambia.

" tatizo ni kwamba bado naamini Salum atarudi kwa ajili yangu, nashindwa kuacha kumpenda" Nasreen alitikisa kichwa na kuona kama dada yake atapoteza akili huyu.

" nakuonea huruma sana dada, yaani kwa upande wangu mimi namuomba sana Mungu anijalie mume anae eleweka na sio mpenzi wa miaka nane iliyopita dada yangu unapoteza muda" alisema Nasreen na kumalizia chai yake.

Naima alitabasamu na kutazama picha tena kisha akasema, "namuamini sana Salum."


Nasreen alitabasamu na kumwambia.

" Ujue dada mimi naelewa mawazo yako, yote huyo ni Salum ndo unamuwaza, kila baba akija na wazo la wewe kuolewa lazima upinge kwa sababu unampenda sana Salum lakini una uhakika huyo Salum aliwahi kukupenda? Miaka 8 sasa tangu aondoke hajawahi kurejea wala kutuma ujumbe wowote ule kwako? Unauhakika gani yupo hai?"

Nasreen aliongea na ghafla mdomo wake ukawa mzito maana alihisi kachafua hali ya hewa tayari.

Naima alimgeukia na kumtazama kwa jicho kali mno Nasreen akahisi uwoga na kuomba samahani hapo hapo.

Naima aliinuka na kutoka nje kabisa ya chumba, alipofika sebuleni aliitwa na na mama yake ambae alimuona anatembea kama vile anapepea.

" Unaenda wapi we binti? Baadae Mzee Onana na familia yake watakuja kutembea hapa nyumbani, na ujio huu ni maalum kwa ajili yako."

Naima alimsikia mama yake lakini hakutaka kumzingatia aliendelea na safari yake.

Nasreen au Nana alijionea huruma.

"Jamani mimi ni mjinga sana, nimefanya nini sasa huu mdomo jamani? Alisogelea kioo na kujizaba mashavu yake.

" Mimi ni mjinga, mjinga sana tatizo ni mdomo huu kamdomo kataniponza mimi, Mungu wangu Ramadhan inakaribia ufanye mdomo wangu uwe na stara tafadhali "

Alijisemea na kuushika moyo wake, bado aliona hana cha kufanya kuirejesha mood ya dada yake, alijitupia kitandani.

☆☆☆☆☆

Naima alitembea haraka haraka, njia za vijijini hazina mambo mengi hata hivyo, ghafla akakumbana na mtoto aliekuwa anaenda nyumbani kwao.

"Dada Naa, hii ni yako" mtoto huyo alikuwa anahema sana kana kwamba asingeweza kupumua. Lakini baada ya kumkabidhi Naima bahasha alikimbia na kuondoka zake.

Alifungua bahasha hiyo hata kabla hajamuuliza Huyo mtoto hiyo bahasha alipewa na nani, mtoto alikuwa amekimbia tayari.

" isiwe tabu, nitaisoma tu, na nikiisoma ntajua imetoka wapi?" Alipoisoma aliona kabisa ilikuwa maalum kwa ajili yake, alifungua kwa makini na kukutana na Anwani mbili, Anwani moja ilitoka Oman Mascot na jina lilisomeka Salum, huku nyingine Naima, Tanga Tanzania.

Naima alihisi moyo wake ukiripuka, jamani jina Salum lilikuwa jina ambalo alikuwa akiliota siku zote.
Kabla hajaisoma hiyo barua alikaa chini na kuanza kulia kwanza, moyo wake ukienda mbio kwa furaha. Akaanza kuifokea barua akisema.

" Salum wewe ni mshenzi, mwanaume mjinga sana wewe, mwenzio nimekumiss sana, ulikuwa wapi miaka yote hii Salum Nakupenda" alijisemea na kujiandaa kuisoma baada ya kuvuta pumzi nyingi sana.

Lakini kabla hajasoma Barua yake ilinyakuliwa na kijana mmoja ambae alisimama mbele yake ghafla.

Naima alikasirika mno, maana kijana huyo alikuwa mgeni kwenye macho yake. Alionekana mzuri mno na mtanashati, lakini hakumfahamu kabisa.

" Tafadhali sana kaka, sikujui wala hunijui , nipe barua yangu kwa amani tu. Ni muda mrefu sana nimeusubiri ujumbe wa huyu mtu aliepo kwenye hiyo barua, samahani sana nipatie" Naima aliongea kwa hisia mno kiasi kwamba kijana huyo aliekuwa akiisoma ile barua alimuonea huruma.

" mh! Naitwa Ibrahim Onana, bila shaka wewe ni Naima Omary " Naima alishtuka Ibrahim Onana huenda huyu ndo kijana ambae, leo familia yake itaenda kwak kwa ajili yake.

" vyovyote mi sijali, naomba barua yangu" aliongea Naima. Lakini Ibrahim hakumrudishia ile barua aliichana chana hiyo barua mbele ya Naima na kumwambia

" Sahau kabisa kuhusu huyu mtu, aliekutumia hii barua, kwa sasa ukurasa wa kitabu cha maisha yako unaenda kubadilika" Naima kwanza alibaki ameganda mdomo wake ukiwa wazi, yaani! Anha! Huyu kaka ni mwehu ama? Alijiuliza na hakupata jibu lakini tayari barua ilichanwa.

Naima alishindwa kustahimili, maumivu ambayo aliyahisi kwenye moyo wake na mwisho alizimia.

SEHEMU YA: 02

Endelea.......
Ibrahim alimtazama Naima aliekuwa kazimia hapo chini, akatabasamu tu na kujiuliza kama Naima alimpenda huyo Salum namna hiyo kweli?

Alishusha begi lake mgongoni na kutoa chupa ndogo ha maji ambayo aliyaanda kunywa, kwa ajili ya dharura zake mwenyewe akamwagia naima.

Haikuchukua muda sana Naima alizinduka alipokuwa amelala kwa tabu sana, akakutana na uso wa Ibrahim. Ibrah alikuwa kijana mwenye sura nzuri sana kwanzia alipomuona wakati huo, lakini kwa nini sasa ana roho mbaya hivyo? Jambo hilo lilomuumiza sana Naima.

Alijikuta tu anakosa raha wakati akimwangalia, alijitahidi akainuka alipokuwa amezimia hapo chini ya mti, macho yake yakatua kwenye karatasi za barua iliyochanwa chanwa na Ibrahim jamani nyie huyu kaka.

" kwa nini sasa umechana, imenichukua miaka nane kusubiri hii barua kutoka kwa huyu mtu, kwa nini umechana jamani?" Naima alianza kulia huku akikusanya vipande vidogo dogo vilivyokuwepo hapo chini kisha akaviweka kwenye bahasha.

" nadhani taarifa zimefika nyumbani kwenu tayari" Ibrahim alimwambia huku akimshika mkono wake na kumuinua kutoka chini alipokuwa akiokota vipande vya barua.

" ni wazi kwamba, utakuwa mke wangu hivi karibuni kwa hiyo jiandae, ki hisia, ki akili na kimwili, kwa sababu sitaki mama wa watoto wangu awe na historia na mwanaume yeyote tofauti na mimi hapa." Ibrahim aliongea Naima akaunyakua mkono wake kutoka kwake.

" una kichaa nahisi, unadhani nitaolewa na wewe? Ndoa ni hiari sio lazima na hakuna wa kunilazimisha, imekula kwako sitaolewa na wewe hata nirogwe" Naima aligeuka na bahasha yake akaanza kurudi nyumbani kwao, hakutaka kumjali Ibrahim hata kidogo. Kwanza mwanaume mwenyewe kamuona wakati huo tu, kwanz kwa nini ajihakikishie atamuoa wakati yeye hajataka, kwani huyu mwanaume ni kichaa.

Ibrahim alimtazama huko nyuma alivyokuwa akitembea kwa haraka, ni kama vile alifukuzwa. Ibrahim alitabasamu na kujisemea tu.

" wewe ni mwanamke, na sio mwanamke tu. Ni mwanamke mzuri na mrembo sana, unastahili kuthaminiwa sana, ndo maana nataka kukuoa, naamini ukiwa mke wangu, utakaa katika nafasi unayostahili wewe kama mwanamke wa thamani sana" alimazila kuongea mwenyewe Ibrahim kisha akageuka kuendelea na safari yake.

Naima alipofika nyumbani alipita moja kwa moja sebuleni na kuwakuta wageni kadhaa nyumbani kwao. Aliwafahamu lakini hakuwasalimia kabisa.

Alipofika jikoni, alichukua kikombe na kuchota maji mtungini alimuona Nana kabla hajaanza kunywa maji, Lakini hakumsemesha.

Nasreen alidhani labda ni kwa sababu ya maneno aliyomwambia hapo asubuhi.

" Kadaa nisamehe mwenzio, sikudhamiria kusema vile natamani unisamehe na unisemeshe mwenzio" Alimkumbatia kwa nyuma lakini Naima aliusukuma mkono wake mbali.

