Mimi ni Samira Said. Msichana wa kawaida niliyekulia Morogoro—nikiwa na ndoto nyingi na uwezo mdogo wa kuzitimiza. Nilikuwa na umri wa miaka 23 tu, moyo wangu ukiwa bado na makovu ya kuachwa na mchumba niliyempenda kwa miaka mitano. Nilikuwa nimevunjika, nimekata tamaa, na nilihitaji mwanzo mpya.
Ndipo nikaingia kwenye ulimwengu wa mitandao ya kijamii—TikTok, Instagram—nikianza kushare maisha yangu ya kawaida, mavazi ya bei rahisi, tabasamu la kutunga, na matumaini yaliyofichwa nyuma ya video fupi. Watu wakaanza kuniona. Wakaanza kunifollow. Na ndipo alipoingia Jay Mo.
Alikuwa mwanaume wa ndoto: mwenye picha za kuvutia, sauti ya staha, na uwezo wa kifedha. Hakuwahi kuniomba chochote. Alinitia moyo, akanitumia pesa, akanilipa ada ya chuo, na kunifanya nijisikie kama malkia. Kila siku iliyonisogeza karibu naye, nilihisi kama maisha yangu yanabadilika kwa neema ya ajabu. Tulikubaliana tukutane Dar es Salaam kwa mara ya kwanza...
Nawaza kama nisingefungua akaunti ya tiktok na Instagram ningesalimika na makucha haya. Au nisingeshikwa na tamaa ya Maisha mazuri ya jiji la dar es salaam huenda ningenusurika na janga hili. Endelea kusoma hadithi hii kujua Zaidi kisa na mkasa uliomkuta samira na mapenzi ya mtadaoni…
PENZI LA MTANDAONI
Sura ya 1:
Jua lilikuwa linazama polepole nyuma ya milima ya Uluguru, likiacha kivuli cha dhahabu juu ya nyumba za tope na bati zilizopitwa na wakati. Samira alisimama mbele ya dirisha la chumba chake kidogo, akitazama anga kwa macho yaliyojaa huzuni. Siku hii haikuwa ya kawaida kwake. Ilikuwa siku ambayo rasmi, alithibitisha kuwa mtu aliyempenda kwa miaka mitano hakuwa wake tena.
“Niishie hapa, Samira. Sina tena cha kukupa. Maisha yamebadilika,” ndivyo ujumbe wa mwisho wa Faheem ulivyosoma. Mchumba wake wa zamani, mtu aliyemfanya aamini kuwa upendo wa kweli upo, alikuwa amemaliza kila kitu kwa maneno machache tu kwenye WhatsApp. Hakuna maelezo, hakuna huruma—tu ukatili wa kweli wa mapenzi ya kisasa.
Aliusoma ujumbe huo kwa mara ya kumi na moja, kila mara akihisi kama moyo wake unadungwa sindano za baridi. Faheem alikuwa sehemu ya maisha yake—aliwahi kumwambia ndoto zake, mapungufu yake, na hata zile siri ambazo hakuwahi kumweleza mtu mwingine yeyote. Na sasa, yuko peke yake.
“Basi,” alijisemea kwa sauti ya chini, machozi yakianza kumtiririka taratibu. “Hiki siyo mwisho wangu.”
Alichepua machozi na kuchukua daftari lake la zamani lililokuwa na orodha ya malengo aliyokuwa nayo alipokuwa kidato cha nne. Moja ya malengo hayo lilikuwa: Kuwa mwanamke huru na mwenye mafanikio.
Samira alikuwa na miaka 23 sasa. Hakuwa na kazi rasmi. Alikuwa bado anapambana kulipa ada ya chuo kwa msaada wa mama yake mdogo, aliyekuwa akifanya kazi kama nesi Arusha. Lakini alikuwa na kitu kimoja—ndoto. Na leo, ndoto hiyo ilikuwa imechochewa na huzuni. Alijua kuna kitu kipya kinahitaji kuanza.
Alishika simu yake ya TECNO Spark 7, iliyojaa nyufa kwenye kona, na kufungua TikTok. Hapo awali alikuwa na akaunti ya kuangalia tu video za watu wengine. Lakini sasa, kitu ndani yake kilimwambia: Nianze kushare maisha yangu. Nianze upya.
