Zaria hakutegemea kama angekuja kupendana na Shemeji yake Kenan huku upendo aliokua nao kwa mumewe Dante ukafa. Sio kama alitaka, ila kuna mambo yalipekelea kuzaliwa kwa penzi zito baina yake na shemeji yake.
Je ni mambo gani hayo? Nakuja…….
Sehemu ya : 01
Ilianza kama ndoa ya mfano. Watu waliowajua Dante na Zaria walikuwa wanawaonea wivu wa heri. Walikua marafiki, wapenzi na sasa wamekua mume na mke kwa miaka mitatu❤️.
Hakukuwa na usaliti, hakuna ugomvi, hakuna makelele ya majirani kuomba waache kugombana kwa sababu hawakuwahi kugombana.
Zaria alikuwa msomi mwenye shahada mbili, lakini hakufanya kazi. Dante, mume wake, hakuwa na mpango wa kumruhusu.
“Sitaki mke wangu atoke nje kuhangaika na kazi wakati mimi nipo” Dante alimwambia mara kwa mara. “Huwezi kupambana na dunia hii wakati mimi nipo. Ntakupatia kila kitu unachotaka”
Zaria aliishi maisha ya amani. Alikuwa nyumbani muda mwingi, akisoma vitabu, akipika mara chache kwa kupenda kwake, akipendeza, akisubiri mumewe arudi kazini. Dante alikuwa mfanyabiashara. Alimiliki maduka ya vifaa vya ujenzi maeneo tofauti jijini. Alikua anafanya vizuri.
Siku moja Zaria alianza kujisikia vibaya. Kichwa kilimuuma sana, macho yalimzunga, alihisi kama dunia inamzunguka kila akisimama. Hapo mwanzo aliona ni hali ya kawaida.
“Pengine ni presha au njaa” alijisemea. Lakini hali haikubadilika hata baada ya kula vizuri na kulala.
Alipoanza kuona kuwa kila siku hali inazidi kuwa mbaya, ndipo Dante alipoanza kumshawishi aende hospitali.
“Babe, tafadhali nenda tu kwa daktari, Siwezi kukaa hapa nikikuona unaumia hivi. Leo nimeahirisha kazi kwa ajili yako” Dante alisema jioni moja.
“Leo siwezi, Lakini kesho ntaenda, sawa?” Zaria alijibu kwa udhaifu.
“Asante mpenzi wangu. Ukifika hospitali, niite kama kuna chochote”
Kesho yake, Dante hakuweza kumpeleka hospitali kwa sababu alikua na kikao muhimu ofisini. Zaria akaenda peke yake.
Hospitali ya mtaa wao ilikuwa tulivu, haikuwa na msongamano. Alipokelewa vizuri, akapimwa na kufanyiwa vipimo mbalimbali.
Baada ya kusubiri kwa zaidi ya saa moja, daktari aliyeitwa Samweli alirudi na bahasha ya majibu. Alimwita Zaria kuingia kwenye chumba chake.
“Bi Zaria” Dokta Samweli alimuangalia kwa macho ya huruma. “Naomba uketi vizuri”
Zaria alikaa kimya, moyo wake ulikuwa unadunda kwa kasi.
“Tumefanya vipimo vyote, Na kwa masikitiko makubwa…tumegundua kuna uvimbe kwenye ubongo wako” Aliongea Dokta Samweli kwa upole
Zaria alishindwa kuongea. Alimtazama daktari kana kwamba hakusikia vizuri.
“Uvimbe upo sehemu ngumu sana kufanyiwa upasuaji. Tumefanya uchunguzi wa kina, lakini tumebaini kuwa umesambaa kwa kiwango kikubwa.”
“Unamaanisha nini…?” Zaria aliuliza, macho yakiwa na machozi tayari.
“Namaanisha… maisha yako yamebakisha muda mfupi. Tunaamini ni kati ya miezi minne au mitano ya kuishi, ikiwa hali haitabadilika”
Zaria alishindwa kujizuia. Alilia kwa uchungu. Akajikunja kwenye kiti, akashika kichwa. Daktari Samweli alijaribu kumtuliza kwa muda mrefu, lakini kilio kilikuwa kizito.
“Pole sana Bi Zaria” daktari alisema. “Hatuwezi kufanya upasuaji kwa sasa, lakini kuna dawa ambazo zitakusaidia kupunguza maumivu na kuchelewesha kasi ya ugonjwa. Tutaendelea kukufuatilia kila wiki”
Zaria alinyamaza kwa muda. Kisha akauliza kwa sauti ya chini:
“Naweza kuishi miezi mingapi zaidi…kama nitakuwa natumia dawa hizi?”
“Pengine miezi mitano au zaidi kidogo. Lakini siwezi kukuhakikishia.”
Baada ya kutulizwa na kupatiwa dawa, Zaria aliondoka. Safari ya kurudi nyumbani ilikuwa ndefu na kimya. Alijisikia kama dunia nzima imesimama. Hakutaka kuamini kile alichoambiwa.
Alipofika nyumbani, alimkuta Dante amerudi mapema kutoka kazini.
“Zaria!” Dante alimkimbilia na kumbusu. “Habari ya hospitali? Nini kimeonekana?”
Zaria alikaa kimya. Kisha akaanza kulia.