" Nana kwa sasa niache, nahitaji kuwa mwenyewe tafadhali " Naima aliondoka jikoni na kuelekea chumbani kwao. Nana alikosa furaha kabisa na kukipiga kichwa chake.

" yote haya ni ujinga wako, hujui kuuziba mdomo wako why?"

" Nana dada yako yuko wapi?" Aliuliza Bi Sada ambae ni mama yao.

" yaani mama hata sijui niseme nini? Nilimwambia maneno mabaya asubuhi leo kwa hiyo bado ana hasira na mimi. Nahisi na mlivyomwambia asubuhi, sidhani kama atakubali kuolewa huyu"

" hata usijali mwanangu, mara hii atake asitake ataolewa tu. Sitakubali ujinga uendelee, ujue dada yako ana miaka 26 sasa, tusifanye mchezo asipo olewa yeye itakuwa ngumu kwako wewe pia kuolewa na siwezi kuruhusu hilo"

" mama usiseme hivyo. Kwa sababu dada hawezi kuwa sababu ya mimi kuto olewa, mimi najua kila mtu ana rizq yake"

" sawa Kadogoo, nenda kamsindikize Anati, kwa Baba lea muendee nguo ya Naima, leo shangazi zako wameamua kusimamia hili."

" sawa mama" Nasreen alitika nje na kumfata Anati, huyu alikuwa binamu yao mtoto wa shangazi yao mkubwa.

Chumbani Naima alikuwa amejifungia kwa nguvu analia sana, kila alipowaza Ibrahim alivyochana barua yake alihisi kuchanganyikiwa.

" hapana siwezi kumsamehe huyo kaka, labda kwenye mwili wangu uliokufa " alipiga kelele kila alipojaribu kugundisha vile vipande vya karatasi na vika kataa kuleta maana ya maandishi.

☆☆☆☆

Upande wa Pili Ibrahim alifika nyumbani kwa Babu yake Mzee Onana alipokelewa na binti wa miaka 20 aitwae Mariam.

" jamani kaka Ibrahim, ni siku nyingi sana, babu na Bibi kaka Ibrahim amefika" aliongea Mariam kwa sauti Ibrahim akatabasamu na kumpatia begi alilokuwa nalo mgongoni.

" jamani mjukuu wangu, kidogo uchelewe na taarifa tulitoa kwa kuchelewa kwao binti sijui ingekuwaje?" Alisema Mzee Onana ambae alikuwa kajiandaa kwa safari tayari.

" Babu mtu hata hajakaa wewe tayari unawaza safari, ndo nini sasa?" Mariam iongea Ibrahim akacheka sana .

" Mzee Onana naona unazidi kuzeeka sasa, hujui kama sasa hivi na saa tano na kwa Omary utaenda saa Nane mchana baada ya dhuhur" aliongea Bi Onana. Ibrah na Mariam walicheka sana.

" Babu naona sasa kijiji kinakukataa ntakupeleka mjini wewe, inatosha kulima na kunywa kahawa za asili" Ibrah alimtania babu yake ambae alicheka na kusababisha meno yake kuonekana.

" wazazi wako wanasemaje huko mwanangu, mama yako hajambo?"

" ndio babu, binti yako hajambo kabisa amewamiss sana, na anatarajia kuja huku baada ya Ramadhani " alisema Ibrahim na wakati huo Mariam alimtengea vitanio vitamu ambavyo aliviandaa mwenyewe kwa msaada wa bibi yake.

" aah shukrani sana, Bi Mariam wewe ndo hutaki kuja Dar es salaam kazi kudeka tu hapa kwa wajina wako"

" mimi ni mkoba wa bibi kaka, kwa hiyo nipe uvumilivu "

Baada ya mapokezi na mapumziko ya muda mfupi, Ibrahim alipata muda wa kuongea na bibi pamoja na babu yake.

Alipokuwa Dar es salaam mama yake alimuhimiza sana suhala la kuoa akiwa bado kijana, na mara nyingi alimwambia ni vizuri kuoa ili asirudi nyuma katika maendeleo yake, na kwa kuwa yeye amekuzwa na kulelewa na mzazi mmoja tu ambae ni mama, kamuona mama yake akipambana, na kuhangaika kwa ajili yao yeye na Mariam, Basi hakutaka kumpinga, hata hivyo katika misingi ya dini ndoa ni sitara, na kwa mafanikio aliyokuwa nayo wakati huo. Aliona ni vyema sana akaoa kwa sababu alikuwa na uwezo mkubwa sana wa kuitunza na kuihudumia familia yake.

Kwa hiyo alipomwambia mama yake kwamba yupo tayari kuoa, mama yake alimuuliza kama anamchumba tayari au amsaidie kutafuta, Ibrah aliomba mama yake amtafutie kwa sababu aliamini wazi kwamba mama yake siku zote ni mzuri mno kwenye kuchagua watu sahihi.

Na mama yake alimkumbuka Naima moja kwa moja, akamuulizia kwa wazazi wake ambao ndo hao Mzee Onana na Mke wake, walimwambia kuwa Naima bado yupo nyumbani na amekuwa akikataa posa za watu, ila walimuahidi watajaribu, na sasa wameongea na wazazi wa Naima tayari bado Naima mwenyewe.

Ili kuongea na Naima ilibidi Ibra aje yeye mwenyewe, alipo muona tu Naima kwenye picha kadhaa alijikuta amempenda sana yaani. na sasa ndo wapo kwenye harakati za kwenda kwao Naima.

" Natumai uliamua hili kwa kufikiria zaidi, japo binti hukuwahi kumuona lakini Natumaini zaidi kwamba utampenda tu ukimuona" alisema Bi Onana. Ibrah akatabasamu, kwa sababu alionana nae, na hawakuonana tu. Bali walizinguana pia.

" sina shaka na mwonekano wake bibi, ninachotaka mimi ni mke tu" alijibu Ibrah, bibi na babu yake walifurahi sana kusikia hilo.

Na maandalizi yalikuwa tayari na washenga wao kadhaa walikuja, baada ya adhuhuri, walianza safari ya kwenda nyumbani kwa kina Naima.

Wakati huo upande wa pili Naima alikuwa ameandaliwa tayari na amepodolewa kabisa kwa ajili ya kumpokea mgeni wake. Lakini uso wake haukuwa na furaha hata kidogo, Nana alielewa hilo lakini angefanya nini sasa? Hata hivyo alitamani sana dada yake aolewe. Hakumuamini huyo Salum hata kidogo na watu walimsema sana dada yake.

" Wageni wamefika" ilikuwa sauti ya Anati ambae alichungulia dirishani na kuona msafara wa gari mbili ndogo zikiwa zimeongozana. Nasreen alimtazama Naima moja kwa moja Naima alikuwa kakunja uso wake tu. " dada tafadhali usiwe hivyo leo, nakuomba" aliongea Nana, Naima alimtazama kwa makini bila kuongea kitu.

ITAENDELEA..........


SEHEMU YA: 03
Endelea.......
Baada ya wageni kuwasili walikaribishwa kwa heshima na taadhwima, wakapata mazungumzo mazuri sana na wazazi wa Naima.

Na baada ya muda Naima aliitwa akawaandalie wageni chochote kitu kwa mujibu wa utaratibu ili aweze kuonekana kwa mwenzi wake mtarajiwa.

Nasreen alimuinua Naima taratibu wakaelekea jikoni, walipofika jikoni Nasreen aliandaa kila kitu na kuweka kwenye sinia moja kubwa kisha akamkabidhi Naima.

" Dada usiwe hivyo, najua sio rahisi lakini kwa sasa jaribu kumpa nafasi huyo kaka japo sijamuona, lakini naimani ukimpa nafasi akakutendea vyema kama mwanamke wake utampenda tu" aliongea Nasreen, Naima akaweka kila kitu chini kisha akamkumbatia na kumwambia.

" Nana mdogo wangu we hujui kitu, hujui kwa nini nipo hivi, huyu kaka leo mimi nimekutana nae nilipo ondoka asubuhi nikiwa na hasira, kitu alichofanya kwangu ni maumivu matupu, leo nilipokea barua kutoka kwa Salum, ile naifungua tu huyu kaka katokea kaichana"

Nasreen alihisi moyo ukimpasuka, ni takribani miaka nane sasa dada yake alikuwa akisubiri hata ujumbe mdogo tu kutoka kwa Salum, alafu huyu shemeji mpya? Nasreen alijisikia vibaya sana na kumuonea huruma dada yake hapo hapo.

" sasa dada wewe unahisi tufanye nini? Najua unajisikia vibaya sana lakini huenda kuna kitu Mungu kakuepusha nacho."

" Nana acha basi kuongea kama mtu asie jua kitu na wewe, huyu Ibrahim mimi siwezi kumpenda kamwee! Hata awe vipi? Mwanaume gani asiejali hisia za mtu? Mimi bado sijawa chochote kwake alipaswa kulinda mipaka yake" Naima alifoka utafikiri Nana ndo alisababisha

" lakini dada ni yeye sio mimi"

" sijali, ni kwa sababu haunielewi pia, kwa nini mnanifanyia hivi lakini?"