Akaandika jina la akaunti mpya: @MremboWaMorogoro. Akaweka picha ya profaili aliyopiga akiwa kwenye bustani ya Man’yanya. Mavazi yake yalikuwa rahisi—gauni ya mitumba ya rangi ya waridi aliyoinunua kwa elfu tatu sokoni—lakini sura yake ilionyesha uzuri wa asili, tabasamu la kweli, na macho ya msichana aliyejeruhiwa lakini bado anasimama.
“Maisha ya mrembo maskini. Hakuna filters. Hakuna uongo,” aliandika kwenye bio ya akaunti hiyo.
Siku hiyo hiyo alianza kupost video ya kwanza: akionyesha namna alivyochagua outfit nzuri ya elfu tano kwa ajili ya kuenda chuoni. Alitumia muziki wa Afrobeat unaopendwa sana, akachanganya na ucheshi wa Morogoro wenye lafudhi laini. Haikupita saa moja, video ilikuwa na likes mia tatu. Saa mbili baadaye, followers walikuwa elfu moja.
Alishangaa.
“Imeanzaje kuenea hivi haraka?” aliuliza kwa mshangao huku aki-refresh tena na tena.
Ujumbe wa kwanza DM uliingia kutoka kwa msichana wa Dar es Salaam:
“Wewe ni mrembo sana! Naomba ujifunze kutoa tips za fashion.”
Samira alicheka kidogo—hisia mpya, za furaha kidogo, zilianza kuchukua nafasi ya maumivu aliyokuwa nayo asubuhi. Alijibu kwa upole na mshangao, “Asante mrembo. Nitafanya hivyo.”
Ndipo DM ya pili ikaja. Na hii ilibadilisha kila kitu.
Jina: Jay Mo
Profaili: Mwanaume mrefu, mweusi mwenye uso wa kujihami, akiwa na suti za gharama na magari ya kifahari nyuma yake. Verified account.
Ujumbe:
“Samira… una uzuri wa kipekee. Nimeangalia video zako zote. Una kitu cha pekee. Naomba tukutane someday, but for now, naomba nikufahamu zaidi.”
Moyo wa Samira uliruka kidogo. Alijishika kifua.
“Who is this?” aliuliza kimoyomoyo, macho yake yakikodolea picha ya Jay Mo.
Alicheki tena akaunti yake. Followers 150k. Picha za Dubai, Zanzibar, na Dar zilikuwa kila kona. Picha zote zilikua hazina sura yake labda aoneshe mgongo tyu au mkono tu.
Lakini alikumbuka alivyotapeliwa na mapenzi. Alitaka kuwa makini.
Akamjibu kwa busara:
“Asante kwa ujumbe wako mzuri. Sina hakika kama niko tayari kwa kitu chochote cha mapenzi sasa, lakini naweza kuzungumza.”
Jay Mo alijibu ndani ya dakika mbili:
“Fair enough. Sitaki kukulazimisha. Naanza kama rafiki.”
Rafiki.
Neno dogo lenye maana kubwa.
Na kwa Samira, hiyo ndiyo ilikuwa tiketi ya safari ya maisha mapya.
PENZI LA MTANDAONI
Sura ya 2:
Siku iliyofuata ilikuwa ya jua kali Morogoro, lakini ndani ya mabweni ya chuo kikuu cha Elimu na Maendeleo ya Jamii, hewa ilikuwa nzito. Samira alikuwa ameamka mapema, akaoga kwa maji ya baridi aliyoyachemsha kwa jiko la mkaa usiku, kisha kuvaa dera lake la pinki lililofifia rangi na viatu vya raba vya zamani.
Alipojitazama kwenye kioo kidogo cha plastiki kilichopasuka upande mmoja, alitabasamu kwa shida.
“Wewe ni mzuri,” alijisemea kimoyomoyo, akijipa nguvu.