“Babe, usiniambie ni kitu kibaya, Umeona nini?” Dante alisema kwa hofu
“Nina uvimbe kwenye ubongo…Dokta amesema nitakufa kabla ya miezi mitano…”
“Hapana, Hapana mpenzi wangu. Sio wewe. Hapana. Hii si kweli” Dante alishika kichwa
“Ni kweli, Wamesema hakuna upasuaji. Dawa tu za kupunguza maumivu” Zaria alijibu kwa sauti ya kulia
Dante alikaa kimya kwa muda. Kisha akamkumbatia mkewe kwa nguvu.
“Tutapambana pamoja. Siwezi kukupoteza. Sitaki kukuona unaumia. Nipo hapa, Zaria. Tutaishi kila siku kama ni ya mwisho. Tafadhali, usilie”
Zaria alijaribu kutabasamu kidogo. Alijisikia angalau vizuri kuona upendo wa mumewe.
Wiki mbili zilizofuata, Zaria alikua analia kila siku. Hakuamini kuwa maisha yake yamebakiwa na miezi minne tu. Lakini kwa mapenzi ya Dante, alijifunza kukubaliana na hali.
Dante alifanya kila kitu. Alitoka kazini mapema kila siku, akapika mwenyewe, akafanya usafi, akamuogesha Zaria. Aliwasha redio na kucheza naye, alimpeleka matembezi mafupi. Walicheka na kulia pamoja. Alifanya kila siku kuwa ya kipekee.
Lakini Zaria hakumwambia mama yake aliyekua Tabora kuwa anaumwa, Alisema:
“Sitaki mama ajue ninaumwa kiasi hiki. Nitampigia mara kwa mara kuonyesha niko sawa. Sitaki ashtuke”
Lakini hali ilianza kubadilika wiki ya tano. Dante hakuwa yule yule. Alianza kurejea nyumbani usiku sana. Hakua na tabasamu wala mapenzi yale ya mwanzo. Alikua mkali. Alikua kimya. Hakuwa tena anampikia Zaria wala kumsaidia.
Siku moja Zaria alimuuliza
“Babe, mbona siku hizi huniangalii tena? Umekuwa mbali sana…”
“Unaona kama sikuangalii? Huwezi hata kujitahidi kupika chai. Unataka kila kitu nifanye mimi?” Dante alijibu kwa hasira
“Mimi mgonjwa…”
“Basi kaa tu apo uendelee kusema ni mgonjwa” Dante aliongea kwa sauti ya kukasirika na kutoka nje.
Zaria alijikuta analia kila siku. Alikua analala njaa mara nyingine. Wakati mwingine Dante hakurudi nyumbani usiku mzima. Ilipofika wiki ya sita, akaanza kuoa Dante anampiga.
Siku moja alimkuta Dante kwenye simu usiku wa manane, akicheka sana.
“Wewe unacheka na nani usiku huu?” Zaria aliuliza kwa sauti ya taratibu.
Dante alimwangalia kwa macho ya hasira.
“Usinihoji. Wewe ni mgonjwa, si polisi.”
“Kuna mtu mwingine? Kuna mwanamke mwingine Dante??”
“Niache!, Sitaki kelele” Dante alisimama kwa hasira akampiga Zaria kofi.
Zaria alianguka sakafuni. Alijikokota hadi chumbani na kulia usiku mzima. Asubuhi alipokua peke yake alitazama dirishani na kusema kwa sauti ya chini:
“Bora ningekufa wiki ya kwanza…kuliko kuona upendo wote ukibadilika hivi…”
Lakini hakuwa tayari kusema chochote kwa mama yake wala kwa rafiki yeyote. Alikua kimya, lakini ndani ya moyo wake alianza kuhisi kuna mtu mwingine. Mwanamke mwingine. Lakini hakuwa na ushahidi. Na hakumjua hata jina.
Lakini alijua upendo wao umebadilika. Na kwa mara ya kwanza, Zaria akajikuta akimwomba Mungu kwa sauti ya chini
“Mungu…kama bado una mpango na maisha yangu… nisaidie. Siogopi kufa…lakini siwezi kufa kwa huzuni ya mapenzi kupotea”
Je nini kitaendelea???
Nakuja……
SEHEMU YA : 02
Dante alikuwa mtu mwingine kabisa. Hakukuwa na dalili hata moja ya yule mwanaume aliyekuwa akimpenda Zaria kwa moyo wote.
Sasa alikuwa na hasira zisizoeleweka. Kila siku, alirudi nyumbani akiwa amekunja uso, hakuwa akizungumza, na hakutaka kuona wala kusikia kitu kutoka kwa Zaria.
Lakini kilichomuumiza zaidi Zaria ni kwamba Dante alianza kumpiga. Si mara moja. Alianza kwa kofi, baadaye mateke na hata kumkaba. Zaria alianza kupata maumivu mwilini.
Alama nyekundu zilianza kujitokeza kwenye mikono yake, mapajani na hata mgongoni. Alilia sana usiku, si kwa sababu ya maumivu ya mwili pekee, bali kwa sababu ya maumivu ya moyo💔.
Siku moja alipigwa vibaya sana. Dante alirudi akiwa amelewa kidogo. Hakumwambia hata “hujambo.” Alipotaka kumkaribisha chakula, Dante alimvuta kwa nguvu hadi jikoni.
“Wewe una akili kweli? Unanipikia nini hii?” Dante aliuliza kwa sauti kali.
“Nimepika wali na maharage kama ulivyosema jana…” Zaria alijibu kwa sauti ya upole.
“Usinijibu!” Dante alipiga kofi moja la nguvu.
Zaria alianguka chini. Dante hakuishia hapo. Aliendelea kumpiga mateke kama ya farasi au ya punda. Mpaka alipohisi amechoka ndipo akaenda sebuleni na kuwasha TV kana kwamba hakufanya kitu.