" kukufanyia nini tena mwali wetu" aliingia Shangazi yao aitwae Tuma alichukua sinia na kumpatia Naima.

" mwali wangu, naomba tuelekee sebuleni tafadhali wageni wanakusubiri wewe tu" alisema Aunt Tuma na Naima akatangulia huku Nana pamoja na Aunt Tuma wakiwa nyuma yake.

Mdogo mdogo hadi Sebuleni, Nana alipomuona Ibrahim moyo wake ulishtula mno. Ni kwa sababu alikuwa anamfahamu vyema sana.

' huyu Si Ibrahim Onana, mfanyabiasha maarufu Wa maduka ya urembo na vipodozi huko jijini Dar es salaam? Licha ya utajiri wake ana sifika kwa nidhamu na ustaarabu wake wala hana skendo, na amekuwa mwanamitindo maalum wa mavazi ya kiume pamoja na vipodozi mbalimbali , yaani hamna kitu kinauma kama crush wako ageuke kuwa shemeji yako' Nana aliwaza macho yake yakiwa kwa Ibrahim, alitabasamu kwa lazima huku moyo wake ukidunda dunda kwa nguvu.

" Naima alipofika sebuleni akakutanisha macho yake na macho ya Ibrahim alijikuta ameganda bila hata kusogea.

" Naima" mama yake alimuita ili kumshtua Naima akasogea na kuanza kugawa vikombe vya kahawa kwa wageni, alipofika kwa Ibrah alisimama na kumtazama kwa macho ya chini. Ibrah aligandisha macho yake kwa Naima huku akitabasamu kwa namna ambavyo alikuwa kamkubali sana.

Alimshika mkono wake kidogo wakati anapokea kikombe. Naima aliutoa haraka Ibrah akatabasamu.

Kitendo hicho kila mtu alikiona hadi Nana, na watu wote walitabasamu na kukonyezana. Naima alisimama pembeni ya Nana akiwa na aibu maana kila mtu aliwaona na Ibrah hakuamisha macho yake kwake. Nana akamkonyeza Naima akakosa amani kabisaa.

Naima alikuwa na wasiwasi akatamani akimbie aondoke eneo hilo kwa aibu, lakini hakuwa na mbio.

" wewe ni sawa na Almasi inayotazamwa na wengi huoni shem hachomoi dada wewe" Nana alimkonyeza na kumpiga bega kidogo. Naima alitamani kuaga Nana akamcheka.

" ila dada acha hizo bhana, huoni kama shemeji ni mzuri sana wewe hahaha, em tulia bhana utuletee mbegu yake kwenye familia." Naima alihisi hasira na kumkanyaga Nana mguu wake kwa nguvu.

" Subhanallah!" Nana alipiga kelele kila mtu akamgeukia. Nana kuepusha shari akaanza kuimba.

" walhadulillah, laillaha ilallah, Allah Akbar " alijikaza huku akiimba kila mtu akacheka.

" hivi Nasreen huwa zinakutosha wewe?" Aunt Tuma alimsema Nasreen akacheka.

" aunt Tuma kwani we huoni kama jambo kubwa limetokea hapa, nimejikuta tu nahisi furaha isiyo kifani." alijibu Nana huku Naima akimcheka kwa chinichini.

Ibrah pekee ndo aliona kama Naima alimkanyaga Nasreen kwa nguvu. Alishindwa kuficha kicheko chake, na akagundua kama hawa dada wawili ni very dramatic.

Nana alipo ona anachekwa na shemeji alishindwa kuvumilia aliondoka hapo mbio mbio kuelekea jikoni.

" Da Naima ndo nini sasa kuni embarrass mbele ya familia ya wakwe, hakika sijapenda uwii mimi jamani." Akakumbuka namna Ibrah alivyomcheka.

" woi woii woii, nijifiche wapi sasa? Aah! Kwanza najificha nini? Yule si shemeji tu bhana ala? Kwanza akitokea mbele yangu akanicheka najifanya Eliud wa cheka Two haha. Mwah Sukari hapa. Alafu navunga sicheki wala simkohoi." Alichukua sambusa nne na kukaa chini ya kabati ya jiko na kuanza kula mdogo mdogo. Akisubiri tukio linaloendelea sebureni liishe zake.

ITAENDELEA........


SEHEMU YA: 04

Endelea.......

Ibrah na Naima walipewa nafasi ya wawili kuzungumza, walipofika kwenye benchi la nje Naima alikaa kimya bila kuongea kitu chochote, Ibrah alitabasamu na kumsogelea. Bahati mbaya mkono wake ukaugusa mkono wa Naima aliutoa mkono wake haraka kama mtu aliepigwa shoti.

" samahani mara hii ni bahati mbaya" alijitetea Ibrah.

" sijali kikubwa unatambua sitamani hata uniguse" alisema Naima akaendelea kuangalia mbali, bila kumtazama Ibrah usoni.

" aah! Najua haunipendi, au niseme umenichukia lakini sawa haina shida naweza nikasitisha kila kitu ambacho nimepanga kwako, ili uwe na furaha, lakini nikuombe tu, usimsubiri huyo Salum, hawezi kuwa wa kwako" alisema Ibrah Naima akamgeukia na kumtazama kwa makini.

" sio mwanaume sahihi kwako, hakuna mwanaume ambae anaweza kumsubirisha mwanamke kwa miaka nane, na aishi bila mwanamke mwingine huo ni uongo, tafakari" aliongea Ibrah Naima akamkazia macho kisha akacheka.

" unaongea utadhani labda unamfahamu sana Salum wewe, yule ni mwanaume wa kwanza kwenye maisha yangu, nilianza mahusiano na yeye tu. Na aijawahi kutokea kumpenda mtu mwingine zaidi yake, kwa hiyo usijaribu kunishawishi nikupende kwa kumchafua yeye"

" binti samahani, kumbuka mimi ni mwanaume, tena rijali. Siwezi kufanya mambo ya kike mimi eti nimchafue ili unipende? Hilo haliwezekani kuhusu kukuoa naweza nikakuoa nikitaka hata kama hautaki, lakini kukufanya unipende hiyo ni juu yako, ndo maana nimesema naweza kuhairisha hili suhala pia nikatafuta mwanamke mwingine kwa sababu nimekuja huku kuoa. Ila ki ukweli nimekupenda sana wewe ndo maana sitaki uharibikiwe kwa mtu asie sahihi." Alimaliza kuongea Ibrah akainuka ili aondoke.

" Usijali " aliendelea kabla ya kuondoka. " nitasitisha mipango yote ya ndoa ili ubaki na amani ya moyo wako, sitavumilia kuona unalia ukiwa na mimi kwa sababu haunipendi, na siwezi kuwa mbinafsi kwa sababu nakupenda sana, lazima niijali furaha yako"

Alimaliza kuongea akaanza kuondoka, Naima aliinuka mbio na kwenda kuushika mkono wa Ibrah kwa mikono yake miwili.

" Tafadhali " aliongea kwa sauti ya upole sana. Ibrah aligeuka kumtazama huku akiyatazama macho yake mazuri na malegevu. Hakika Naima alikuwa binti mrembo mno kiasi kwamba kila mwanaume ambae angemuona kwa mara ya kwanza basi angetamani kumfanya wa kwake.

" naomba usi sitishe kitu chochote " Ibrah alishangaa na kumtazama kwa macho ya kina.

" upo sahihi, mimi sikupendi, lakini upendo wa mwanamke una tengenezwa, siwezi jua huko alipo Salum anaishi vipi japo barua ulio ichana ingenipa mwanga, lakini familia yangu inafuraha kwa sababu unataka kunioa" aliongea kwa upole huku akimtazama usoni Ibrah.

" kwa hiyo?" Ibrah alihoji

" kwa hiyo naomba, unioe tu na unitengenezee mazingira sahihi ya kukupenda, natumai nitamsahau Salum na nitakuona wewe kama mume wangu"

" kwa hiyo unataka niishi chini ya kivuli chake, nimekupenda ndio Naima, lakini sitavumilia kuona naoa mwanamke ambae atanifanya mimi kama chaguo la pili baada ya mpenzi wake wa kwanza, hiyo ni wazi kwamba siku ex wako akija utamchagua yeye na uniache mimi"

" hawezi kuja" alijibu Naima

" una uhakika na hilo?"

" sijui kwa sababu barua uliyoichana kuna kipande kimoja niliona neno hilo. Siwezi kuja kwako"
Ibrah alitabasamu kwa uchungu na kumuuliza.

" upo tayari kuniamini ili nikusimulie barua nzima ilisema nini?

" hapana, haina haja, najua ananipenda sana, bila shaka aliomba msamaha kwa kutokuja na hawezi kuja" Ibrah alisikitika mno na mwisho alikubali.

" sawa, kama unahisi hivyo. Ila afya yako ya akili inahitajika sana ili uwe salama, ondoka kwenye mahusiano toxic" Alimaliza kuongea Ibrah na kutaka kuondoka.