Aliweka poda ya bei rahisi usoni, akanyoa nyusi kidogo kwa wembe, kisha akaweka hereni zake za plastiki alizozinunua kwa buku tano Kariakoo mwaka jana. Alikuwa tayari kwenda chuoni—siyo tu kusoma, bali pia kupambana na dunia ya vionjo, fasheni na presha ya maisha ya mtaani.
Darasa lilikuwa limejaa wanafunzi waliokuwa busy kujiandaa na mitihani ya mwisho wa muhula. Samira alikaa kwenye benchi ya pili upande wa kushoto, karibu na dirisha. Lakini alihisi macho mengi yakiangalia upande wake—hasa kutoka kwa marafiki zake wa karibu: Lisa na Natalie.
Lisa alikuwa mweupe, mrefu, mwenye midomo ya pinki iliyopakwa vizuri, na nywele zake zilikuwa zimetengenezwa kwa staili ya twist ya gharama. Mavazi yake yalikuwa ya kisasa—crop top ya fashion nova na suruali ya jeans ya kuchanika kwenye mapaja. Natalie, upande mwingine, alikuwa mweusi mwenye muonekano wa ‘model’, na alivalia jumpsuit nyeusi iliyombana mwilini kama gloves.
“Sammy!” Natalie alimuita huku akimpungia mkono. “Njoo hapa mami. Tunakupigia story za mitihani.”
Samira alinyanyuka kwa aibu kidogo na kukaa nao. Alijua kabisa walikuwa kwenye ligi nyingine. Mavazi yao, simu zao, na hata vipodozi vyao vilikuwa vinamzidi mara kumi. Lakini walikuwa marafiki—hata kama kwa nyakati nyingine alihisi kama wa kuchezea.
“Habari ya asubuhi?” Samira aliuliza, akijitahidi kuonekana mwenye furaha.
“Poaaa!” Lisa alijibu huku akimpiga busu wa hewani. “Lakini Sammy, mbona siku hizi umepotea? Hata status zako zimepoa.”
Samira alicheka kwa kujifanya. “Yaani mnaona mpaka status? Aisee, nimekuwa busy na assignments.”
Natalie alimkazia macho, macho yake yakiwa makini. “Au ni yule mchumba wako? Yule Faheem? Mlikuwa goal sana...”
Samira alipumua kwa kina. Alijua wakati huu utakuja. Hakutaka kulia, wala kuonekana mnyonge. Alijikaza.
“Hapana,” alijibu kwa sauti ya kawaida. “Tumeachana wiki iliyopita.”
Kimya kidogo kilitawala.
Lisa alitua mkono begani mwake. “Ooh pole sana Sammy. Lakini ni bora. Mapenzi hayalipi. Sisi tumeshaamua bana, mwanaume maskini siyo future. Tafuta mwanaume anayeweza kukuweka mjini.”
Natalie aliingilia haraka. “Exactly. Kwani unadhani haya maisha tunayovaa hivi ni kwa salary ya NSSF? Hapana mami. Tunajijua.”
Samira alitabasamu kwa aibu, akitaka kubadili mada, lakini kabla hajasema lolote, Lisa alikaribia kidogo na kunong’ona, lakini kwa sauti iliyosikika vizuri.
“Samira, acha nicheke... Wewe unahangaika na stress za Faheem wakati mimi mwenzio...”
Akatabasamu kwa madaha, kisha akatoa simu yake ya iPhone 13 Pro Max na kuonyesha picha.
“Look... this is James. Mubaba wangu kutoka Dar. Ananipeleka Zanzibar weekend hii. Na hiyo hotel ni Serena.”
Natalie alipiga kelele kidogo. “Eeeeh! Serena tena? Wewe Lisa umefungua njia!”
Lisa alicheka na kujigamba. “Siyo njia tu. Mimi sasa hivi nina allowance ya laki tano kila wiki. Na ameniahidi gari kabla ya mwezi kuisha.”
Samira alimeza mate kwa shida. Hakutaka kuonekana anavutiwa, lakini moyoni alimwambia, Hivi maisha bora hayawezi kupatikana bila mwanaume tajiri? Hata kama hakupenda kuwaza hivyo, ukweli ni kwamba maisha yalikuwa magumu. Mama yake mdogo Arusha alimtumia elfu ishirini tu kwa wiki—pesa ambayo haitoshi hata kununua bundle, chakula na sabuni.