Zaria alibaki sakafuni, akivuja damu puani, akitetemeka.Aliposimama, alijua hilo lingeweza kuwa tukio lake la mwisho kama angeendelea kukaa hapo.
Aliingia chumbani kwake, akachukua khanga moja, akajifuta damu na machozi, kisha akavaa viatu na kutoka nje.
Alitembea bila kujua aende wapi. Alienda mpaka akafika kwenye sehemu ya wazi yenye miti midogo midogo na nyasi ndefu, mbali kabisa na nyumba yao. Alikaa kwenye jiwe kubwa, akaangalia angani, macho yakiwa yamejaa machozi.
Alikua hana pa kwenda. Hakutaka kumpigia mama yake. Mama yake alikuwa Tabora na hakujua chochote kuhusu ugonjwa wake. Kama angeropoka, mama angejua kila kitu. Na hilo Zaria hakutaka kabisa litokee.
Lakini kulikuwa na mtu mmoja tu ambaye Zaria alijua angemsaidia kwa moyo wake wote. Huyo alikuwa Kenan.
Kenan ni rafiki mkubwa sana wa Dante. Walikuwa marafiki tangu chuo kikuu. Wamepitia mengi pamoja. Kenan alikuwa mume wa Alisha, mwanamke ambaye Dante alimtafutia na hata kuwa msimamizi wao wa ndoa. Kwa hiyo Kenan alikuwa kama ndugu wa familia.
Zaria alitoa simu yake mfukoni akampigia Kenan.
“Halo, Kenan…” alizungumza kwa sauti ya unyonge.
“Shemeji! Upo salama?” Kenan aliuliza mara moja.
“Hapana… tafadhali, unaweza kuja? Tafadhali sana, njoo…”
Kenan hakusubiri maswali zaidi. “Niko njiani”
Haikupita muda mrefu, gari ya Kenan aina ya Rav4 nyeusi ilisimama karibu na pale alipo Zaria. Alishuka kwa haraka na kumkimbilia.
“Zaria! Mungu wangu… nini kimekupata?” alimuuliza kwa hofu akimwangalia usoni na kwenye mikono, alama za kipigo zikiwa wazi kabisa.
Zaria alilia. “Kenan, nimeteseka… nimenyamaza sana… lakini siwezi tena. Dante ananipiga. Na hana huruma nami tena. Na bado ninaumwa”
Kenan alimsikiliza kimya. Alishindwa hata kusema kitu. Alimshika mkono kwa upole.
“Twende. Usijali. Twende tu. Ntakusaidia”
Walipanda gari wakaelekea nyumbani kwa Zaria na Dante. Walipofika, Dante alikua nje anakunywa bia kwenye baraza ya mbele ya nyumba.
Alipowaona, hakushtuka. Alisimama taratibu na kumuangalia Kenan, halafu akamuangalia Zaria, Kisha akaongea kwa sauti ya ukali
“Kenan, karibu ndani. Zaria usiingie ndani, sikutaki ndani kwangu”
Kenan alishtuka. “Unamaanisha nini?”
“Nimesema akae nje”
Zaria aliinamisha kichwa, machozi yakimdondoka. Kenan akamuangalia, akamgusa bega, halafu akaingia ndani.
Huko Ndani, Dante alimkaribisha kana kwamba hakuna tatizo. Akamwambia akae kisha wakaanza mazungumzo direct.
“Mimi nimeamua… sitaki tena kuishi na Zaria”
“Kaka, unamaanisha nini? Mbona mlikua mnapendana sana? Na unaijua hata hali yake kiafya?” Kenan alimwangalia kwa mshangao😳
“Najua. Anasumbuliwa na ugonjwa wa kichwa. Lakini sioni sababu ya kubeba mzigo wa mtu aliyekaribia kufa. Siwezi”
“Dante… una akili kweli wewe? Huyo ni mkeo. Mkeo wa ndoa. Mmeishi naye miaka mitatu”
“nimechoka bhana! Unadhani kumhudumia mtu anae karibia kufa ni rahisi?? Alafu nina mwanamke mwingine yupo tayari kuchukua nafasi yake”
Kenan alifura kwa hasira. “Nani huyo?” 😡
“Hilo halikuhusu.”
“Dante, huu ni ukatili. Mtu ambaye amekupenda hivi, amekulea, amevumilia hadi sasa, leo unamtupa kama takataka? Unajua anavyoumia?”
“Nimempa kila kitu. Nimemjali kwa wiki nyingi sasa. Lakini sasa basi. Huyu hawezi tena kuwa mke. Anasubiri kufa. Aondoke”
Kenan alinyamaza kwa sekunde chache, akavuta pumzi. “Unachokifanya sio sahihi, kaka”
Dante hakujibu. Alisimama na kwenda chumbani. Dakika mbili baadaye akarudi na sanduku la nguo za Zaria mikononi. Akamkabidhi Kenan.
“Chukua. Na hii hapa ni mfuko wa dawa zake. Usimrudishe tena hapa! Simtaki”
Kenan alichukua vitu hivyo bila kusema chochote. Akatoka nje. Zaria alipomuona akitoka na sanduku lake, alianguka chini kwa huzuni. Alijua huo ndio mwisho wa ndoa yake.
Kenan aliweka vitu kwenye gari. Kisha akarudi na kumsogelea Zaria. Bila kusema kitu, alimwinua taratibu na kumbeba hadi kwenye gari. Alimfungulia mlango wa mbele, akamkalisha kwa upole.