" Tafadhali, usiwaambie chochote familia yangu. Nitaolewa na wewe tu" alisema Naima Ibrah akamkubalia na wakaelekea wote sebuleni wakiwa na nyuso za tabasamu.

" Nasreen ona" Anati alimuonyesha Nana kwa mbali amuone dada yake alivyojaa tabasamu.

" wow! dada yupo in love, ni matumaini yangu kwamba nitapata skin care nyingi sana" alijisemea Nasreen na kuanza kuwaza, nguo atakazo vaa siku ya harusi, hata hivyo shemeji yake mwanamitindo, kwa nini asimfanyie mpango.

" nyie mimi watajuta watu fulani, alafu nitamshawishi dada aninunulie simu mpya, hii kwa sasa imejaa, ni mwendo wa picha tu niwatambie huko status, kila nguo nitakayoivaa ntaipost, wakiniuliza Nana hiyo nguo jamani, jibu ni moja tu nauza. Nawapangia bei alafu wakinituma napata cha juu. Jamani nakuwa dalali wa online." alijisemea Nana huku akiwaza mambo yakatavyokuwa mazuri kwake.

Akiwa anazunguka kwa furaha ghafla akafungua macho yake na kubaki ameganda. Alikuwa Naima kasimama mbele yake akimtazama kwa makini.

Nana alitulia na kuweka nywele zake sawa.
" aah! Nilikuwa nakuja kukupa kampani dada, twende kwa shemeji sasa" alisema Nana. Naima akamrejesha.

" hauna akili, wakina Ibrah tayari wameondoka zao, tumebaki familia"

" wewe kweli?" Alijisemea

" Nana mdogo wangu, acha wenge basi. Usipende kujenga kasri kwenye hewa, sasa wakati wana agwa we huku jikoni ulikuwa umebaki una waza nini?" Nana alikosa aseme nini?

" kusema ukweli natamani harusi yako iwe ya kipekee dada, ndo maana nimewazq sana ntavaa nini? Kuhusu wewe sina mashaka kwa sababu shemeji ni mwanamitindo na anajua kumpangilia mtu kwa mavazi yake na kila kitu, najua ataku design unavyostahili kuwa" alipo ongea hivyo Naima akashtuka.

" umesema ni mwanamitindo? Kwani wewe Nana unamfahamu Ibrah?"

" dada wewe wa wapi? Shemeji ni mtu mkub....." kabla hajamaliza kuongea mama yao aliingia jikoni na kuwakatisha.

" Naima ndoa yako ni wiki, kutokana na makubaliano yao, inabidi uwekwe ndani kwa siku hizi chache zilizobaki" Naima alishtuka.

" sasa mama mbona ghafla sana, ndoa ina process nyingi sana hadi kufikia" Naima aliongea. Nana akashtuka

" mama hatujafanya maandalizi yoyote yale tayari washapanga ndoa? Mbona ghafla na sijajua hata nashona kitambaa gani?" Alisema Nasreen. Moyo wake ulivunjika ni kama walimtoa nje ya reli kabisa.

" Nana wewe wasiwasi wako nini? Aunt yako nipo hapa, kikubwa wewe fanya kunitafutia cherehani ambayo unajua itanisaidia mimi, kisha baada ya hapo, wewe na Anati pangeni vitambaa ambavyo vitawatosha nyie. Hakutakuwa na watu wengi sana cha muhimu hapa ni ndoa, kijana anamtaka mke wake, kesho kutwa mahari inaletwa. Haya Naima Tuondoke " Aunt Tuma ambae aliingia na kudakia maongezi hakusubiri jibu alimchukua Naima na kuondoka nae.

" Aunt sasa unampeleka wapi? Dada Naima vipi kuhusu wewe sasa? Mbona sielewi" alisema Nasreen mama yake akamtazama kisha akatabasamu na kumvuta karibu.

" sikiliza binti yangu mrembo, kitu pekee ambacho wewe huelewi ni kwamba, dada yako ni bi harusi mtarajiwa kwa hiyo hatakiwi kuonekana onekana hovyo, na kwanzia leo atakaa chumbani kwa shangazi yenu mpaka ndoa ipite aondoke na mume wake. Nana alihisi kizunguzungu.

" kumbe kuolewa ni mtihani namna hii sikutarajia kabisa" alijisemea mama yake akatabasamu na kumshika shavu.

" baada ya Naima ni wewe Nasreen, kwa sasa kuwa mvumilivu tu utaelewa kila kitu" Mama yake alimvuta mkono wakaongozana kuelekea sebureni. Huko aliwakuta ndugu zake wapo bize. Ghafla akakumbuka ilikuwa siku maalum kwa ajili ya ndoa ya Ruaida, na Ruaida ni rafiki wa karibu sana na Naima.

" sa itakuwaje?" Alijiuliza lakini hapo hapo meseji iliingia kwenye simu yake.

[ ni harusi ya Ruaida, siwezi kwenda kwa sababu tayari nimewekwa ndani, naomba ufanye unachofanya uwatoroke hapo nyumbani uende kwa niaba yangu, Ruaida akikuuliza kuhusu mimi, usimjibu chochote kama nimechumbiwa mwambie tu kwamba, ni ghafla nimeingia kwenye siku zangu, uzuri anaielewa hali yangu nikiwa kwenye siku zangu.] Ujumbe ulitoka kwa dada yake Naima. Nana aliona haya sasa mawazo.

" huu sasa mtihani, usiku ndo kama huo unaingia nawatoroka vipi hawa wazee mimi." Alijiwazia Nana. Lakini alipo muonq Anati akiwa bize kufatilia nguo na vitambaa mtandaoni, alimfuata mama yake na kumwambia.

" mama si ulisikia aunt alisema nitafute cherehani"

" ndio Nana. Kwani kuna shida"

" hapana mama naona muda ni sasa, ngoja niende kwa mama Nestory kabla watu wengine hawajamuwahi, si unajua wiki hii ni wiki ya mwisho tuanze mwezi mtukufu ee?"

" Nana kuwa basi muwazi, unazunguka utadhani kuna uhalifu unapanga kuufanya?" Baada ya kuambiwa hivyo Nana alihisi kizunguzungu, mbona ghafla sana mama kamshtukia.

" aah! Sasa mama jamani, hapana sio hivyo ila tu nafaa kumuwahi kabla watu wengine hawajaikodi cherehani yake"

" anha sawa, muage baba yako" mama yake alimwambia na hicho ndo kitu ambacho Nana hakutaka.

" sasa mama na wewe jamani, baba tena, huoni yupo bize sana suhala la dada limekuja ghafla tutamchanganya."

" sawa nenda ila hakikisha unawahi" Nana alipoambiwa hivyo alifurahi sana akikimbilia chumbani kwake akachukua mkoba wake akaweka nguo kadhaa pamoja na mafuta yake, akatoka nje.

Alipofika nje aligeuka kuitazama nyumba yao kisha akaongea kimoyo moyo, samahani sana wazazi wangu inabidi niwahi huko niendako na kwa kweli sidhani kama ntawahi kurudi, niliacha utundu tangu zamani lakini mara hii ni ya mwisho. Sirudii tena nafanya mara hii tu.

ITAENDELEA........

SEHEMU YA: 05

Endelea.......
Nasreen alienda moja kwa moja nyumbani kwa kina Ruaida, lakini alikuta watu wengi nje na akashindwa kuingia ndani ya ukumbi. Aliamua kumtumia ujumbe Farida, mdogo wake Ruaida, akimwomba amsaidie kuingia. Farida alifika haraka na wakazungumza kidogo kuhusu kutokuwepo kwa Naima.

"Farida, Naima alitaka kuja sana, lakini ana dharura. Nimekuja kwa niaba yake," alisema Nasreen akijaribu kumfariji Farida.

"Pole sana, Nasreen. Tukubali tu hali ilivyo. Twende ndani tukamuone bibi harusi," alisema Farida huku akimwongoza Nasreen kwa siri kuelekea chumba cha bibi harusi.

Walipofika chumbani, Ruaida alifurahi sana kumuona Nasreen na kumkumbatia kwa furaha. "Nasreen, nilidhani Naima angekuja. Nimekumiss sana," alisema Ruaida kwa sauti ya huzuni kidogo.

"Ruaida, Naima alikuwa na dharura, lakini alinituma nij3 badili yake nimuwakilishe. Natumai haujachukia si ndio?" Alisema Nasreen huku akimtazama Ruaida machoni.

" ni siku yangu muhimu, lazima nijisikie vibaya kwa sababu... unaujua ukaribu wangu na Naima"

Najua dada Ruaida lakini, dada Naima Anaomba radhi sana, alipata hedhi yake leo na wewe pia si unamjua akiwa hedhi." alisema Nasreen kwa upole.

Ruaida alihisi huzuni lakini alitabasamu na kusema, "Sawa, Nashukuru sana kwa kuja pia, Nasreen Naima ni rafiki bora sana kwangu, ameona kushindwa kwake basi isiwe sababu ya mimi kukosa tabasamu ndo maana amemutuma hapa." Nasreen alitabasamu na kumkumbatia Ruaida.