“Jamani... lakini siyo kila mtu atapata mubaba wa Dar,” Samira alisema kwa kucheka. “Wengine tutasubiri bahati ya kuingia Bongo Movie.”
Lisa na Natalie walicheka, lakini Natalie alimtazama Samira kwa makini, kisha akashusha sauti.
“Sammy, kwa upendo wote. Wewe ni mrembo. Una umbo, una uso, na akili zako zipo. Lakini ukiendelea kuogopa mapenzi ya pesa, utabaki kutafuta ada kila semester. Achana na maumivu ya Faheem. Fungua macho. Fursa zipo.”
Lisa alitikisa kichwa kwa kuunga mkono. “Au unangoja nini? Instagram yako inaendelea vizuri. Watu wengi wa Dar wakiona sura yako, lazima wakutake. Usiogope kudate na pesa.”
Samira alitabasamu kwa mashaka. “Nitafikiria.”
Lakini moyoni hakufikiri tu—alihisi shinikizo. Alihisi kama kila msichana sasa alikuwa anapigania maisha kwa mwendo wa mkato. Je, yeye alikuwa mjinga kwa kuamini mapenzi ya kweli bado yapo?
Baada ya kipindi kuisha, Samira alirejea bwenini akiwa na mawazo mengi. Alifungua simu yake na kuingia DM.
Jay Mo alikuwa amemuandikia tena.
“Umeamka vipi mrembo wangu? Ungekuwa karibu, ningekupikia breakfast ya king. Lakini kwa sasa, hebu nijue siku yako ilivyoanza...”
Alishusha pumzi ndefu.
Kisha akamjibu:
“Sijalala vizuri. Leo nimekuwa na siku ya presha chuoni. Na marafiki zangu wananifanya nijihisi masikini. Lakini najitahidi.”
Dakika tatu baadaye, ujumbe mwingine uliingia:
“Samira, wewe siyo masikini. Wewe ni malkia ambaye hajajua taji lake bado. Muda ukifika, nitahakikisha huna tena presha ya ada, chakula au hata pressure ya marafiki. Subiri tu.”
Alifuta machozi kwa kidole gumba. Hakuwa anajua kama ni maneno ya kweli au tamu za mitandaoni. Lakini kwa sasa, moyo wake ulihitaji maneno hayo.
Aliweka simu pembeni, na kwa mara ya kwanza tangu alipoachwa na Faheem, alihisi mwanga mdogo wa tumaini.
PENZI LA MTANDAONI
Sura ya 3:
Saa ilikuwa saa mbili na nusu asubuhi, kengele ya simu ya Samira iliita kwa sauti ya "Sauti Yako" ya Maua Sama — wimbo alioupenda kwa sababu uliongelea mwanamke mwenye ndoto, anayepambana na dunia. Alijinyanyua kutoka kitandani kwa uzito, macho yake yakiwa bado na ukungu wa usingizi wa usiku, na viungo vya mwili wake vikilalamika kutokana na uchovu wa jana.
Aliangalia dirisha lake dogo la mbao, ambapo jua la Morogoro lilikuwa linaanza kupenya kwa aibu. Aliamka, akachukua kibeseni chake na kwenda bafuni kuchota maji ya kuoga. Alijua leo ilikuwa siku ndefu chuoni—kuna presentation ya Sociology saa nne, kisha mid morning test ya Gender and Development saa sita na nusu.
Baada ya kuoga, alirudi chumbani akiwa amebeba chupa ya maji na vipodozi vyake viwili tu: poda ya Elf na lipgloss ya KISS inayomalizika. Alivaa gauni lake jeupe la mistari ya buluu, na kisha kujiangalia kwenye kioo chake kilichopasuka kona. “Hivi ndo nakwenda chuo… kama msomi au housegirl?” alijicheka, kisha akavuta begi lake dogo la mgongoni.