Zaria aliangalia upande mwingine akilia kimya kimya. Alikua ameumia, si tu kwa kipigo, bali kwa kuachwa kama hana thamani.
Kenan alijikuta akimuangalia sana. Moyo wake ulijaa huruma. Hakua amewahi kumuangalia shemeji yake namna ile. Lakini leo, alipomwona vile alivyojeruhiwa, macho yakiwa mekundu, akitetemeka, roho ili muuma💔.
Alipomkumbatia kumtuliza, Zaria aliweka kichwa chake kifuani mwa Kenan. Mwili wake ulikua laini, wa joto, na mwepesi. Kenan alihisi kitu tofauti. Kwa mara ya kwanza, alihisi msisimko wa ajabu. Akiwa bado amemkumbatia, alihisi kitu ndani ya mwili wake kikitembea. Alihisi kitu ambacho hapaswi kuhisi. Alishtuka, akaachia kumbatio taratibu.
“Pole sana, Zaria, Tutapambana pamoja. Usiogope.” Alisema kwa sauti ya chini
Zaria aligeuka na kumuangalia, machozi yakiwa yamejaa. “Asante Kenan. Sijui ningefanya nini leo kama usingekuja.”
Kenan alishika usukani na kuondoka taratibu. Hakujua aende wapi. Lakini alijua kitu kimoja tu, kuwa Zaria sasa ni jukumu lake.
Je nini kitaendelea??
Nakuja……..
SEHEMU YA : 03
Kenan hakuwa na mahali pengine pa kumpeleka Zaria isipokuwa nyumbani kwake. Hakuwa tayari kumpeleka kwa ndugu zake kwa sababu hakutaka kueneza habari.
Pia, hakutaka kumpeleka kwa rafiki mwingine yeyote kwa sababu hakuwa na hakika nani angemwelewa. Jambo la haraka aliloweza kufanya ni kumpeleka kwake, hata kama mke wake, Alisha, hakuwepo mda huo.
Walipofika, Kenan alipaki gari na kumfungulia Zaria mlango. “Karibu nyumbani, Zaria. Usiogope, utakuwa salama hapa” alisema kwa sauti ya utulivu.
Zaria alishuka kwa shida. Mwili wake ulikuwa umechoka. Alikuwa hajala vizuri siku kadhaa, na kichwa kilikuwa kinamuuma. Kenan alimshika mkono na kumwingiza ndani.
“Pumzika hapa sebuleni, nikuandalie juice. Halafu nitakuonyesha chumba cha wageni ambako utalala”
Zaria aliketi kwenye kochi. Nyumba ya Kenan ilikuwa kubwa, safi na tulivu. Ilikuwa na harufu nzuri ya dawa ya kusafishia sakafu na maua ya plastiki ya mapambo.Kenan alirudi na glass ya juice ya embe.
“Kunywa hii kwanza.”
Zaria alikunywa polepole. Baada ya hapo Kenan alisimama na kusema, “Nakupeleka chumbani sasa. Utakuwa unatumia hiki chumba kwa muda wote utakaohitaji”
Waliingia kwenye chumba cha wageni. Kitanda kilikuwa kimetandikwa vizuri, kulikuwa na kabati dogo, meza ya pembeni na taa ndogo. Kulikuwa pia na taulo safi na sabuni bafuni.
“Naomba uoge, ubadili nguo. Nitakuletea chakula baada ya muda mfupi” Kenan alisema kwa upole na kuondoka.
Zaria akaoga kwa muda mrefu. Maji ya moto yalikuwa tiba kwa mwili wake uliokuwa na maumivu. Alipotoka, alivaa nguo safi ambazo Kenan alimpatia, t-shirt nyeupe na suruali ya kulalia.
Baada ya hapo, alikaa kitandani na kuchukua simu yake. Alijaribu tena kupiga namba ya Dante, lakini aligundua kuwa amesha mblock. Aliangalia simu kwa muda, halafu akaweka chini na kushusha pumzi ndefu. Macho yake yakaanza kujaa machozi.
Wakati bado yuko chumbani, Kenan aligonga mlango.
“Zaria, chakula kipo tayari. Njoo tule pamoja mezani.”
Zaria alifuta machozi na kufungua mlango. “Asante Kenan. Nashukuru sana”
Walikaa mezani sebuleni. Chakula kilikuwa wali mweupe na mchuzi wa samaki. Kulikuwa pia na kachumbari pembeni.
“Umepika wewe mwenyewe?” Zaria aliuliza.
Kenan alicheka kidogo. “Ndio. Sijui kama ni kitamu lakini nimejitahidi”
“Ni kizuri” Zaria alisema huku akiweka samaki kidogo mdomoni.
Baada ya muda mfupi, Zaria akauliza kwa sauti ya chini, “Kenan… Alisha yuko wapi?”
Kenan alikaa kimya kwa sekunde chache. Alionekana kutafakari kabla ya kujibu.
“Yuko dukani kwake, Alikwenda kufunga mizigo ya wateja” alijibu
Zaria alitazama sura ya Kenan kwa muda. Alijua kwamba Kenan hajui Alisha yuko wapi. Alitaka kumwuliza zaidi lakini akajizuia. Hakutaka kuonekana anachunguza ndoa ya watu.
Baada ya kula, Kenan alimletea Zaria mfuko wake wa dawa.
“Hizi ndio dawa zako, unakumbuka dozi?”