" Da Ruaida uhakika kabisaa, nitahakikisha unatabasamu." Ruaida alimwambia nakuamiania mdogo wangu.

Nasreen alipata muda wa kubadili mavazi yake na kujipodoa vizuri kwa sherehe. Alijisikia vizuri na kujiunga na kundi la wasichana waliokuwa wakiimba na kucheza qasida kwa ajili ya harusi.

☆☆☆☆☆

Upande wa Ibrahim, alikuwa amechoka na alikuwa tayari kulala, lakini kabla hajalala, babu yake, Mzee Onana, alimwambia, "Ibrahim, tuende msikitini, kuna ndoa ya kufungisha huko si unajua tena ukishakuwa mzee wa kijiji." Aliongea mzee Onana.

Ibrahim hakupinga. Alivaa kanzu nzuri na kumuaga bibi yake kwa uzuri kabisa. Babu yake alimsifia kuwa kijana mtanashati na anayejipenda. Waliongozana moja kwa moja hadi msikitini. Sala ya magharibi ilifuata, kisha watu wote walisoma dua maalum kwa ajili ya ndoa.

Bwana harusi, ambaye alikuwa amepangwa maalum kwa ajili ya ndoa hiyo, alifurahi sana. Ibrahim alitamani yeye ndiye awe anafungishwa ndoa hapo, huku akili yake ikimuwaza Naima, yule binti mrembo sana aliyemuona siku hiyo.

Baada ya hapo, waliondoka kuelekea nyumbani kwa kina Ruaida. Wakati huo, Nasreen alikuwa na kundi la wasichana kadhaa wakicheza na kuimba qasida kwa ajili ya harusi. Sauti ya Nasreen ilikuwa ya kuvutia sana kiasi kwamba iliteka umakini wa watu wote waliokuwepo. Hata maharusi walipofika, walitulia kwanza kumsikiliza muimbaji.

Ruaida alimkaribia Nasreen wakati wa kwenda kumtunza na kusema kwa sauti ya shukrani na ya chini sana, "Nana, asante sana kwa kuja, na asante sana kwa sauti yako nzuri. Umeleta furaha kubwa kwenye sherehe yangu."

Nasreen alitabasamu kwa furaha na kusema, "Ni furaha yangu kuwa hapa na kuifanya siku yako iwe maalum Da Ruaida. Ndio wajibu wangu kama rafiki na dada yako mdogo." Ruaida alitabasamu na kumshukuru.

Sherehe iliendelea kwa furaha na vicheko, huku Nasreen akifurahisha watu kwa muda aliokuwa nao na marafiki hapo, kwa kuimba. Hakujutia kwenda kwa niaba ya dada yake, kwani aliweza kuleta furaha kwenye siku maalum ya Ruaida.


SEHEMU YA: 06

Endelea.......
Baada ya Nasreen kumaliza kuimba, wageni walikaribishwa vyema sana hadi chumbani kwa Ruaida. Ndoa ya Ruaida ilihitimishwa kisheria na kidini, na cheti cha ndoa kilitolewa kwa furaha kubwa. Wakati wa kuandaa chakula cha wageni, Nasreen alisaidia kwa bidii, akishirikiana na wenyeji vizuri sana. Nyakati zote hizo, Ibrahim alimuona Nasreen na alimtambua, lakini Nasreen hakumuona Ibrahim.

Ibrahim akiwa amekaa karibu na vijana wenzie, alisikia mazungumzo ya vijana wawili miongoni mwao ambao hakuwajua majina kwa upande wake, lakini waliitwa Hamza na Fatih. Hamza alisema,

"Huyu binti ni mrembo sana na anaonekana ni mgeni hapa kijijini."

Fatih alimjibu, "Hapana, sio mgeni. Alikuwa akiishi Dar es Salaam kwa muda mrefu na amerudi huku kijijini hivi karibuni."

Hamza ambaye hakuwa kamfahamu Nasreen hapo mwanzo alisema, "Mimi nimetokea kumpenda na natamani kumfanya wa kwangu daima yaani awe mke wangu."

Fatih alimcheka na kumwambia, "Yawezekana kumfanya wako, lakini wasichana waliokaa mjini kwa muda huwa hawakubali kuolewa vijijini labda kama umteke."

Hamza aliona hilo ni wazo zuri na akamwambia Mwenzie.

" kweli ee, naona bora hivyo "
" kama upo tayari kwa hilo mimi ntakusaidia" alijibu Fatih na Hamza akapanga mpango wa kumteka Nasreen baada ya harusi. Ibrahim alisikia mazungumzo hayo na akanyamaza kimya kama hajui kitu chochote.

Baada ya harusi, Nasreen aliondoka mapema sana ili awahi nyumbani kwa sababu aliondoka kwa kutoroka.

" naomba Mungu zaidi nyumbani niwe sijatafutwa maana, sijui ntajibu nini jamani" alijisemea huku akiongeza mwendo

Wakati anaondoka, vijana wale wawili, Hamza na Fatih, walimuona na kumfuata nyuma nyuma ili watimize lengo lao la kumteka na kumfanya mke wao.

Ulikuwa usiku, hivyo Nasreen hakujua kama anafuatiliwa, hata hivyo kijiji chao kilikuwa kijiji salama zaidi isingekuwa rahisi kwake kuhisi hatari yoyote ile. Alikuwa akitembea haraka sana ghafla akahisi vishindo vya watu wakikimbia nyuma yake.

" Tobaa! Kusiwe na watu wabaya tu" alijisemea Nasreen kimoyo moyo akaendelea na safari zake.

Nasreen aliongeza mwendo akaanza kutembea haraka, lakini alichelewa. Hamza aliwahi kusimama mbele yake na kuanza kumchekea.

" ki ukweli wewe ni mrembo sana, hivi unajua hilo?"

" hii mbuzi vipi tena jamani?" Aliwaza Nasreen.

Nasreen alifikiria kugeuka nyuma ili arudi alipotoka kwa usalama wake, lakini huko pia alikutana na mtu. Upande mwingine haukuwa na njia zaidi ya mashamba ya watu. Alianza kulalamika akiwaomba wampishe njia apite.

Hamza alitabasamu na kumwambia, "Samahani, sina nia ya kukuacha uende kwa sababu nataka uwe mke wangu."

Nasreen alishangaa na kucheka kwa sauti, eti awe mke wake? Huyu ni wazimu ee? Alimtazama vizuri kabisa na kumwambia, "Unaota ee? Siwezi kuwa mke wako hata ndotoni, niache nipite."

" kwani mimi nina kasoro gani lakini? Wewe mbona ni mwanamke mzuri tu, unafaa kuwa mwanamke wangu, nitakutunza"

" sikutaki jamani, hee! We kaka vipi?"

Walianza kubishana na wakati huo Fatih alimwambia Hamza, "Kujichelewesha kwako, unapoteza muda. Huyo ni wa kibebwa tu."

Fatih alimchukua Nasreen na kuanza kuondoka nae akiwa kampiga taxi bega. Nasreen alianza kupiga kelele akiomba aachwe.

" we kaka umechanganyikiwa, mimi sifai kuwa mke bhna, mi sitaki"
Hamza alimwambia, "Siwezi kukuacha kwa sababu nakupenda na bahati mbaya sina pesa za mahari, wala uwezo wa kukumiliki bila kutumia nguvu."

Nasreen aliendelea kupiga kelele akimlaani Hamza. Wakati huo huo, Ibrahim alitokea mbele yao, kwa kuwa Hamza ndo ambae alikuwa mbele. Ibrahim alimshambulia Hamza kwa mtama na kumuangusha shambani kwa kishindo. huku Fatih akimshangaa.
" jamani we kaka vipi?" Nana aliisikia hiyo sauti lakini hakujua huyo kaka aliekuja kusaidia alikuwa nani?.
Fatih alianza kukimbia na Nasreen. alimwambia Hamza, "Hakikisha unakuja, utamkuta mkeo nyumbani kwako."
" wakati huo Hamza alikuwa hoi lakini hakutaka kumkosa Nana awe mke wake.

Ibrahim alimfuata Fatih aliyekuwa akikimbia akiwa kambeba Nana begani. huku Nana akimpiga Fatih ngumi za mgongo akiomba kuachwa na kupiga makelele na kufurukuta. Ibrahim alimfuata Fatih, lakini Hamza alimshika Ibrahim mguu. Ibrahim alimwinua Hamza na kumpiga ngumi moja nzito ya sikio, akamdondosha chini kwa kuhisi kizunguzungu na kushindwa kuendeleza ubishi wake. Ibrahim alitabasamu kisha akamkimbilia Fatih, ambaye alikuwa mbele zaidi akiwa kambeba Nasreen.