Akiwa tayari, aliketi kitandani kwa dakika tano kabla ya kuondoka. Kama kawaida yake, alifungua DM ya Instagram, akiangalia kama kuna ujumbe mpya kutoka kwa Jay Mo. Na kweli, kulikuwa na moja. Siyo voice note, siyo emoji—ni ujumbe wenye uzito.
📩 “Samira, honestly… I don’t like kutafuta wewe kila siku kwenye DM. Nipe namba yako tafadhali. Nataka tuwe na mawasiliano ya kawaida. Na pia, nataka nikutumie hela ya matumizi kidogo. For school, for food, for you. Hakuna masharti, just because I can.”
Moyo wa Samira ulipiga dundo la kasi. Mikono yake ilitetemeka kidogo, macho yakitua kwenye ujumbe huo kwa sekunde kumi mfululizo. Hakujua kama ni furaha, mshangao, au wasiwasi. Alifuta macho yake kidogo, akavuta pumzi.
Akajikumbusha maneno ya Lisa jana:
“Tafuta mwanaume anayeweza kukuweka mjini.”
Na Natalie: “Pesa ni muhimu mami. Ukitaka upambane na ada, tumia akili.”
Lakini bado aliwaza, “Nampa namba yangu halafu nini? Kama akinitumia hela, atanidai mapenzi? Nitakuwa nimeuza utu wangu kwa hela?”
Alishusha pumzi nyingine ndefu, kisha akaiweka simu mfukoni na kutoka kwenda chuoni.
Njiani kuelekea chuo, alikutana na wanafunzi wengine wakiwa na vifaa vya presentation—wengine wakiwa wamevaa rasmi, wengine kwa mwonekano wa kifahari. Alitembea polepole, akiwaza maisha yake. Wanafunzi waliokuwa na fedha waliweza kuchapisha slide zao kwa rangi, walibeba laptop za kisasa, na hata walikuwa na muda wa kunywa coffee kutoka kwa Food Truck ndogo iliyokuwa mbele ya chuo.
Yeye alikuwa na slide zake za maandishi ya mkono, na matumaini kuwa projector itafanya kazi.
Darasani, aliketi pembeni huku mwalimu wao, Bi. Regina, akiwaandalia presentation schedule.
“Namba tatu, Samira Said na Jonas Mwaisumbe. Andaaleni.”
Aliamka na Jonas kwenda mbele ya darasa, miguu ikitetemeka. Jonas, aliyekuwa mpole na mchangamfu, alimnong’oneza, “Samira, relax. Utafanya vizuri. Wao wote wana mavazi, lakini wewe una akili.”
Walifanya presentation yao kuhusu "The impact of gender stereotypes in rural Tanzania," na mwalimu alionekana kuvutiwa. Alitoa pongezi chache na akasema:
“Hongera. Mmeonyesha tafiti nzuri. Ingawa slide zenu hazijachapishwa vizuri, uwasilishaji ni mzuri.”
Samira alitabasamu kwa mara ya kwanza siku hiyo. Lakini furaha hiyo haikudumu muda mrefu. Baada ya kipindi, Jonas aliondoka mapema, na Samira akabaki mwenyewe. Simu yake ikaita kidogo—notification ya DM kutoka Jay Mo tena.
📩 “Samira. Sitaki kuonekana kama nasisitiza. Lakini kuna watu wanaweza kusaidia bila kutaka malipo. Mimi ni mmoja wao. Hii dunia ina maumivu mengi. Let me ease yours, even if kidogo.”
Maneno hayo yalimgusa.
Aliwaza: Hana hata namba yangu, lakini anaweza kuniambia maneno kama haya? Wanaume ninaowajua chuoni hawajawahi kusema hivi hata tukikaa pamoja siku nzima.
Alikaa kwenye bustani ya chuo, kwenye benchi lililochakaa nyuma ya library, na kufungua DM. Akatype taratibu:
“Namba yangu ni 0757 09XXXX. Lakini Jay Mo… naomba tujue mipaka. Siko tayari kwa ahadi za mapenzi. Na kuhusu hela, sihitaji kwa sasa, lakini siwezi kukataa msaada kama ni kwa moyo wa dhati.”
Alimtuma. Akahisi mwili wake ukitetemeka.