“Ndio. Asante”
Zaria alimeza dawa hizo pale pale. Baada ya dakika chache, alianza kuhisi uzito mkubwa wa usingizi. Dawa hizo kila siku zilimpa hali ya kulegea mwili na usingizi mzito.
Walipokuwa wanatazama runinga pamoja sebuleni, macho ya Zaria yalizidi kuwa mazito. Aliinamia bega la Kenan bila kujua. Muda mfupi baadaye, alikua amelala kabisa. Hakuweza hata kufumbua macho, wala kujua kinachoendelea.
Kenan aligeuka na kumwangalia. Zaria alikuwa amelala kwa utulivu. Alikuwa mrembo. Nywele zake zilikuwa zimelala vizuri upande mmoja. Uso wake ulikuwa na amani, lakini alama za majeraha zilibaki kwenye mashavu yake.
Kenan alihisi kitu moyoni. Alishangaa jinsi alivyoanza kumuonea Zaria huruma. Kila alivyomtazama, moyo wake ulizidi kumuumia. Lakini pia, ndani kabisa, kulikuwa na hisia tofauti alizojitahidi kuzipuuza. Mwili wake ulianza kuwa na joto. Akashtuka.
Akasimama na kumbeba Zaria mikononi mwake, kwa upole kama mtoto mdogo. Akampeleka hadi chumbani kwa wageni. Akamuweka kitandani, kisha akamfunika kwa shuka.
Alisimama sekunde chache akimtazama. Alitaka kusema kitu, lakini alijizuia. Haraka akageuka na kutoka mle chumbani mbio. Akaenda kukaa sebuleni, akiwa amechanganyikiwa.
Zaria alilala kwa muda mrefu sana. Dawa zilimchosha mwili. Alipoamka, saa ya ukutani chumbani ilisoma saa 6:00 usiku. Alikaa kitandani kwa muda akijiuliza ni alifikaje chumbani.
Dakika chache baadaye, alisikia mlango wa mbele ukifunguliwa. Kisha sauti ya gari likizimwa. Alisha alikuwa amerudi.
Zaria alisikiliza kwa makini. Alisikia mlango wa sebule ukifunguliwa kwa nguvu, kisha hatua za haraka zilisikika huku Ikifuatia sauti ya Kenan.
“Ulikuwa wapi hadi saa sita usiku?”
Alisha alijibu kwa sauti ya dharau. “Nilikuwa dukani, nimekwambia. Kuna mizigo ya wateja tulikua tunapakia”
“Unafikiri mimi ni mtoto? Duka lako limeshafilisika. Unacheza kamari kila siku. Hicho ndicho kilikufanya uchelewe, si ndio?”
Alisha alicheka. “Unajua nini Kenan? Hujanielewa kabisa. Si kila kitu ni kamari.”
“Usinifanye mjinga. Nimevumilia sana. Unadhani sikujua unafanya nini?”
“Hata kama nafanya, utaniambia nini? Wewe mwenyewe si mkamilifu. Kuna kipindi ulikua hutoki hata ofisini ukarudi nyumbani mapema. Kila mtu ana mapungufu yake”
Kenan alionekana kukasirika zaidi. “Sawa. Kama huna heshima, basi ujue kuna mtu mwingine sasa ataishi hapa”
Alisha alikaa kimya kwa muda mfupi. “Mtu gani?”
“Zaria yupo chumbani. Atakuwa anaishi nasi kwa muda.”
Zaria alishikwa na mshituko aliposikia hayo. Alitega sikio zaidi ili asikie zaidi.
Ila kwa Alisha hakushangaa. Badala yake, alitabasamu kidogo. Tabasamu la ajabu, kama mtu anayefurahia jambo fulani.
“Sawa” Alisha alijibu kwa sauti ya kawaida. “Hakuna shida”
Kenan hakumwona akitabasamu. Alikuwa ameenda jikoni kuchukua maji. Alisha alibaki sebuleni akionyesha kuna kitu alificha moyoni.
Je nini kitaendelea?
Nakuja………
SEHEMU YA : 04
Asubuhi ya siku iliyofuata, Kenan aliamka mapema sana. Alikuwa hajalala vizuri usiku. Mawazo kuhusu Zaria yalikuwa yamemjaa kichwani. Hakuelewa kabisa kwa nini alikuwa anahisi hivyo.
Alijua kabisa Zaria ni mke wa rafiki yake, na zaidi ya hapo, alikuwa mgonjwa. Lakini kila alivyomwangalia, alihisi kitu tofauti huruma, uchungu, na kwa namna fulani, ukaribu usio wa kawaida.
Alipofika jikoni, alianza kupika chai. Alichemsha maziwa, akaandaa mkate wa siagi na mayai ya kuchemsha. Alipomaliza, aliweka kila kitu mezani, kisha akapumua kwa nguvu. Hakujua hata kwanini aliamka kumuandalia Zaria chai.
Alirudi chumbani kwake kujiandaa kwa ajili ya kwenda kazini. Kama kawaida, Alisha alikuwa bado amelala. Hakuwahi hata siku moja kuamka kumpikia chai au kumuandalia nguo. Kenan alikuwa ameshazoea kufanya kila kitu mwenyewe.
Baada ya kuvaa suti yake na kubeba begi lake, alimsogelea Alisha kitandani na kumnong’oneza, “Leo tafadhali baki nyumbani. Zaria atakuwa mpweke sana. Hakikisha pia unanunua mahitaji ya ndani, sabuni, unga, na juisi. Pesa nimeweka mezani”
Alisha hakujibu. Aligeuka tu upande mwingine, akaendelea kulala. Kenan alitoka chumbani, akiwa ameshika funguo za gari. Alielekea kwenye chumba cha wageni alipomuweka Zaria. Aligonga mlango taratibu.