Nasreen alifurahia zaidi baada ya kumuona Ibrahim,, na hapo alimtambua mtu ambae alikuja kumuokoa yeye alikuwa shemeji yake, Ibrahim Onana. na Ibrahim alimshambulia Fatih kwa mtama mrefu. Fatih alimwangusha Nasreen huko shambani na kujipanga upya kusimama ili na yeye apigane na Ibrahim. Walipigana kwa nguvu, lakini hatimaye Ibrahim alimshinda Fatih. Fatih alikimbia baada ya kupigwa mitama mara kadhaa na kuona. Mh! huu moto siuwezi.

Nasreen alimshangilia Ibrahim kwa furaha, "Asante sana, Shemeji, kusema ukweli umeupiga mwingi kwa kunisaidia! Umenisaidia sana Asante mno."

Ibrahim alitabasamu na kumwambia, "Usijali, Nasreen. Nipo hapa kukulinda, unadhani jambo baya likikukuta wewe dada yako atakubali kuolewa na mimi sasa? "

Nasreen alitabasamu na kumwambia " furaha yangu. Ni kuona nyie wawili mkifanikisha ndoa yenu, asante sana, hawa wapuuzi wawili, eti walitaka kunioa jamani."

Ibrahim alitabasamu na kuanza kuondoka bila kuongea zaidi. Nana alimtazama Ibrahim alivyokuwa akiondoka kwa madoido, ghafla moyo wake ukaanza kudunda.

" jamani Ibrahim ni mzuri nyie, alafu ana manguvu, ana kila sababu ya kupendwa na mwanamke kama mimi jamani." Alishika mashavu yake hisia akibaki kumtazama Ibrah. Ghafla akakumbuka Ibrahim ni shemeji yake, aiii! Nafsi ilimsuta akaanza kumlaani shetani.


SEHEMU YA: 07

Endelea.......
Nasreen alipofika nyumbani, alihisi moyo wake ukidunda kwa kasi. Milango yote ilikuwa imefungwa, na hali ya utulivu ilitawala. Alijua wazi kwamba familia yake ilikuwa imelala. Kwa haraka, alituma ujumbe kwa dada yake, Naima, akimwomba amfungulie mlango.

Naima, aliyekuwa amekaa sebuleni kwa wasiwasi, alishtuka kidogo aliposikia simu yake ikilia. Alikuwa akimsubiri Nasreen kwa hamu, akijua kwamba alihatarisha kila kitu kwa kumruhusu mdogo wake kuondoka bila idhini ya wazazi. Aliposoma ujumbe wa Nasreen, alinyanyuka haraka na kufungua mlango kwa tahadhari kubwa.

"Nana, umefanikiwa kurudi salama?" Naima aliuliza kwa sauti ya chini, akihakikisha hakuna mtu aliyesikia.

"Ndiyo, dada. Lakini nilikuwa na wasiwasi sana. Hakuna aliyeniulizia, siyo?" Nasreen aliuliza huku akishusha pumzi ndefu.

"Hakuna mtu aliyegundua. Tulia sasa," Naima alimjibu kwa utulivu, akimshika mkono na kumwongoza ndani kwa haraka. Wote wawili walitawanyika kimya kimya; Nasreen akaelekea chumbani kwake, huku Naima akirudi chumbani kwa aunt Tuma.


Naima alipofika chumbani kwa aunt Tuma, alijaribu kutembea kwa tahadhari ili asimshtue. Lakini ghafla, aunt Tuma alishtuka na kuwasha tochi ya simu yake, akimulika uso wa Naima.

"Unatoka wapi wewe, mwali?" Aunt Tuma aliuliza kwa sauti ya kushuku.

Naima aliganda kwa sekunde chache, akitafakari jibu la haraka. "Nilienda kunywa maji, aunt," alijibu kwa sauti ya chini.

Aunt Tuma alimkazia macho kwa muda, kisha akasema, "Usirudie kufanya ujinga wa kutoka usiku. Kama ni maji, si ungeniambia nikuletee? Haya, lala sasa."

"Samahani, aunt. Sitafanya tena," Naima alijibu kwa unyenyekevu, kisha akapanda kitandani na kushusha pumzi ndefu ya faraja.

Chumbani kwake, Nasreen alijilaza kitandani baada ya kuoga na kujisafisha. Alimshukuru Mungu kwa kumfikisha salama nyumbani bila kugundulika. Lakini ghafla, taswira ya Ibrahim ilimjia kichwani. Uso wake mtanashati na tabasamu lake la upole vilimjia kama ndoto. Nasreen alijikuta akimlaani shetani kwa mawazo hayo, akijaribu kuyafukuza kwa nguvu.

"Ni shemeji yangu, siwezi kumtamani," alijisemea kwa sauti ya chini, akijigeuza upande mwingine wa kitanda na kufumba macho kwa nguvu.


Asubuhi ilipofika, Naima alikuwa wa kwanza kuamka. Alisogea dirishani kwake na kumuita Nut, kasuku wake mpendwa. "Nut, njoo hapa," aliongea kwa sauti ya upole, akinyosha mkono wake nje ya dirisha.

Nut aliruka haraka na kutua mkononi mwa Naima. "Habari yako, Nut?" Naima aliuliza huku akimwangalia kwa upendo.

Nut alitikisa mkia wake na kuruka kidogo, kana kwamba alikuwa akijibu, "Nipo vizuri."

Naima alitabasamu na kusema, "Najua unatamani nitoke nje, tukaongee zaidi kwenye kiota chako. Lakini siwezi kutoka, Nut. Mimi ni mwali sasa, na hivi karibuni nitaolewa."

Nut alihuzunika, akainamisha kichwa chake. Naima alimtikisa kwa upole na kusema, "Usijali, Nut. Itabidi umzoee Nana. Atakupa kila aina ya matunzo unayostahili."

Nut alibaki kimya, akimtazama Naima kwa macho ya huzuni.


Baada ya muda, familia ilikutana mezani kwa kiamsha kinywa. Nasreen aliagizwa kumpelekea Naima chakula chumbani kwake, kwani Naima hakuwa akiruhusiwa kutoka nje. Nasreen alibeba sinia na kuelekea chumbani kwa dada yake.

"Dada, habari za asubuhi?" Nasreen aliuliza huku akimkabidhi chakula.

"Asubuhi ni njema, Nana. Umeamka salama?" Naima alijibu kwa tabasamu.

" ndio nipo salama sana japo uchovu kidogo tu"

" pole, usikute jana umecheza sana Qasida, nakujua wewe Nana."

"Wacha nikuambie kilichotokea jana harusini," Nasreen alianza kusimulia kwa furaha. Alimweleza Naima kila tukio, kuanzia nyimbo za qasida hadi jinsi alivyokutana na watu mbalimbali. Naima alicheka sana, hasa aliposikia jinsi Nasreen aliyokumbana nayo usiku alipokuwa akirudi nyumbani.

"Unajua, dada, Ibrahim ni mwanaume wa kipekee sana. Yule ni Askari anayejiheshimu na mwenye uwezo wa kujitegemea, usimkose mwanaume anaekupenda kwa dhati kama yule." Nasreen alisema kwa tabasamu.

Naima alitabasamu na kusema, "Ni wazi kwamba familia yangu nzima mnafurahia kuona mimi naenda kuolewa naye. Sasa kwa nini nisimridhie?"

Nasreen alimkumbatia dada yake kwa upendo na kusema, "Usimuwaze tena Salum, tafadhali. Ibrahim ni chaguo sahihi."

Naima alikubali kwa kichwa na kusema, "Nakuahidi, Nana. Nitajaribu kumpa nafasi Ibrahim."

Baada ya mazungumzo hayo, Nasreen alitoka nje kuendelea na ratiba zake, huku Naima akibaki chumbani akitafakari. Alianza kuona umuhimu wa kumpa Ibrahim nafasi, akiamini kwamba huenda Salum hakuwa sehemu ya hatima yake.


SEHEMU YA: 08

Endelea.......
Ibrahim alikuwa ameketi kwenye sebule ya nyumba yao akishirikiana na mdogo wake Mariam kupanga mavazi yatakayofaa kwa mke wake mtarajiwa, Naima. Mariam alitabasamu huku akiwa amejipanga na mawazo mengi mazuri.

"Kaka, mi nadhani wewe na bibi harusi mvae sare siku ya harusi yenu. Mnaweza mtoke kwa rangi zinazolingana!" Mariam alisema kwa furaha.

Ibrahim alitingisha kichwa huku akitabasamu, "Hapana, Mariam. Sio lazima maharusi wavae sare. Mimi najua namna ambavyo mwanamke wangu akivaa na mimi nikavaa, bado tutaendana mno."

Mariam alimtazama kwa macho yenye mshangao, kisha akasema, "Sasa kwa nini umeniita hapa kama unajua kila kitu, kaka?"

Ibrahim alicheka kwa sauti ya chini na kusema, "Mariam, kuna baadhi ya vitu vinahitaji macho ya mtoto wa kike. Unajua vizuri urembo wa mwanamke unavyopaswa kuwa."

Mariam alitabasamu na kuanza kuonyesha mawazo yake, akimchagulia aina ya vipodozi na mapambo ambayo yanadhaniwa kumfaa Naima kutokana na umbo lake zuri na sura yake ya kuvutia.