Dakika mbili baadaye, simu yake ilipiga — namba mpya ya Dar. Alishangaa, akainua macho yake, akajibu kwa tahadhari.
“Halo…”
Sauti ya kiume, ya upole, ya kuvutia, ya kijasiri ilisikika upande wa pili.
“Sauti yako… ni nzuri zaidi kuliko nilivyofikiria,” Jay Mo alisema. “Samira, asante kwa kuniamini. Sitakuangusha.”
Alinyamaza. Hakujua la kujibu.
Kisha Jay Mo akaongeza, “Na… umepokea tu M-Pesa?”
Alishtuka. Akafungua M-Pesa.
Kuna ujumbe:
Umetumiwa TZS 150,000 na 0755 XXXXX kwa jina: J.M Tech Holdings.
Samira alifumba macho.
“Jay Mo… kwa nini?” aliuliza kwa sauti ya chini.
“Kwa sababu naamini katika kusaidia mtu ambaye ana nia. Sihitaji chochote. Ila tafadhali… usijiachie. Endelea kupambana. Uko karibu sana na ndoto zako.”
Baada ya mazungumzo hayo mafupi, simu ikakata. Samira aliketi pale kwa dakika nyingine 20. Alihisi aibu, furaha, mshangao na maswali.
PENZI LA MTANDAONI
Sura ya 4:
Baada ya Jay Mo kutuma Tsh 150,000 na kuzungumza naye kwa mara ya kwanza kwa simu, moyo wa Samira ulikuwa bado haujatulia. Aliendelea kuhisi joto la maneno yake, ukarimu wake, na zaidi ya yote—ahadi ya maisha bora.
Jioni ile aliporudi bwenini, aliketi kitandani akiwa ameshikilia pochi yake ndogo ya rangi ya blue navy. Aliifungua taratibu na kutoa noti chache za elfu kumi na elfu tano. Aliziweka kwenye godoro, akazihesabu. Mara ya mwisho kuwa na kiasi kama hicho cha pesa mkononi ilikuwa miaka miwili iliyopita.
“Ni bahati yangu kutoka kwa Mungu,” alijisemea. “Na sitaiharibu.”
Siku iliyofuata, aliamka mapema tofauti na kawaida. Aliomba ruhusa chuoni kukosa darasa la mchana la Community Development Policies, kisingizio akiwa na appointment ya afya. Lakini ukweli ni kwamba moyo wake ulimvuta mjini.
Alivaa dera lake la kijani, akafunga leso kichwani, kisha akapanda daladala kutoka Kihonda kuelekea katikati ya jiji la Morogoro. Jua lilikuwa kali, lakini roho yake ilikuwa nyepesi. Alijua anaanza kujibadilisha.
Kituo chake cha kwanza kilikuwa City Style Boutique, duka dogo lililojipachika jina kubwa lakini lenye chaguo nzuri za nguo. Alizunguka ndani ya duka akiwa na uso wa kutokuamini, akishika gauni moja baada ya lingine.
“Dada, hili gauni la pinki linapendeza kweli... ni bei gani?” aliuliza huku akilitazama kwenye kioo.
“Mia saba, lakini tunakupa offer ya mia tano kwa mteja mpya,” msichana wa duka alijibu kwa tabasamu.
Samira alilitazama kwa sekunde chache, akafikiria. “Nitachukua,” alisema kwa uhakika.
Aliendelea kuchagua—top tatu za kisasa, suruali ya mlegezo wa mguu, na sketi ya jeans ya katikati ya mapaja. Alipoenda sehemu ya viatu, alipata flat shoes za kipekee, sandal nyeupe za glitters, na raba za pinki zilizokuwa on sale.
Alijua hawezi kuondoka bila kusuka.
Akaingia Salon Mariah Beauty & Styles, salon ndogo lakini maarufu inayotumiwa na wanafunzi na wake wa viongozi. Alipewa kiti mbele ya kioo kikubwa, na msusi akamuuliza, “Tutasuka nini leo dada?”
Samira alitabasamu, akasema, “Cornrows na mtindo wa Ghana weaving. Nataka kuonekana classy lakini simple.”