“Zaria… ni mimi, Kenan.”
Zaria alikuwa tayari macho. Alikuwa amelala kidogo tu, kisha akaamka mapema na kushindwa kulala tena. Alikaa kitandani muda wote akitazama picha kwenye simu yake, picha za yeye na Dante walipokuwa kwenye furaha yao.
Alikuwa analia kimya kimya, machozi yakimwagika bila sauti. Alipomsikia Kenan akigonga mlango, alifuta machozi haraka.Alienda kufungua mlango.
Alipokutana na Kenan, macho yao yaligongana kwa muda mfupi. Kenan aliona kabisa macho yake yamevimba kwa kilio.
“Chai iko tayari mezani, Kunywa, halafu usisahau kunywa dawa. Pia tafadhali usilie tena. Leo nikitoka kazini ntakwenda kuongea na Dante. Nitajaribu kuongea naye, labda abadilike” Kenan alisema kwa upole.
Zaria alitikisa kichwa taratibu. “Asante sana Kenan. Nitajitahidi kuwa sawa”
Kenan alitabasamu kidogo, akamwangalia kwa sekunde chache, kisha akageuka na kuondoka. Aliondoka kwenda kazini, moyo wake ukiwa mzito.
Baada ya Kenan kuondoka, Zaria alijilazimisha kutoka chumbani. Alikwenda mezani na kuanza kunywa chai aliyo andaliwa na Kenan.
Alikula polepole, hakuwa na hamu ya kula lakini alijua lazima apate kitu tumboni ili dawa zifanye kazi. Alipomaliza, alimeza dawa zake, kisha akaenda kukaa sebuleni kutazama Tv ili kuondoa mawazo.
Ilipofika saa nne asubuhi, Alisha aliamka. Alitoka chumbani akiwa amevaa dera refu la nyumbani, nywele zake zikiwa bado zimevurugika. Alipoingia sebuleni, alimkuta Zaria amekaa kwenye kochi, akiwa anatizama movie.
“Habari ya asubuhi” Alisha alisema kwa sauti ya kawaida.
“Nzuri,” Zaria alijibu kwa sauti ya adabu. “Na wewe je?”
“Salama tu” Alisha alikaa kwenye kochi jingine. “Pole kwa yaliyokupata”
“Asante” Zaria alisema, macho yake yakishuka chini. Alikaa kimya kwa sekunde chache, kisha akasema kwa sauti ya chini
“Siwezi kuamini kuwa Dante amebadilika kiasi hiki. Wakati mwingine najihisi kama niko kwenye ndoto mbaya”
“Umevumilia sana. Lakini pole, dunia imejaa watu wa aina tofauti. Kuna wanaume hawajui thamani ya kile walicho nacho hadi wakipoteze” Alisha alisema.
Zaria aliuliza kwa taratibu. “Utani ruhusu niweze kuishi hapa kwa mda?? Kenan amekubali ila sikukuomba wewe na mimi sina pengine kwa kwenda”
“Bila shaka. Siwezi kukufukuza. Ukiona bado hujajisikia kwenda mahali pengine, unaweza kubaki kadri unavyojisikia. Hapa ni nyumbani pia”
Zaria alitabasamu kwa mara ya kwanza tangu afike. “Asante Alisha. Asante sana kwa moyo huu”
“Usijali. Tupo pamoja” Alisha alisema kisha akasimama. “Ngoja nirudi chumbani nijitayarishe nataka kutoka”
“Sawa” Zaria alibaki sebuleni, moyo wake ukiwa umepoa kidogo. Alijaribu kuangalia movie, lakini akili yake ilikuwa bado kwa Dante.
Wakati huo, Alisha akiwa chumbani kwake, alijitayarisha haraka sana. Alivaa nguo nzuri, akajipulizia manukato ya bei ghali, akachukua pochi yake na kutoka.
Hakusema chochote kwa Zaria alipompita sebuleni. Alitembea kwa haraka kana kwamba ana mahali pa muhimu sana pa kwenda.
Muda huo huo, huko kwa Dante, hali ilikuwa tofauti.
Dante alikuwa nyumbani siku hiyo. Alikuwa na kazi ya kuandaa ripoti ya biashara kwenye laptop yake.
Alikaa kwenye meza ya kulia chakula akitumia saa nyingi kuandika na kufanya hesabu. Alikuwa peke yake, nyumba ikiwa kimya kabisa.
Ghafla, mlango wa mbele uligongwa. Dante alisimama na kwenda kuufungua. Alipoufungua, alimshtuka kumuona Alisha. Walipoangaliana, walitabasamu😊.
“Umefika saa ngapi??” Dante aliuliza.
“Mda sio mrefu, Nimeku miss” Alisha alijibu kwa sauti ya utundu.
Bila kusema kitu kingine, walikumbatiana kwa nguvu. Kisha wakaanza kubusiana mfululizo, wakipapasana kama watu waliomissiana sana. Dante alibeba pochi ya Alisha na kuiweka sebuleni, halafu akamkokota hadi chumbani kwake.
Waliingia chumbani na kufunga mlango. Walijirusha kitandani na kuanza kushiriki tendo la ndoa kwa mahaba makali, wakicheka, wakilia, wakigusa kila sehemu ya miili yao. Walionekana kufurahia kila dakika waliyo nayo pamoja.