Wakiwa wamejikita katika majadiliano hayo, ghafla simu ya Ibrahim iliita mezani. Alinyanyua simu na kutazama jina lililoonekana. Moyo wake ulipiga kwa nguvu—ilikuwa ni Naima. Ibrahim alishangazwa mno, kwani mara zote yeye ndiye aliyekuwa akimpigia Naima, lakini leo ni tofauti.

Alimtazama Mariam kwa macho yanayodhihirisha mshtuko na furaha. Mariam alimtazama naye akitabasamu, kisha akaondoka polepole huku akisema kwa utani, "Naona wifi kafanya hatua moja zaidi leo. Niachie nafasi, kaka." Mariam aliondoka huku akicheka kwa upole.

Ibrahim alikusanya hisia zake na kisha akapokea simu kwa nidhamu, akianza kwa sauti ya utulivu, "Mke wangu mtarajiwa, habari zako?"

Simu hiyo ilianza kwa tabasamu upande wa Naima. Kwa mara ya kwanza, sauti yake ilikuwa ya upole zaidi na haikuonyesha ukuta wa baridi aliokuwa nao hapo awali. "Umeamkaje, mpenzi?" Naima alisema kwa sauti tamu.

Ibrahim alisita kwa sekunde chache, macho yake yakiwa yamejawa mshangao. Alihisi kana kwamba hakusikia vizuri. "Hivi kweli hii ni Naima? Au umekula kitu kibaya? Una homa, mpenzi wangu?" aliuliza huku akiona moyo wake ukipiga kwa kasi.

Naima alicheka kwa sauti tamu, na kusema, "Hapana, sina homa. Kwa nini unaniuliza hivyo?"

Ibrahim alijibu huku akiona hajui pa kujificha, "Kwa sababu unasema maneno ambayo hata sijui kama ni kawaida kutoka kwako. Kweli Naima wa leo ni yule yule wa jana?"

Naima alitabasamu zaidi na kusema, "Naongea maneno haya kwa sababu niko mbele ya daktari wangu binafsi. Sina cha kuhofia, si ndiyo?"

Ibrahim alihisi msisimko wa ajabu, mapigo ya moyo wake yaliongezeka mara dufu. Alijikuta akishikilia kifua chake kwa utulivu, akicheka kwa upole. "Naima, kata kwanza. Nakupigia mwenyewe," alisema huku akijaribu kudhibiti furaha yake.

Naima alikata simu, na kwa sekunde chache, alicheka peke yake, tabasamu lake likiangazia uso wake mzuri na angavu. Upande wa Ibrahim, alibaki akijaribu kujituliza, huku akimtazama simu yake kana kwamba haamini lililotokea. Alimshukuru Mungu kimya kimya kwa mabadiliko ya taratibu kati yao.


Baada ya muda mfupi, simu ya Ibrahim iliwaka tena. Alimpigia Naima. Naima alipokea kwa sauti ya utulivu, lakini utamu wa sauti yake ulidhihirisha furaha iliyokuwa ndani yake.

"Mpenzi," alizungumza Naima, sauti yake ikiwa nyepesi kama wimbo wa asubuhi.

Ibrahim alitabasamu upande wa pili wa simu na kusema kwa utani, "Sasa naamini ni kweli wewe ni Naima. Sauti yako leo ni tofauti kabisa, sijui imebadilika kwa sababu gani?"

Naima alicheka kwa upole na kusema, "Labda imebadilika kwa sababu sasa najifunza kuwa karibu na wewe hapo, mume wangu mtarajiwa."

Ibrahim alihisi moyo wake ukidunda kwa kasi zaidi. "Huo ndio ugonjwa wako sasa, Naima. Ni umeathirika kwa mapenzi yangu! Au kuna kingine?" alisema kwa utani huku wote wakicheka.

Baada ya utani huo wa kimapenzi, Ibrahim aliongoza mazungumzo kwenye mada muhimu zaidi. "Naima, tena afadhali umenitafuta, ni kuhusu mavazi yetu ya harusi, unadhani tuvae nguo za rangi gani? Au kuna mtindo wowote unaopenda?"

Naima alitulia kwa muda, kisha akasema kwa aibu, "Ibrahim, huenda ikakushangaza, lakini mimi sijui sana kuhusu mitindo ya kisasa ya mavazi."

Ibrahim alitabasamu na kumjibu kwa sauti ya upole, "Usijali, mke wangu mtarajiwa. Hilo ni jambo dogo sio kila mti kajiweka huko."
Naima alinyamaza kidogo, kisha akamjibu, "Nadhani Nana anaweza kuwa na unashauria mzuri zaidi. Ngoja niongee na Nana kisha tutakupatia mawazo yetu."

Naima alimuita Nasreen, ambaye alikuja kwa haraka huku akiwa na shauku. "Nana, Ibrahim anauliza kuhusu mavazi yetu ya harusi. Kama unavyojua dada yako hakuna nalo jua" alisema Naima kwa tabasamu.

"Simu ikatwe kwanza, dada! Mimi siwezi kuongea shemeji akiwa hewani" Nasreen alisema. Naima alimuelewa Nasreen kisha akakata simu,

Nasreen aliingia mtandaoni na kuzisaka picha kadaa kisha alimuonyesha Naima, wakiwa wanajadili rangi na mtindo wa mavazi.

Baada ya muda mfupi, walichagua mavazi rasmi yaliyopangiliwa vyema. Naima aliwasiliana na Ibrahim kupitia WhatsApp, akamtumia picha za mavazi waliyoyapenda na kuchagua. Ibrahim alipendezwa sana na mapendekezo hayo.

" Hizi ni safi kabisa kwa wakati wa sasa Naima, kumbe Nasreen ni mtaalamu?"

" ndio, ujue Nana ni fundi mzuri sana, alipokaq kwa Aunt Tuma huko Dar es Salaam alijifunza ushonaji na hadi sasa kabobea, ndo maana kwake ni rahisi sana."

" kwa kweli hata mimi naona, sasa basi acha niwasilishe hizi kwa mafundi alafu ntakurejea" alimwambia Naima, Naima alitabasamu.

Baada ya muda, Ibrahim alikuwa tayari na mtindo kamili wa mavazi kwa ajili ya harusi yao. Alipowasiliana na mafundi wake, waliomba vipimo vya bibi harusi. Ibrahim alishangaa na kusema kimoyomoyo, "Huu ni mtihani sasa. Nitafanyaje kupata vipimo vya Naima bila kumpa usumbufu?"

Alimpigia simu Naima mara moja, na wote wawili walianza kuwaza suluhisho la haraka. Wakiwa wanajadili, ghafla Mariam alikuja na kusema, "Kaka, usijali. Siku ya kutoa mahari si ndo leo nitakuwepo pia, na kwa sababu Nasreen atakuwa pale, itakuwa rahisi kwake atampima kwa siri na kuniletea vipimo vyote."

Ibrahim alitabasamu kwa furaha na kusema, "Hilo ni wazo zuri, Mariam. Asante sana kwa msaada mdogo wangu mzuri.!"


SEHEMU YA: 09

Endelea.......

Muda ulipofika, Mzee Onana, akiwa amejawa na fahari, aliongoza msafara wa wazee wenzie kuelekea nyumbani kwa Mzee Omary kwa ajili ya kutoa mahari ya Naima. Ilikuwa ni tukio kubwa lililosheheni furaha. Shangwe, vigelegele, na nyimbo za asili vilitawala wakati mzigo wa mahari ulipokelewa kwa mikono miwili.

Nyumbani kwa kina Naima, hali ya furaha ilikuwa dhahiri. Lakini Naima mwenyewe alikuwa chumbani akizungumza na Ibrahim kwa simu. "Sikia kelele hizi, Ibrahim. Vigelegele vinapita uwezo wangu wa kuvumilia, nahisi kama vile masikio yangu yatapasuka." alisema kwa utani huku akitabasamu.

Ibrahim alicheka na kusema, "Pole, mke wangu. Unavumilia kwa sababu yangu, si ndiyo? Jikaze mara hii tu."

Naima alitabasamu na kusema kwa upole, "Kwani nilichelewa wapi kukupenda wewe, Ibrahim? Hivi unajua kama wewe ni very romantic. "

Ibrahim alisisimka moyoni, lakini aliendelea kucheka na kumjibu, "Wakati ambao mimi pia sikuruhusu umpende mtu mwingine. Nilijua siku moja utakuwa wangu tu. Nakupenda sana Naima."

Kauli hiyo ilimfanya Naima amsifu Ibrahim kimoyomoyo, akimwona kuwa mwanaume wa kipekee. Kwa dakika hizo chache za mazungumzo yao, walihisi ukaribu zaidi na zaidi, huku hisia zao zikikua kwa kasi.