Wakati nywele zake zikiendelea kusukwa, alitazama kwenye kioo kwa muda mrefu. “Hivi ndivyo wanawake wa Dar huonekana?” aliwaza.
Baada ya kusuka, alisimama na kujigeuza mbele ya kioo. “Mungu wangu…” alijisemea. “Hivi ni mimi?”
Alipotoka salon, alienda moja kwa moja kwenye duka la vipodozi, Princess Beauty World. Harufu ya marashi na lotions ziliupokea uso wake.
“Habari dada, naweza kusaidia?” mfanyakazi wa duka alimsalimia kwa furaha.
“Nahitaji mafuta ya ngozi yatakayofanya ninge, niwe na glow ya kifahari,” Samira alieleza bila aibu.
Msichana wa duka alitabasamu. “Aah, hiyo ni kazi ndogo. Haya hapa ni American Dream Body Butter, hufanya ngozi ing’ae kama imelowekwa na maziwa ya asali.”
Akamwonyesha chupa ya cream yenye harufu tamu na nembo ya bendera ya Marekani.
“Kisha tumia hii Egyptian Oil Serum, unapaka usiku kabla ya kulala. Ngozi yako itakuwa smooth kama mtoto.”
Samira alikubali bila kusita. Alinunua bidhaa zote, pamoja na lip gloss mpya, foundation ndogo ya brown sugar, na eyelash za kuwekea kwa gundi.
Wakati akirudi bwenini usiku wa saa mbili, alikuwa na mikoba miwili mikubwa mkononi, nywele mpya kichwani, na mwanga usoni ambao haukuwa wa kawaida. Wasichana wa mabweni waligeuka kumtazama, wengine wakibaki mdomo wazi.
“Samira?” mmoja wao aliuliza. “Wewe ndo huyu au kuna dada yako pacha?”
Samira alicheka tu. Hakujibu mengi.
Alipoingia chumbani kwake, aliweka nguo zote kitandani, akaziangalia kwa furaha. Kisha akasimama mbele ya kioo chake cha plastiki na kusema, “Huu ni mwanzo wangu mpya.”
Alichukua simu yake, akaweka ring light aliyokuwa ameazima kwa roommate wake, na kuanza kurekodi video ya TikTok.
🎥 “Habari wapendwa, leo nataka kuwaonesha outfits tatu ninazopenda zaidi katika wardrobe yangu. Hii ya kwanza ni casual chic…”
Alibadilisha nguo moja baada ya nyingine, akicheza na kupiga poz kwa ujasiri. Kila mara alipojigeuza, alikuwa akitabasamu zaidi. Mwili wake uliweza kuvaa mitindo aliyokuwa akiiwazia miaka mingi. Urembo wake haukuwa tena wa kujificha.
Alipomaliza, aliandika caption:
"From heartbroken to glowing… Morogoro mrembo atawale. ✨❤️ #glowup #fashiononabudget #tanzaniaqueen"
Baada ya saa moja, video ilikuwa na likes 700. Asubuhi yake alipofungua app, alikuwa ameongeza followers 2,000.
Na ujumbe wa Jay Mo ulimkuta:
📩 “You look… stunning. Honestly, I’m happy I reached out to you. This is just the beginning.”
Samira alitabasamu. Hakujibu bado, lakini moyo wake ulisema, Asante Jay Mo. Asante Mungu.
PENZI LA MTANDAONI
Sura ya 5:
Mrembo Anayeng’aa
Siku zilikuwa zinaenda kwa kasi, kama upepo wa mashariki unaovuma kuelekea milima ya Uluguru. Miezi miwili ilipita tangu Samira aingie kwenye dunia ya mitandao, akiwa hajui kwamba TikTok na Instagram zingekuwa mlango wake wa kupaa kutoka maisha ya kawaida kwenda kwenye maisha ya ndoto. Na sasa, wakiwa wanaelekea kumaliza muhula wa mwisho kabla ya likizo ya miezi miwili, kila mtu chuoni alikuwa anazungumzia jina moja tu: "Mrembo wa Morogoro."