Alisha alikuwa mwanamke aliyemvutia sana Dante. Hili halikuanza leo.
Penzi lao lilianza miaka mingi iliyopita walipokuwa chuoni. Walikuwa wapenzi wa ukweli. Waliwahi kuahidi kuoana, lakini bahati haikuwa upande wao. Dante alipata nafasi ya kwenda kusoma Uingereza. Wakati anasafiri, walikubaliana watavumiliana hadi atakaporudi.
Lakini akiwa Uingereza, Dante alisikia taarifa kuwa Alisha ana uhusiano na mwanaume anayeitwa Paul. Hilo lilimvunjia moyo.
Aliumia sana. Hakuwahi kumsamehe moja kwa moja. Ili kujitoa kwenye uchungu, ndipo alipoanza mahusiano na Zaria.Zaria alikuwa mpole, mrembo, na muelewa. Walipendana kwa kasi. Na baada ya miezi michache, walifunga ndoa.
Lakini miaka miwili baada ya ndoa, Alisha alijitokeza tena. Alikuja na machozi, akaomba msamaha. Alisema alikosea, na bado anampenda Dante. Alisha alisema uhusiano wake na Paul ulikuwa ni wa muda mfupi, hakuwa na mapenzi ya kweli kama alivyokuwa na Dante.
Dante alijikuta anaingia tena kwenye mtego wake wa zamani. Penzi likarudi. Wakaanza kuonana kisiri.
Wakati mwingine walikutana hotelini, wakati mwingine ofisini kwa Dante.
Lakini Dante hakutaka Alisha awe mbali naye. Alishindwa kumpa nafasi rasmi kwenye maisha yake kwa sababu tayari alikuwa ameoa. Lakini pia hakutaka ampoteze tena.
Hapo ndipo alipokuja na mpango wa kumtambulisha kwa rafiki yake mkubwa, Kenan. Alimshawishi Kenan kuwa Alisha ni mwanamke mzuri, mwenye tabia nzuri, anayefaa kuwa mke. Kenan bila kujua chochote, alikubali.
Walianza mahusiano, na baadaye walifunga ndoa.
Tangu siku hiyo, Alisha akawa karibu sana na Dante bila yoyote kujua. Waliendelea kuwa wapenzi kisiri. Kila walipokutana, walifanya kila kitu kana kwamba hawakuwahi kuachana.
Na sasa, walipokuwa kitandani wakikumbatiana, hakuna kati yao aliyefikiria kama wanafanya kosa. Kwao, ilikuwa ni furaha waliyoikosa kwa muda mrefu.
Je nini kitaendelea??
Nakuja……..
SEHEMU YA : 05
Mda huo Kenan alikuwa ofisini lakini akili yake haikuwa kwenye kazi. Kila mara alikua anafungua faili, anasoma ukurasa mmoja halafu anaufunga.
Alijaribu kufanya kazi lakini hakukusanya akili kabisa. Mawazo yake yote yalikuwa kwa Zaria. Alivyomuacha asubuhi, akiwa mpweke, akitoka kwenye ndoa yenye maumivu, ilimchosha sana akili.
“Lazima niongee na Dante leo” Kenan alijisemea.
Alifuta kila ratiba iliyokuwa mbele yake. Mikutano, miadi, kila kitu. Kisha akampigia simu secretary wa Dante kujua kama yupo ofisini.
Lakini secretary alimjibu kwa sauti ya kawaida, “Dante hajafika leo kazini, anafanyia kazi nyumbani”
Kenan hakuuliza zaidi. Alikatisha simu na kuchukua funguo zake. Aliondoka moja kwa moja kuelekea nyumbani kwa Dante. Hakuwa na muda wa kupoteza.
Wakati huo huo, kwa upande wa Dante, alikuwa amelala kitandani akiwa na Alisha. Walikuwa wamejifunika shuka moja, wakiwa wametulia na kuchoka baada ya mapenzi marefu na mazito. Walikuwa kwenye kitanda kile kile ambacho Zaria alikua akilala. Hakuna hata mmoja aliyekuwa na hisia za hatia kwa walichokifanya.
Ghafla mlango wa nje uligongwa. Dante alishtuka. Aliruka kutoka kitandani kwa haraka, akachukua kaptula ya ndani na kuivaa. Akatembea haraka hadi mlangoni. Moyo wake ulianza kumdunda kwa kasi. Alihisi labda wamefumaniwa.
Alipofungua mlango, alishtuka zaidi. “Kenan?” 😳
Kenan alimsogelea bila hata salamu ya kawaida. “Naomba niingie”
Dante alionekana kuchanganyikiwa. “Eh… ndio… ingia.”
Kenan aliingia. Macho yake mara moja yakatua kwenye pochi ya kike iliyokuwa juu ya kochi. Pochi kubwa ya rangi ya pinki, wazi kabisa ilikuwa si ya Zaria.
Hakuwa amewahi kuiona hapo kabla. Alinyamaza, lakini moyoni alihisi kitu kibaya. Pengine angeijua ile pochi angeweza kutambua ni mkewe aliekua kule ndani.
“Kwahiyo Zaria ameondoka jana, na leo tayari umeleta mwanamke mwingine?” Kenan aliuliza kwa sauti ya chini lakini kali.