☆☆☆☆☆☆

Mariam alijipenyeza kwa ustadi kutoka kwa bibi yake, akijua wazi kwamba kazi aliyokuwa nayo ilikuwa muhimu sana kwa kaka yake, Ibrahim. Alimtafuta Nasreen kwa haraka, alimkuta akiwa nje akimwagilia maua. Mariam alimsogelea kwa tahadhari na kusema kwa sauti ya chini, "Nana, nina shida kubwa."

Nasreen aligeuka na kumwangalia Mariam kwa macho ya udadisi. "Shida gani, Mariam?" aliuliza kwa upole.

Mariam alisita kidogo, kisha akasema, "Nahitaji vipimo vyote vya bibi harusi, lakini sijui nitampata vipi Naima?"

Nana alitabasamu na kusema, "Aunt Tuma analinda mlango wake kama simba anaelinda watoto wake, hataki masihara kabisa na bibi harusi wake."

Mariam alitabasamu kwa upole, akijua changamoto hiyo ilikuwa kubwa lakini si ngumu kumshinda Nasreen. "Ni kweli, aunt Tuma ni mkali sana. Lakini nitajitahidi. Usijali, Mariam," alisema huku akitikisa kichwa kwa ishara ya kukubali.

Mariam alishusha pumzi ya faraja na kusema, "Tafadhali, fanya uwezavyo. Kaka yangu anakutegemea kwenye hili."

Nasreen alijipenyeza kwa ustadi kuelekea chumbani kwa Naima, akitembea kwa tahadhari ili asisikike. Alipofika, aligonga mlango kwa upole na kuingia. Alimkuta Naima akiwa bado anaongea na simu, uso wake ukiwa umejaa tabasamu. Nasreen alitabasamu na kusema kwa utani, "Haya sasa, dada, hayo ndiyo mambo ninayoyapenda. Em mwambie shem akate simu mara moja nikufanyie vipimo."

Naima alicheka na kumwambia Ibrahim, "Mpenzi, ngoja nikate simu kwanza. Nana anataka kunifanyia vipimo." Ibrahim alikata simu kwa utulivu, akijua kazi hiyo ilikuwa muhimu.

Nasreen alianza kumpima Naima kwa ustadi, huku akiutazama uso wa dada yake ulivyojaa furaha. "Dada, una bahati sana kuwa na shemeji kama Ibrahim. Hakikisha unaishika nafasi yako vyema. Mimi nakuombea kila siku," alisema Nasreen kwa sauti ya upendo.

Naima alitabasamu na kumkumbatia mdogo wake kwa nguvu. "Asante, Nana. Wewe ni baraka kwangu," alisema kwa sauti ya upole.

Baada ya kumaliza kazi hiyo, Nasreen alichukua daftari lake muhimu na kutoka chumbani kwa tahadhari ile ile aliyotumia kuingia.


Nasreen alimkabidhi Mariam karatasi ya vipimo, akisema kwa tabasamu, "Haya, kazi imekamilika. Peleka kwa kaka yako sasa."

Mariam alirudi nyumbani kwao kwa haraka na kumkabidhi Ibrahim karatasi hiyo. Ibrahim alitabasamu kwa furaha na kusema, "Asante sana, Mariam. Umenisaidia sana."

Mariam alitabasamu na kusema kwa utani, "Lakini kaka, mwambie Naima aongeze kula kidogo. Mwili wake hauendani na umri wake."

Ibrahim alicheka kwa sauti na kusema, "Nitamhimiza hilo. Asante kwa ushauri wako, mdogo wangu."

Baada ya muda mfupi, Ibrahim alipiga picha ya vipimo hivyo na kuwatumia mafundi wake kupitia WhatsApp. Mafundi walimjibu baada ya muda mfupi, wakisema, "Tayari vipimo tunavyo. Subiri tu nguo zako."

Ibrahim aliwakumbusha kwa upole, "Tafadhali, fanyeni haraka. Sina muda wa kutosha."

Ibrahim alishusha pumzi ya faraja, akijua kwamba kila kitu kilikuwa kikienda sawa. Alimshukuru Mungu kwa kuwa na familia inayomsaidia na kumpa nguvu. Alijua kwamba harusi yake na Naima ilikuwa karibu, na kila kitu kilikuwa kikienda kwa mpangilio mzuri hadi wakati huo.


SEHEMU YA: 10

Endelea.......

Majira ya asubuhi, Anati alikuwa ametoka dukani akitafuta mahitaji madogo. Alipokuwa akipanga bidhaa, alikutana na msichana mrembo asiye wa kawaida kwenye macho yake. Msichana huyo alimsalimia kwa sauti ya upole na kujitambulisha.

"Habari yako dada? Naitwa Latifa, samahani kidogo, lakini unakaa kwa kina Naima?" Latifa aliuliza, akitabasamu kwa heshima.

Anati, kwa kuwa alikuwa mgeni katika kijiji hicho na hakuwa na ufahamu mwingi kuhusu majirani, alijibu, "Ndiyo, nakaa huko kwa kina Naima. Kuna jambo gani kwani?"

Latifa alifungua mkoba wake na kutoa bahasha nyembamba, kisha akasema kwa dhati, "Naomba hii bahasha umpelekee Naima. Tafadhali, usiisome, mpelekee mwenyewe asome."

Anati alihisi kutomuamini kwa muda, lakini kwa utulivu wa msichana huyo na sauti yake ya upole, alikubali kuchukua bahasha hiyo. "Sawa, nitaipeleka," alisema, huku akiondoka haraka bila kutoa nafasi ya mazungumzo zaidi.

Wakati huo huo, nyumbani kwa kina Naima kulikuwa na shughuli nyingi. Nasreen na Aunt Tuma walikuwa wameshika misingi ya kazi zao, wakishona kwa umakini mkubwa. Mikono yao ilikuwa bize, vichwa vyao vikiwa na mawazo ya kupanga kila kitu kiukamilifu kwa ajili ya harusi. Shangwe na vicheko vyao vilivunjika kwa haraka Anati alipoingia ndani akiwa kimya.

Anati, aliwaona Nasreen na Aunt Tuma ambae ni mama take wakiwa bize, hakutaka kuwavuruga. Badala yake, alielekea moja kwa moja chumbani kwa Naima. Mlango wa chumba ulikuwa wazi kidogo, na alipoingia, alimkuta Naima akiwa ameketi kwa utulivu akisoma Qur-an. Mwangaza wa asubuhi ulilenga uso wa Naima, ukionyesha uzuri wake wa kipekee.

"Dada" Anati aliita baada ya kuingia ndani.

"kuna nini?" Naima aliuliza kwa mshangao, akinyanyua macho kutoka kwenye Qur-an yake. Haikuwa kawaida ya Anati kuingia kwa kunyata chumbani kwake.

Anati alisita kwa muda kabla ya kutoa bahasha. "Kuna msichana amesema anaitwa Latifa amenipa hii bahasha nikupe. Alisema ni yako na uisome mwenyewe," alisema huku akimkabidhi bahasha hiyo.

Macho ya Naima yalibadilika ghafla, hisia mchanganyiko za mshangao na furaha zikionekana wazi usoni mwake. "Latifa? Amekuja huku?" aliuliza kwa sauti yenye mshangao.

Anati alitikisa kichwa na kusema, "Dada mimi ni mgeni hapa kijijini. Sijui mengi kuhusu watu wa hapa, lakini ndiye aliyenipa bahasha hii."

Anati hakutaka kusubiri majibu zaidi; alitoka chumbani polepole, akimwacha Naima akiangalia bahasha hiyo kwa macho yaliyojaa udadisi. Naima aliifunika Qur-an na kuweka mikono yake juu ya bahasha kwa makini, kana kwamba ilikuwa lulu yenye thamani. Uso wake ulijawa na tabasamu lenye maana kubwa, na ghafla alijikuta akisema kwa sauti ya chini, "Salum wangu mimi."

☆☆☆☆☆☆

Wakati huo huo, upande wa pili Ibrahim alikuwa akisoma jumbe kupitia WhatsApp. Alipata ujumbe kutoka kwa mmoja wa mafundi wake ambao aliwatumia pendekezo la kazi ya kumshonea nguo._"Boss Ibrah, mzigo wako umeanza safari leo asubuhi. Hadi kufika mchana, utakuwa mjini Tanga tayari."

Ibrahim alitabasamu kwa furaha, akijua kwamba nguo zao maalum za harusi zilikuwa njiani. Alijipanga vizuri kuondoka mapema kuelekea Tanga mjini, akijua kuwa kila kitu kinakaribia kuwa kamili.

Aliweka simu yake chini, akifikiria kuhusu Naima. Hisia zake kwa Naima zilikuwa zikikua kila siku, na kila sekunde, na kila hatua ya maandalizi ya harusi yao ilimfanya apate uhakika zaidi kwamba alifanya uamuzi sahihi. Na Naima hatimae alimkubali yeye.


Soma Kitabu

SOMA MAELEKEZO

Bonyeza hi "Soma Kitabu" kisha itakupeleka kwenye fomu yaku login, hakikisha ume login na namba uliyojiunga nayo ndipo utaendelea sasa kusoma kitabu chote