Samira alikuwa akipata followers wapya kila siku. Kila alipoweka video mpya — iwe ni ya makeup tutorial, changamoto za fashion ya bei rahisi, au POV ya msichana anayepambana — likes zilikuwa zinapanda hadi elfu kumi. Video moja aliyoiita “Maisha ya Hostel kwa Budget ya Elfu Tano” ilifika zaidi ya views laki mbili, na akaanza kupata DM za mashabiki, brand ndogo ndogo za kutaka kufanya naye promosheni, na hata wasichana waliotaka ushauri wa maisha.
Mambo yalibadilika.
Alikuwa tofauti.
Alikuwa mpya.
Na kila siku, Jay Mo alikuwa sehemu ya hilo.
“Kila saa tisa kamili mchana” — ni muda maalum ambao Jay Mo alimpigia Samira kila siku. Kama angekuwa na class, angejua Jay Mo atasubiri hadi amalize, kisha simu ingepigwa. Na usiku, kabla hajaingia kulala, Jay Mo alihakikisha anatuma voice note tamu, yenye sauti laini ya kumfariji, ya kumchekesha, au ya kumtia moyo.
Sauti yake ilikuwa na utulivu, na maneno yake yalikuwa kama mafuta ya Egyptian serum aliyokuwa akitumia—yaliteleza rohoni.
“Samira, najua dunia hii inaweza kuwa mbaya. Lakini najua pia kuna wanawake wachache sana waliobarikiwa kama wewe. Usibadilike. Bado nataka kukuona siku moja,” Jay Mo alimsisitiza katika kila mazungumzo.
Na sasa, Samira alikuwa anavutiwa.
Siyo tu kwa sauti ya Jay Mo, bali kwa namna alivyomtia moyo bila kumnyanyasa. Alimtumia hela bila masharti. Hakuwahi kumtusi. Alimuulizia leo yake ilikuwaje. Alikumbuka hata tarehe za mitihani yake. Aliwahi kumtumia bouquet ya maua kwa boda boda na ujumbe mfupi: “Glory is coming, Queen.”
Wakati huo huo, maisha ya Samira chuoni yalizidi kuchangamka. Wanafunzi waliomdharau zamani sasa walimpa nafasi kwenye group discussions. Wasichana waliokuwa wakimwita “mrembo wa mtumba” sasa walikuwa wanamuulizia “mafuta ya American Dream” aliyokuwa anatumia.
Lisa alirudi kutoka Zanzibar siku ya Jumatatu mchana akiwa na shopping bag ya D&G, na ilibidi asimame kwa Samira.
Samira alikaa mezani kwake hosteli, akiwa na laptop ya kuazima, na karatasi za kujiandaa na mitihani
Alikua ameanza kuishi kwa ratiba. Kila dakika ilikuwa na mpango. Na kila saa, alikuwa anajiona karibu na ndoto zake.
Lakini pia alianza kuhisi kitu kingine—hisia.
Siku moja usiku walipokuwa kwenye simu, Jay Mo aliuliza kwa sauti ya upole:
“Samira... nikikuambia nakupenda utaniamini?”
Samira alikaa kimya kwa sekunde tatu. Alisikia damu ikimiminika haraka kichwani. Sauti ya moyo wake ikibisha kama mlango wa chumbani.
“Sitaki kukurupuka,” alijibu kwa sauti ya chini. “Lakini niseme kweli… nafikiri nimeanza kuvutiwa.”
Jay Mo alitabasamu kupitia upande wa pili wa simu. Alisema, “Hiyo ndiyo kitu ya kwanza ambayo nimewahi kuisubiri kusikia kwa muda mrefu.”
Moyo wa Samira ulipiga kwa furaha. Alitazama kwenye dirisha lake dogo la chumba, anga la Morogoro likiwa limetulia. Alijua maisha yake hayakuwa kama ya mwanzo.
Lakini pia hakujua kuwa moyo wa msichana unapopanda juu, kuna uwezekano wa kuanguka vibaya zaidi.
SOMA MAELEKEZO
Bonyeza hi "Soma Kitabu" kisha itakupeleka kwenye fomu yaku login, hakikisha ume login na namba uliyojiunga nayo ndipo utaendelea sasa kusoma kitabu chote