Dante alijikaza. “Huyu wa sasa nampenda zaidi ya Zaria. Zaria si mtu wa aina yangu”
Kenan alitikisa kichwa. “Unajua unakosea sana. Sawa, ndoa huwa zina changamoto, lakini unayemfanyia haya ni mke wako wa ndoa. Mwanamke aliyekupenda bila masharti”
“Kenan, naomba niseme tu ukweli. Nimechoka na Zaria. Nataka niandike talaka mapema. Sitaki hata kubaki naye”
Kenan alimuangalia kwa maumivu. “Na Zaria ataenda wapi? Yule mwanamke amebakisha miezi michache ya kuishi. Unafikiri ni sawa kumtupa mtaani?”
“Kama ataishi kwako, bora. Si unampenda na unamjali kuliko mimi? Aishi kwako basi”Dante alisema kwa sauti ya kejeli.
Kenan alijikaza asimrukie kwa hasira. Alijua Dante hajui analosema. Aliishia kuinuka kwa haraka na kusema,
“Utaumia kwa haya unayofanya. Utajutia” Kisha akatoka nje na kufunga mlango kwa nguvu.
Dante alishusha pumzi ndefu maana ilibaki nusu wafumwe. Na Alisha akiwa kajifunga shuka alikua kajibanza nyuma ya mlango wa chumbani jasho likimtoka.
Kenan aliamua kurudi nyumbani moja kwa moja. Alikuwa na hasira nyingi. Alipoingia, alikuta Zaria amelala kwenye kochi. Alikuwa hajala. Mezani palikuwa hapana hata kikombe, wala sahani. Alisha hakuwepo kabisa. Hii ilimaanisha Zaria alishinda njaa. Kenan aliumia zaidi💔.
Aliingiza mkono mfukoni akachukua simu na kumpigia Alisha. Simu iliita lakini haikupokelewa. Aliipiga tena mara mbili, bado haikupokelewa. Akamsogelea Zaria taratibu na kumgusa bega.
“Zaria… samahani, samahani sana.”
Zaria alifumbua macho taratibu. “Kuna nini?”
“Pole kwa kushinda njaa. Nilidhani Alisha angekusaidia leo, lakini hajafanya chochote. Tafadhali, jiandae. Twende tukale mahali. Sitaki uendelee kukaa hapa ukiteseka na njaa”
Zaria alitaka kukataa lakini alipomuona Kenan alivyojaa huruma usoni, alinyamaza. “Sawa, ngoja nijitayarishe”
Alienda chumbani na kuvaa moja ya magauni aliyobeba kwenye sanduku lake. Gauni jekundu, refu linalo bana vizuri umbo lake. Hilo gauni alilinunuliwa na Dante siku ya maadhimisho ya ndoa yao ya kwanza.
Alipotoka chumbani, Kenan alipigwa butwaa. Alisimama muda mfupi bila kusema. Kisha akapiga hatua mbili mbele, akatabasamu.
“Wow…umependeza sana. Gauni hilo linakufaa sana.”
Zaria alijikuta anatabasamu. “Asante.”
Kenan alishindwa kuvumilia. “Kuna kitu cha ukweli nataka nikwambie, Zaria. Wewe ni mwanamke mzuri sana. Yaani mtu yeyote anayekupoteza, anakosea sana”
Zaria alitabasamu kidogo. “Nashukuru Kenan. Umenifanya nijisikie vizuri leo”
Walitoka wote, wakaelekea kwenye mgahawa mmoja wa utulivu mjini. Walikaa sehemu ya juu ya jengo, pembeni mwa dirisha lenye mandhari ya barabara kuu.
Waliagiza chakula, Zaria alichukua wali wa nazi na samaki wa kukaanga, Kenan akachukua chipsi na mishkaki. Waliongea mengi. Wakatabasamu. Kwa mara ya kwanza tangu matatizo yaanze, Zaria alicheka.
Wakati huo, kwa upande wa Dante na Alisha, walikuwa bado chumbani. Walikuwa wamevaa, wamekaa kitandani wakizungumza.
“Leo tumeponea chupuchupu” Alisha alisema kwa sauti ya uoga
Dante alitikisa kichwa. “Kenan amekuja bila taarifa nusu atugundue. Lakini bado hajui kuwa mke wake ni mwanamke ninayempenda”
Alisha alicheka kidogo, akamgusa begani. “Tuliwahi kuwa na penzi la ajabu sana. Siwezi kuacha kukupenda, hata nikijitahidi kujizuia”
Dante akashika mkono wake. “Sina haja ya kujificha tena. Niko tayari kumpa talaka Zaria Maana Ndoa yako na Kenan haina maana kama moyo wako uko kwangu”
Alisha alionekana kushangaa. “Unamaanisha kweli?”
“Ndio. Sitaki kujibana bana tena. Zaria hayupo moyoni, Ni wewe ninayekupenda”
Alisha alinyamaza kwa muda mfupi, akamwangalia kwa makini. “Na Kenan je?”
“Kenan ataumia, lakini hayo ni maisha. Mapenzi hayaangalii historia! Tutaongea nae ataelewa”
Alisha alitabasamu. “Basi kama ni hivyo… tutaendelea kushirikiana mpaka mwisho”
Kitu ambacho Dante alisahau ni huwezi kumtoa mtu moyoni kirahisi namna iyo. Japo alidai hampendi Zaria ila bado alikua moyoni ingawa hakulijua ilo sababu ya penzi lake kwa Alisha.
Je nini kitaendelea?
Nakuja……….
SOMA MAELEKEZO
Bonyeza hi "Soma Kitabu" kisha itakupeleka kwenye fomu yaku login, hakikisha ume login na namba uliyojiunga nayo ndipo utaendelea sasa kusoma kitabu chote